2016-11-18 15:52:00

Mtazameni Mfalme wenu anavyoning'inia Msalabani!


Tangu zamani za kale utawala wa kifalme ulishamiri sana hapa duniani. Mfalme aliweza kushika dola na kupanua utawala wake kwa kupambana vita na wa wafalme wengine. Ingawaje sasa aina hiyo ya  utawala imefifia, lakini kuna bado nchi kadhaa duniani zinatawaliwa na wafalme. Mfalme atakayebaki hadi mwisho ndiye mshindi wa kweli na wengine ni wababaishaji tu. Leo Kanisa linahitimisha mwaka wa Liturujia, na katika nafasi hiyo tunasherekea sikukuu ya Kristu Mfalme kama anavyotuandikia Luka: “Nao ufalme wake hautakuwa na mwisho.”

Ufalme ni kiini cha mahubiri ya Yesu. Katika Agano jipya wazo la ufalme limeelezwa mara mia moja na ishirini na mbili. Yesu mwenyewe amelitamka karibu mara tisaini. Lakini kwa bahati mbaya sikukuu hii ya Kristu Mfalme haieleweki hata katika kanisa kwa sababu inachanganywa na ufalme wa ulimengu huu. Kutokana na utata huo hata Yesu mwenyewe aliwahi kuingizwa karibu mara tatu na Ibilisi kwenye pilikapilika za kampeni za kuwania ufalme wa ulimwengu huu.

Mara ya kwanza Ibilisi mwenyewe alimwambia Yesu: “Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake.” Hapa Ibilisi anajitokeza kama rafiki na kumshawishi Yesu kuchukua dola. Anamwambia: “Angalia upo mbele ya dola na fahari yake. Akili unazo, mvuto kwa watu unao, nguvu unazo, fanya juu chini chukua dola. Jambo la msingi ni kunisujudia mimi.” Kusujudu ni kuyapokea mapendekezo ya Ibilisi ya kutawala, kudanganya, kunyonya, kujifikiria mwenyewe na kutafuta ukubwa kwa hila. Yesu alipokataa kugombea aina hii ya ufalme inasemwa: “Basi Ibilisi akamwacha akaenda zake kwa muda.” (Lk. 4:13) yaani akasitisha kampeni kwa muda akisubiri wakati mwafaka.

Mara ya pili, Ibilisi alijitokeza kwa njia ya binadamu: “Ibilisi akamwingia Yuda, aitwaye Iskariote, naye ni mmoja wa wale Thenashara, akaenda kwa Wakuu wa makuhani na majemadari jinsi atakavyoweza kumtia mikononi mwao.” (Lk. 22:3-4). Hawa ndiyo watawala wa ulimwengu huu wanachama wanaofuata mapendekezo na sera za Ibilisi. Mara ya tatu, ndiyo katika Injili ya leo Yesu akiwa msalabani. Msalaba huo  ndiyo ni alama ya kuapishwa Yesu rasmi na kuishika dola yaani kutawala ulimwengu huu kadiri ya fikra za kimungu. Katika shamrashamra hizo za kuapishwa huoni alama yoyote ile ya kifalme kadiri ya mawazo na fikra za walimwengu. Kwa mfano kuhusu mahala, kwa kawaida wafalme au maraisi wanaapishwa Ikulu au uwanja wa Taifa na hapo kunakuwepo na mbwembwe za kukata na shoka! Lakini Yesu anaapishwa Mlimani Kalvari mahali pa kuwaadhibu wahalifu. Kiti chake cha kifalme ni Msalaba na kupigiliwa misumari. Mashahidi wake ni wevi wawili, halafu wapambe wa sherehe za kutawazwa mfalme, wanaomzomea, na kumdharau. Urujuani ni rangi rasmi ya mavazi amayovaa mfalme siku ya kusimikwa. Lakini Yesu yuko uchi wa nyama. Aibu yao milele!

Hapa ndipo inapogota imani ya Wakristo, imani inayofumbatwa katika Fumbo la Msalaba, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa wa Kristo Yesu kutoka wafu! Binadamu daima tunauelekea ufalme unaotuvuta kwa sasa hivi, ufalme unaofumbatwa katika mambo ya mpito na tunadhani huo ndiyo utakaoshinda na kudumu. Ili kutuelewesha vizuri zaidi tofauti za falme hizi, Luka anatuletea makundi matatu ya watu waliokuwa pale Kalvarini wakimtazama Yesu anavyotawazwa mfalme.

