2016-11-20 09:18:00

Msifunge kamwe malango ya huruma, upatanisho na msamaha!


Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu inahitimisha mwaka wa Liturujia wa Kanisa pamoja na kufunga rasmi maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Liturujia ya Neno la Mungu inahitimisha kwa kumleta Yesu Kristo Mfalme wa ulimwengu mbele ya macho ya watu wa mataifa, ili kumwona huyo mteule wa Mungu asiyekuwa na utukufu, aliyetundikwa Msalabani, akavikwa taji la miiba kichwani! Akapewa fimbo ya mwanzi mikononi mwake, bila mavazi wala pete ya kifalme, bali mikono yake inafungwa kwa misumari na kuuzwa kwa vipande thelathini vya fedha!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican Jumapili tarehe 20 Novemba 2016 kama sehemu ya kufunga Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma. Anasema, Ufalme wa Yesu ni kielelezo cha wokovu na msamaha; upendo usiokuwa na mipaka, wenye uwezo wa kuponya kila jambo; ni upendo uliomwezesha Neno wa Mungu kufanyika mwili na kukaa kati ya watu wake katika udhaifu na umaskini wao wa maisha ya kimwili! Hapa duniani akaonja vitimbwi vya ukosefu wa haki, usaliti, upweke, mateso, kifo na ufufuko wa wafu! Upendo wa Kristo umeshinda na unaendelea kushinda dhidi ya dhambi, kifo na woga!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Kanisa linatangaza ushuhuda wa Kristo Mfalme wa milele, Bwana wa historia na kutokana na ukuu wa upendo wake usiokuwa na kifani na kwa vile ni Nafsi ya pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu; ufalme wake utadumu milele! Kwa furaha, Mama Kanisa anashangilia ukuu wa upendo wa Kristo unaogeuza dhambi kuwa ni neema; kifo, kuwa ni ufufuko, woga kuwa ni chemchemi ya matumaini. Changamoto kubwa ni kuhakikisha kwamba, kweli Yesu anakuwa ni Mfalme katika maisha ya waamini. Injili inaweka mbele ya macho ya waamini makundi makuu matatu ya watu: Watu waliosimama wakimtazama Yesu; Askari waliokuwa chini ya Msalaba na yule mhalifu aliyesulubiwa pamoja na Yesu.

Baba Mtakatifu anayachambua makundi haya ya watu kwa kusema, wale watu waliosimama wakimtazama Yesu, wakashikwa na bumbuwazi wasiwe na msimamo wowote katika tukio hili, ni kama inavyotokea hata kwa waamini leo hii, kushindwa kuchukua nafasi katika ushiriki mkamilifu wa Ufalme wa Yesu; kwa kushindwa kupokea kashfa ya upendo wake unaojikita katika hali ya unyenyekevu, bali watu wanaamua kukaa pembeni na kuchungulia ili kuangalia yale yatakayomsibu Yesu! Lakini, watu watakatifu wanaofuata njia yake ya upendo, kila siku wanajiuliza, Je, upendo wa Yesu unawasukuma kwenda wapi? Na wanatoa jibu gani katika maisha yao?

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kundi la pili linawajumuisha wakuu wa watu, askari na mhalifu mmoja, wanaomcheka na kumdhihaki Yesu, ili aweze kujiokoa mwenyewe ikiwa kama ni Mteule wa Mungu! Kishawishi cha Shetani anayemtaka Yesu kutenda kama wanavyotenda kadiri ya mantiki ya walimwengu, yaani ashuke kutoka Msalabani, ili awashinde wapinzani na adui zake. Wanashambulia kiini cha maisha yake, yaani upendo kwa kumtaka ajiokoe mwenyewe, ili kuonesha ukuu na utukufu wake! Hiki ni kishawishi kikubwa cha kwanza na cha mwisho katika Injili, lakini Yesu anakaa kimya, anaendelea kuonesha upendo, msamaha sanjari na kuishi mateso yake kama kielelezo cha utimilifu wa utashi wa Baba yake; upendo utakao zaa matunda!

Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanaotaka kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Yesu kujifunga kibwebwe ili kupambana na kishawishi hiki, kwa kumtaza Yesu Msalabani, ili waweze kuwa ni wafuasi wake aminifu, kwani hapa hakuna njia ya mkato katika kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, imekuwa ni fursa makini ya kuzama na kuambata mambo msingi ya imani kwa kuutazama Uso wa Kristo Mfalme unaong’ara katika Fumbo la Pasaka; pamoja na kugundua Uso mpendelevu na ujana wa Kanisa unaofumbatwa katika ukarimu, uhuru, uaminifu, umaskini wa vitu, lakini tajiri mkuu wa upendo na umissionari. Huruma ya Mungu ni kiini cha Injili kinachowahamasisha waamini kuachana na tabia ya mazoea na desturi zinazoweza kuwa ni kikwazo katika huduma ya Ufalme wa Mungu, kwa kujielekeza zaidi katika fadhila ya unyenyekevu wa Ufalme wa Kristo Yesu unaopingana na falme za kila nyakati!

Injili inamweka mbele ya macho ya waamini pia yule mhalifu aliyemwomba Yesu kumkumbuka katika Ufalme wake, baada ya kumwangalia, akajiaminisha katika Ufalme wake bila kujifungia katika ubinafsi, dhambi na historia yake ya kale na kwa njia hii anaonja huruma ya Baba wa milele. Kila wakati waamini wanapompatia Mungu nafasi anawakumbuka, anawasamehe na kusahau dhambi zao. Mungu anawakumbuka wote kwani ni watoto wake wapendwa, tayari kuwakirimia nguvu ya kusimama upya na kuendelea na safari ya toba na wongofu wa ndani.

Baba Mtakatifu anawataka waamini kamwe wasifunge malango ya upatanisho na msamaha, wawe tayari kutenda wema kwa kufungua malango ya matumaini na fursa kwa watu wengine. Hata ikiwa kama Lango la huruma ya Mungu linafungwa, lakini Moyo Mtakatifu wa Yesu, Lango la huruma ya Mungu utaendelea kubaki wazi. Moyo Mtakatifu wa Yesu uliotobolewa kwa mkuki ni chemchemi ya huruma, faraja na matumaini. Waamini wengi wamepita katika malango ya huruma ya Mungu na huko wameonja wema na upendo wa Mungu katika maisha yao.

Daima waamini wakumbuke kwamba, wamevikwa vazi la huruma ya Mungu, vazi ambalo wanapaswa kuwavika pia jirani zao, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu. Bikira Maria, Mama wa Kanisa awasindikize waamini katika safari ya maisha yao, ili waonje huruma na msamaha kama ilivyokuwa kwa yule mnyany’anyi. Kwa hakika, Bikira Maria atasikiliza na kujibu kilio cha watoto wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.