2016-11-21 12:06:00

Waraka wa Kitume: "Misericordia et misera": "Huruma na amani"


Hiki ni kipindi cha huruma ya Mungu kinachopania kuwaonjesha maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii: huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka na kwamba, kila mtu anaalikwa kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu katika maisha yake. Ni kipindi cha huruma ya Mungu, ili maskini na wanyonge waweze kuangaliwa kwa heshima pamoja na kujali utu na mahitaji yao msingi kwa kuzingatia mambo msingi katika maisha badala ya kugubikwa na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani. Ni muda wa huruma ya Mungu, ili wadhambi waweze kutubu na kumwongokea Mungu. Ni kipindi cha kujenga na kudumisha utamaduni wa mshikamano, udugu na upendo unaowashirikisha wote bila ubaguzi!

Ili kuweza kukabiliana na changamoto za umaskini wa hali na kipato, kila mwaka kuanzia sasa Jumapili ya XXXIII ya Mwaka wa Kanisa, itakuwa ni Siku ya Maskini Duniani, kama sehemu ya mchakato wa maandalizi ya Maadhimisho ya Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu inayofunga Mwaka wa Liturujia ya Kanisa. Hii inatokana na ukweli kwamba, Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alijitambulisha na maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii na kwamba, Siku ya hukumu ya mwisho, watu watahukumiwa kwa jinsi walivyowajali na kuwahudumia maskini. Lakini, ikumbuke kwamba, maskini ni kiini, amana na utajiri wa Habari Njema ya Wokovu. Bila ya kupambana na umaskini haiwezekani kuwa na haki wala amani! Siku ya Maskini Duniani itakuwa ni njia nyingine ya Uinjilishaji mpya inayopania kupyaisha Uso wa Kanisa katika mchakato wa kuendeleza wongofu wa kichungaji, ili kuwa kweli shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu!

Hivi ndivyo anavyoandika Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kichungaji ”Misericordia et misera” yaani ”Huruma na amani” uliotiwa mkwaju na Baba Mtakatifu mwenyewe Jumapili tarehe 20 Novemba 2016 wakati wa kufunga rasmi Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema, Mwaka wa huruma ya Mungu umekuwa ni kipindi muafaka cha kuadhimisha na kumwilisha huruma ya Mungu katika maisha na utume wa Kanisa kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu. Huruma ni kiini na muhtasari wa maisha na utume wa Kanisa unaofunua ukweli wa ndani kabisa wa upendo wa huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu anasema ”Misericordia et misera” ni maneno ya Mtakatifu Agostino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa yanayomwonesha yule mwanamke mdhambi aliyekutana na huruma ya Mungu, kiasi kwamba, udhaifu wa dhambi zake ukafunikwa upendo wa huruma, bila hukumu ya kifo iliyokuwa inamkabili yule mwanamke mzinzi! Huruma ya Mungu ikawa ni chachu ya toba, wongofu wa ndani na matumaini ili kuendelea na safari! Msamaha ni alama makini ya upendo wa Mungu uliofunuliwa na Kristo Yesu katika maisha na utume wake, hadi pale Msalabani alipowaombea watesi wake msamaha.

Huruma ni kielelezo makini cha upendo wa Mungu unaosamehe, unaopyaisha na kubadili mwelekeo wa maisha, kielelezo cha ufunuo wa Fumbo la Mungu ambao ni huruma ya milele inayowakumbatia na kuwaambata wote pasi na ubaguzi, kiasi cha kuwakirimia maisha mapya, chemchemi ya furaha na matumaini ya maisha mapya yanayovunjilia mbali ubinafsi ili kutenda wema, kufikiri vyema na kuondoa huzuni moyoni. Huu ni mwaliko kwa waamini kufanya mang’amuzi ya huruma inayowakirimia furaha, hata kama maisha bado yanasheheni matatizo na changamoto mbali mbali, ili kuondokana na utamaduni wa huzuni, utupu na upweke unaopelekea msongo wa mawazo kwa watu wengi!

