2016-11-23 16:50:00

Huduma za kijamii ni matunda ya uwajibikaji wa kiimani Jimbo kuu la Tabora


Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza na kuwashukuru watawa, waamini walei na viongozi wa Kanisa wanaojisadaka bila ya kujibakiza katika sekta ya elimu, ili kuwarejeshea watu utu na heshima yao; kwa kuwajengea matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi; kwa kuwashirikisha na kuwaingiza katika mfumo wa maisha ya kijamii! Kufundisha wajinga ni sehemu ya matendo ya huruma kiroho.

Maadhimisho ya Sinodi ya kwanza ya Jimbo kuu la Tabora, Tanzania kunako mwaka 2013 yaliongozwa na kauli mbiu “Sinodi Tabora, Yesu hu seba, Yaani, Taa ya Uhai wa imani yetu! Hii ilikuwa ni fursa ya kupembua umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha na utume wa Kanisa; Uwajibikaji wa familia katika ujenzi wa Kanisa; umuhimu wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene sanjari na kujikita katika dhana ya utamadunisho, ili kweli imani iweze kumwilishwa katika uhalisia wa maisha waamini. Sinodi ilikuwa ni nafasi ya kuangalia changamoto katika ulimwengu mamboleo, hususan katika misingi ya upatanisho, haki na amani.

Sinodi ya Jimbo kuu la Tabora iliangalia kwa kina na mapana katekesi na muziki mtakatifu; umuhimu wa kulijenga na kulitegemeza Kanisa; Vyombo vya upashanaji habari katika maisha na utume wa Kanisa;  mwongozo wa Jimbo kuu la Tabora pamoja na miito mitakatifu ndani ya Kanisa. Leo katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu mkuu Paul Ruzoka wa Jimbo la Tabora, Tanzania anaangalia kwa kina na mapana mchango wa Jimbo kuu la Tabora katika kuwainua wanyonge kama sehemu ya ushuhuda wa imani tendaji.

Hivi karibuni Shule ya Viziwi Tabora imeadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake kunako mwaka 1963 inaendelea kutoa matumaini na kwamba, Kanisa linataka kuifanyia maboresho makubwa ili kwamba licha ya kutoa elimu ya msingi na ufundi, iweze pia kutoa elimu ya sekondari kwa siku za usoni. Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu mkuu Mihayo Tabora, AMUCTA ni jitihada nyingine za kuboresha mchakato wa elimu kwa watanzania wote pasi na ubaguzi. Lengo ni kuwajengea watu matumaini mapya ya maisha yao. Kanisa linatekeleza yote haya kwa sababu linabidishwa na imani yake kwa Kristo, chanzo cha uvumilivu na majitoleo yote haya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.