2016-11-17 09:06:00

Jengeni Ufalme wa Mungu katika haki, amani, upendo na mshikamano!


Leo Jumapili ya 34 ya Mwaka,tarehe 20 Novemba 2016, Kanisa linaadhimisha sherehe ya Yesu Kristo Mfalme, Bwana wa mbingu na nchi. Jumapili hii ni ya mwisho katika kalenda ya Liturujia ya Mwaka wa Kanisa. Kwa mwaka huu, Sherehe hii inabeba uzito wa pekee kwani, Baba Mtakatifu Francisko anafunga rasmi maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, tayari kwa Wakristo kuendelea kushuhudia neema na baraka walizojichotea wakati wa maadhimisho haya, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu!

Kadiri ya utaratibu wa kalenda ya kanisa, mwaka wa kanisa huanza na jumapili ya kwanza ya majilio na kilele chake ni jumapili hii ya leo tunapoadhimisha sherehe ya Yesu Kristo Mfalme. Leo hii tunayo kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kumaliza mwaka salama, mwaka wa kanisa na tunamwomba tena baraka zake tunapojiandaa kuanza mwaka mpya wa kalenda katika liturjia yetu. Sherehe hii iliwekwa rasmi kuadhimishwa na Kanisa lote na Baba Mtakatifu Pio wa XI, 1925 na lengo likiwa na kusherehekea utukufu wa Yesu Kristo. Katika Waraka wake wake mwa kitume  “Quas Primas” wa 11/12/1925 – aliandika; watu watafute amani ya Kristo katika ufalme wa Kristo. Hivyo tunasherehekea sikukuu ya Yesu Kristo Bwana wa mbingu na nchi. Enzi na utawala vyote ni vyake.

Sherehe hii  iliwekwa rasmi na Baba Mtakatifu Pio wa XI dhidi ya wapinga uwepo wa Mungu, waliodai utawala wa kiimla.  Tupate tafakari chache toka maandiko matakatifu juu ya ukuu huu wa Mungu kama ulivyotangazwa na Kristo ili itusaidie kuelewa ukuu wa sherehe hii na wajibu wetu mbele ya Mungu. Katika Waraka kwa: Kol. 1,19 – tunasoma hivi – kwa maana Mungu alipenda utimilifu wote ukae ndani yake. Katika  Waraka: Kol. 2,9 – tunasoma juu ya ukuu wa Kristo na kazi yake – maana utimilifu wote wa umungu umekaa ndani yake, hata mwilini mwake. Akiongea na wafuasi wake katika Injili: Mk. 9,1 anasema – pia aliwaambia, amin, nawaambieni, baadhi ya hawa wanaosimama hapa hawataonja mauti kabla ya kuona ufalme wa Mungu unakuja kwa enzi. Katika Injili ya: Yoh. 1,51 – akizungumza na Nathanaeli – akamwambia, amin, amin, nawaambieni mtaziona mbingu zimefunguka na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Mtu.

Katika Kitabu cha Ufunuo. 21:1-3 – tunasoma habari juu ya mbingu mpya na nchi mpya – niliona mbingu mpya na nchi mpya kwani mbingu ya kwanza na ulimwengu wa kwanza vilikuwa vimepita, pia bahari haikuwa  tena. Niliona mji mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu. Umetayarishwa kama bibi harusi aliyejipamba kwa ajili ya mume wake. Nikasikia sauti kubwa kutoka kiti cha enzi ikisema, tazama hema ya Mungu kati ya wanadamu. Naye atakaa kwao, nao watakuwa taifa lake na Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao.

Kupitia huku kuumbwa upya, sisi tunaweza kumwabudu Mungu katika roho na kweli kwani awataka hao wanaomwabudu – Yoh. 4: 23-24 – lakini saa inakuja na ndiyo sasa, waabudu wa kweli wamwabudu Baba katika Roho na ukweli, kwa maana Baba hutafuta watu wamwabuduo hivyo. Mungu ni Roho, basi, wamwabuduo wamwabudu katika Roho na Ukweli. Katika Waraka wa 1Yoh. 3;9 – tunasoma habari ya uwepo wa ufalme wa Mungu kati yetu – kila aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu mbegu ya Mungu imo ndani yake. Huyo hawezi kutenda dhambi, kwa sababu amezaliwa na Mungu. Zawadi hii ya ubatizo yatufanya watoto wa Mungu hapa ulimwenguni.