Baba Mtakatifu anasema, ulimwengu unahitaji mashuhuda na vyombo vya matumaini na furaha ya kweli inayobubujika kutoka katika undani wa mtu anayefurahia uwepo wa Kristo Yesu ndani mwake! Mwaka wa huruma ya Mungu, imekuwa ni fursa kwa waamini kujichotea baraka na wema wa Mungu kwa kuwasamehe watu wake dhambi zao! Ni muda wa shukrani kwa uwepo endelevu wa Fumbo la Utatu Mtakatifu katika maisha ya waja wake kutokana na maondoleo ya dhambi, mwaliko wa kuendelea kuwa waaminifu, watu wenye furaha na ari kwa kuonja huruma ya Mungu, chachu ya mwendelezo wa mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika wongofu wa kichungaji unaopaswa kumwilishwa kila siku, ili kutangaza na kushuhudia Injili inayookoa!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kugundua utajiri mkubwa wa huruma ya Mungu unaofumbatwa katika Liturujia na Sala ya Kanisa, lakini kwa namna ya pekee katika adhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Hapa waamini wanaonja huruma na uwepo endelevu wa Kristo Mfufuka katika maisha na utume wa Kanisa; wanaonja Fumbo la Umwilisho, kielelezo cha uwepo na ushirikiano wa Mungu na watu wake katika mambo yote isipokuwa dhambi! Waamini wanaonja huruma ya Baba wa milele katika Sala ya Baba Yetu; ibada inayohitimishwa kwa kushiriki Ekaristi Takatifu, Sadaka takatifu na kumbu kumbu endelevu ya Fumbo la Pasaka, kwa ajili ya wokovu wa binadamu, historia na ulimwengu mzima!

Baba Mtakatifu anasema, huruma ya Mungu inajidhihirisha kwa namna ya pekee katika maadhimisho ya Sakramenti za Uponyaji yaani: Sakramenti ya Upatanisho na Mpako wa wagonjwa. Waamini wanapata fursa ya kusikiliza na kulitafakari Neno la Mungu kila wakati wanapoadhimisha Siku ya Bwana, changamoto na mwaliko kwa Wakleri kuhakikisha kwamba, wanaandaa vyema mahubiri yao ili kushuhudia ukweli unaosindikizwa na uzuri pamoja na wema. Wakleri wahubiri kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao juu ya upendo wa Mungu kwa watu wake. Kumbe, mahubiri na katekesi ni nguzo muhimu katika maisha ya Kanisa.

Biblia Takatifu ni maktaba inayosheheni ufunuo wa huruma ya Mungu; uwepo wa Mungu kati ya watu wake, licha ya ukosefu wa uaminifu, dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu. Biblia ni chemchemi ya imani ya Kanisa na kwa njia hii, Mwenyezi Mungu anaendelea kuzungumza na watu wake, ili Habari Njema ya Wokovu iweze kuwafikia watu wote. Waamini wajenge na kudumisha utamaduni wa tafakari ya Neno la Mungu kwa kina, yaani ”Lectio Divina” ili kuboresha na kukuza maisha yao ya kiroho.

Baba Mtakatifu anapenda kutoa mkazo wa pekee katika Sakramenti ya Upatanisho inayowaonjesha waamini huruma, upendo na msamaha wa dhambi; mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kumwilisha upendo wa Mungu katika maisha. Wamissionari wa huruma ya Mungu waliotumwa sehemu mbali mbali za dunia wamekuwa ni mashuhuda wa huruma na furaha iliyowawezesha waamini kutubu na kujipatanisha tena na Mungu. Huduma ya Wamissionari wa huruma ya Mungu itaendelezwa na Mama Kanisa na itasimamiwa na Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya.