Kundi la kwanza ni la watu wa kawaida na maskini “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” ambao Mwinjili Luka anawaonea huruma na kutaka kuwaonesha Uso wa huruma ya Baba wa milele. “Wakasimama wakitazama.” Watu hao wamesimama tu na kushangaa kwani hawaelewi kinachoendelea. Wamepigwa na bumbuwazi! Makuhani ndiyo wataalamu wanaolijua Neno la Mungu linaloeleza kwamba Mwana wa Daudi ndiye Mfalme wa kweli naye hana budi asulibiwe na kufa msalabani. Lakini makuhani hawa hawakuelewesha watu hawa. Sasa wamesimama, wamepigwa butwaa na kujipiga vifua vyao. Kwa hiyo makuhani, hawana budi wajifikirie wajibu wao wa kuelewa na kuelewesha tofauti iliyoko kati ya ufalme wa huruma na upendo wa Yesu anayetoa maisha yake kwa ajili ya wengine na ufalme ule wa kuangamiza maisha ya wengine. Huu kwa maneno mengine ni ufalme wa milele yote na wa ulimwengu mzima; ufalme wa kweli na uzima; ufalme wa utakatifu na neema; Ufalme wa haki, amani na mapendo kwa wote pasi na ubaguzi, kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu!

Kundi la pili ni la Wakuu wanaomcheka wa kudharau aina hiyo ya ufalme unaotundikwa juu ya mti wa Msalaba na kusahau kwamba, hapa ni mahali ambapo pametundikwa hekima, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake!: “walimfanyia mzaha, wakisema, ‘Aliokoa wengine; na ajiokoe mwenyewe, kama ndiye Kristo wa Mungu, mteule wake.” Hapa ndiyo wakati mwafaka Ibilisi anapojimwilisha katika wakuu, wanamhoji Yesu kwa nini hashuki Msalabani. Yesu angeshuka Msalabani mara moja angeshika dola, na angewasadikisha watu wote kuwa Mungu ndiye mwenye nguvu na angeepa kuuawa kikatili na hapo bila shaka wangeshikishwa wote adabu!. Yesu angefanya hivyo angeharibu kabisa sura kweli ya Ufalme Mungu aliyotakiwa kuionesha hapa duniani yaani sura ya Mungu aliyefika kutumikia na siyo kutumikiwa.

Kundi la tatu ni askari waliokuwa wanafahamika kwa kutoa mkong’oto wa ngutu! Usiombe kukutana na Askari watesaji wa Kirumi ni afadhali kugongwa na Treni! “Askari nao wakamfanyia dhihaka wakimwendea na kumletea siki, wakisema: Kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi, ujiokoe mwenyewe.” Hii ni lugha ya watu maskini, kwa sababu askari hawa hawakuwa Warumi kama tunavyodhani. Askari hawa walitokea Assiria makao yake makuu yalikuwa Antiokia ndani ya utawala wa Kirumi. Kama ilivyo kawaida kwa askari au polisi wanafanya kazi mbali na familia zao, na wake na watoto wao. Hawapati haki zao inavyotakiwa, mshahara kidogo, na mazingira yao ya kazi ni magumu. 

Kwa hiyo wanalazimika kufanya kazi bila kuridhika, na mapato yake wanatumia nguvu na mamlaka ya piga ua, na kuwanyima watu haki zao za kibinadamu na hata haki za dini zao. Mfano ni pale walipomshurutisha Simoni wa Kirene kubeba msalaba wa Yesu bila kumwomba, bali walimshikiza kwa nguvu kwani wanaamini kwamba ulimwengu hauwezi kwenda bila kutumia nguvu na mabavu. Hata wao wanapokumbwa na kizaazaa cha ulimwengu wa kale wa kuonewa inawabidi kutumia nguvu kujiokoa. Katika nafasi hii wanajaribu kumwonea Yesu huruma wanampendekezea kujisalimisha mwenyewe. Hapa Ibilisi amejimwilisha kwa askari hawa wanaopendekeza Yesu aaminie nguvu zake na kujiokoa mwenyewe na siyo kuwaokoa wengine.