Katika Injili: Lk. – 17; 20-21 – juu ya habari ya ujio wa ufalme wa Mungu – aliulizwa na Mafarisayo, ufalme wa Mungu utakuja lini? Akawajibu, ujio wa ufalme wa Mungu hauna majira yake, wala haiwezekani kusema, upo hapa, au uko kule. Kwa maana ufalme wa Mungu uko miongoni mwenu. Sasa sisi tuangalie maisha yetu na imani yetu. Je inaendana na fundisho hili na uelewa huu wa Yesu? Je tunashiriki kikamilifu katika ujenzi wa ufalme wa Mungu? Maana yake nini ufalme huu? Hakika ni mfalme wa mioyo yetu – mfalme wa upendo na huruma, mfalme wa haki na amani, ni mfalme wa uhuru na maisha.  Ufalme wa Mungu unajengwa na jamii ya wale wenye kumkaribisha Mungu maishani mwao. Kila siku tunasali na kuomba – ufalme wako ufike, utakalo lifanyike duniani kama mbinguni … nasi leo twaitwa kuishi ufalme huo katika akili zetu, mioyo yetu na nafsi zetu, huku tukitimiza mapenzi yake Mungu. Sherehe hii inatupatia nafasi ya kukumbuka juu ya ukweli huu.

Yesu Kristo ni Mfalme wa wafalme, Bwana wa mabwana. Wanaofanya ufalme huo ni wabatizwa. Kila jema tutendalo, lina ujenga huu ufalme. Ufalme huu haupimwi na wingi wa mambo ya nje – idadi ya wakristo, uzuri wa majengo, wingi wa vitu. Hujengwa na mkristo na jumuiya inayoishi na kushika amri za Mungu na kutimiza mapenzi yake. Hujengwa na familia/jumuiya inayopendana, inayosali pamoja, inayomtukuza Mungu – watu na jumuiya iliyowekeza kwenye ukweli, inayoelewana, inayoshirikiana, inayohudumiana kindugu. Hizi ndizo baadhi ya sifa za ufalme wa Mungu na ambazo dunia inataka kupata kutoka kwetu sisi waamini. Hatuna budi kuungana na mtume Paulo katika somo la pili anapotualika kumshukuru Mungu Baba, aliyetustahilisha kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru. Naye alituokoa katika nguvu ya giza.

Sherehe hii inatupatia nafasi ya kuchagua tena kukaa pamoja na Mungu. Askari walimdhihaki – Lk. 23,36 – mmoja wa wale wahalifu waliotundikwa alimtukana akisema, je, wewe si Kristo? Basi jiokoe mwenyewe na sisi pia. Lakini yule mwingine alisema – Lk. 23: 41-42 – sisi kwa haki, tunapokea tuliyostahili kwa makosa yetu, huyu lakini hakutenda mabaya. Akasema, Ee Yesu, unikumbuke mimi unapofika katika ufalme wako.

Ndugu zangu, tunakumbushwa kuwa haitoshi tu kurudia kwa maneno kumwita Mungu au kutaja buru jina lake, yahitaji matendo, yaani kumshuhudia Kristo kweli kweli. Tutafakarishwe na maisha ya ushuhuda ya Mtakatifu Thomas More. Katika maisha yake alikuwa mtumishi wa serikali na mwandishi mashuhuri wa vitabu vya elimu dunia na mbingu. Huyu alipinga waziwazi nia na tamaa mbaya ya mfalme ya kumtaliki mke wake wa ndoa ili apate kuoa mwanamke mwingine. Mtakatifu huyu alipokuwa anapalekwa kuuawa alisema mimi ni mtumishi mwaminifu wa mfalme, lakini kwanza ni mtumishi mwaminifu wa Mungu.

Tumsifu Yesu Kristo. Pd. Reginald Mrosso,C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.