Mapadre wanakumbushwa kwamba, utume wao wa Kipadre unajikita katika Sakramenti ya Upatanisho inayopaswa kujikita katika ukarimu, ushuhuda, huruma; ukweli na uwazi katika kanuni maadili. Mapadre wawe tayari kuwasindikiza waamini katika hija ya toba na wongofu wa ndani kwa kuonesha uvumilivu; kwa kuwa na mawazo mapana na wakarimu katika kutoa msamaha wa Mungu. Mapadre pia wanapaswa kuwa ni kielelezo cha toba na wongofu wa ndani na kwamba, Sakramenti ya Upatanisho inapaswa kuwa ni kiini cha maisha ya Kikristo kwani Mapadre ni vyombo  vya Upatanisho.

Mpango mkakati wa ”Saa 24 kwa ajili ya Bwana” kuanzia sasa utakuwa unaadhimishwa inapokaribia Jumapili ya IV ya Kipindi cha Kwaresma kama njia muafaka ya kuishi kwa undani zaidi Sakramenti ya Upatanisho. Baba Mtakatifu ana laani kwa nguvu zake zote vitendo vya utoaji mimba na kuwataka Mapadre waungamishaji kuwasaidia waamini wa namna hii wanapokimbilia huruma ya Baba wa milele kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Anawataka Mapadre wa udugu wa Mtakatifu Pio X kujitahidi kurejesha umoja kamili na Kanisa Katoliki.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, huruma ya Mungu inajikita na kufumbatwa pia katika faraja bna ukimya katika maisha na utume wa maisha ya ndoa na familia, kwa watu waliokutana, wakapendana na kufunga ndoa Kanisani, huku wakiahidi kuwa waaminifu katika maisha yao yote, lakini kwa bahati mbaya, mara nyingi ndoa inavurugwa kutokana na mateso, usaliti na upweke. Wazazi bado wanaendelea kuteseka kwa kuwa na hofu ya makuzi, malezi na maisha yao watoto wao kwa siku za baadaye. Familia ni mahali muafaka pa kumwilisha huruma ya Mungu katika uhalisia wa maisha ya waamini, dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa dhati na Jumuiya nzima ya waamini kwa kuwa na sera na mikakati makini ya shughuli za kichungaji pamoja na kukuza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Pasiwepo na mtu anayetengwa na huruma ya Mungu.  Waamini wasimame kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Wakati wa kifo, waamini waoneshe heshima yao ya hali ya juu kama inavyotokea wakati mtoto anapozaliwa, kwa kuwapatia huduma za kiroho na kuzikwa Kikristo ili kuwapatia faraja wale wote wanaosikitika na kuomboleza kutokana na kuondokewa na ndugu yao! Kanisa linapaswa kuwa karibu na wote wanaoomboleza kutokana na kifo!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, baada ya maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu, lango la huruma limefungwa, lakini mlango wa huruma ya Mungu ambao huko kwenye mioyo ya waamini bado uko wazi kwani Mungu anapenda kuwainamia ili kuwaganga na kuwaponya, changamoto pia kwa waamini kutenda hivyo hivyo kwa jirani zao kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Utekelezaji huu unaofanywa katika uaminifu na furaha; kwa njia ya huduma na mshikamano. Huruma ya Mungu inapyaisha na kumkomboa mwamini ili kuwa ni chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu anagusia pia Ijumaa ya Huruma ya Mungu iliyomwezesha kushuhudia na kuguswa na mahangaiko ya watu; kuona watu wanaojisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, changamoto ya kugundua furaha ya kuhudumia kama kielelezo cha ushuhuda wa uwepo wa Mungu kati ya watu wake. Bado kuna watu wanaoendelea kuteseka kwa njaa, kiu, ujinga, ukosefu wa fursa za ajira, makazi bora na amani, wote hawa wanahitaji huruma na faraja.

Matendo ya huruma: kiroho na kimwili yanafumbata tunu msingi katika maisha ya kijami, changamoto kwa Mama Kanisa kuendelea kumwilisha matendo haya katika maisha ya watu kwa ari kuu na moyo wa ukarimu! Kuna haja kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha utamaduni wa huruma kwa kuwa ni wasanii na wajenzi wa matendo ya huruma kiroho na kimwili yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Utamaduni wa huruma unasimikwa katika sala, toba na wongofu wa ndani kwa kuwajali na kuwahudumia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.