Aidha imeandikwa: “Na juu yake palikuwa na anwani: “Huyu ndiye Mfalme wa Wayahudi.” Hii nayo ni kebehi ya fikra za kifalme za wana wa ulimwengu huu, waliobobea katika dhana ya mtima nyongo!. Hii ndiyo alama ya ufalme alioutaka Mungu unaoweza kujibu wivu na chuki kwa upendo. Upendo huo ni kama ule wa Bwana arusi. Hutuonesha utukufu wa Bwana arusi yule aliyempenda Bi arusi wake binadamu. Bwana arusi huyo alifanikiwa kutuelewesha jinsi gani anampenda binadamu. Kwamba chochote utakachomfanyia yeye Bwana Arusi atakulipa kwa upendo tu. Hiyo ni sura ya Mungu anayempenda mtu. Unapomtafakari mtu huyo baada ya kufa kwake unajua anatuambia Mungu ni nani, kwani yote yamejieleza katika upendo. Kwamba huyo ni mwanakondoo aliyetumwa kati ya mbwa mwitu. Padre anaposema: “Tazama, mwanakondoo wa Mungu,” hapo unatakiwa kufanya uchaguzi kati ya ufalme wa ulimwengu huu au Ufalme wa mwanakondoo, tayari kushiriki katika mchakato wa ujenzi wake kwa ushuhuda unaojikita katika misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano!

Msalabani walikuwa pia wevi wawili. Mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, “Je, wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi.” Kwa mara nyingine inarudia “Jiokoe wewe mwenyewe. Jifikirie mwenyewe.” Hapa kila mtu anaishi kwa falsafa ya kivyake vyake tu! Hapa tena Ibilisi anajimwilisha kwa majangili wanaomtaka Yesu afikiri kama wao. Jangili huyu anafikiri kwamba watu wote ni majambazi na kazi yao ni kudhulumu na kutoa maisha ya wengine! Hawa mapanga shaaaaa, ni kama kazi; ogopa kukutana nao, utakiona cha mtema kuni!  

Jambazi mwingine hapokei pendekezo hilo anasema: “Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu hiyo hiyo?” Yaani hujui mpango wa Mungu juu ya binadamu. “Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lolote lisilofaa.” Anamtaja Yesu kwa jina “Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.” Kitendo cha kumtaja mwingine jina lake analostahili ni muhimu sana. Hiyo ni sala nzuri anayotufundisha jambazi ambayo inabidi kuitafakari na kuimwilisha katika uhalisia wa maisha! Jambazi huyu anatambua na kuona Uso wa huruma ya Mungu kwa binadamu anataka kuambata upendo na huruma hii katika maisha ya uzima wa milele! Hata katika mateso yake, anajitambua kuwa ni mkosefu na anahitaji kuonjeshwa huruma na upendo wa Baba wa milele!

Kwa sababu sisi tunawadhulumu watu wengine kwa namna moja au nyingine, kwa wivu, hila, uwongo, wizi, udhulumu, rushwa, ufisadi, nk jambazi huyu anatuwakilisha sisi sote. Kwa hiyo sisi tulio majangili mambo leo, inatubidi tutoe ushahidi wa ufalme na ukuu ule wa Yesu na kumwomba Yesu aliye katika ufalme wake, atukumbuke na kutuokoa na ulimwengu huu wa madhulumu usio wa haki, ambao hata yeye alishawishika na akatuingize katika ulimwengu wake, hivi tusali daima kama yule jangili: “Ee Yesu unikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.”

Yesu anamjibu: “Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi.” Yesu alipoingia hapa duniani, hakupokewa na watakatifu bali wakosefu. Hawa ndiyo walibahatika kuwa na mang’amuzi ya kwanza, na watu wa mwisho ni hawa majangili. Hao ndiyo wanatuwakilisha sisi, kuchagua ufalme wa kweli. Neno hilo peponi ni picha inayotokea mara tatu katika agano jipya, ndiyo hatima ya maisha yetu. Ambako sisi sote tutapokewa. Lakini bustani hiyo itakuwa kwa wale waliochagua ufalme ule wa kutumikia kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Nao ufalme wake hautakuwa na mwisho.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.