2016-11-16 09:30:00

Ujumbe kwa Siku ya Wavuvi Duniani, 2016


Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 21 Novemba, inaadhimisha Siku ya Wavuvi Duniani”. Lengo la maadhimisho haya ni kutambua mchango unaotolewa na Jamii ya wavuvi katika mchakato wa shughuli za kiuchumi na kijamii, lakini pia kuona mazingira magumu ya maisha na kazi, ili wote kwa pamoja waweze kusimama kidete kulinda na kutunza rasilimali na utajiri mkubwa unaopatikana katika sekta ya uvuvi kwa maisha na ustawi wa watu wengi zaidi. Sekta ya uvuvi inatoa lishe kwa mamillioni ya watu duniani na inakadiriwa kwamba, inatoa fursa ya ajira kwa watu zaidi ya millioni 50 sehemu mbali mbali za dunia.

Kutokana na umuhimu wa sekta ya uvuvi katika maendeleo ya watu, Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, limetoa ujumbe unaogusia kwa namna ya pekee kabisa hali ngumu na hatarishi wanayokabiliana nayo wavuvi katika maisha na kazi yao. Hili ni kundi la watu wanaonyanyasika na kudhulumiwa sana kutokana na uwepo wa mtandao wa makundi ya kihalifu yanayoendelea kuwatumbukiza wavuvi hawa katika dimbwi la umaskini wa hali na kipato licha ya kuwa ni wachangiaji wakuu katika mchakato wa uchumi duniani.

Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, linazitaka Serikali mbali mbali duniani kuhakikisha kwamba, zinatia sahihi kwenye Mkataba wa Kazi ya Uvuvi wa Mwaka 2007, ili itifaki hii iweze kuanza kutekelezwa. Katika maadhimisho ya Siku hii, hapo tarehe 21 Novemba, 2016 mjini Roma kwenye Makao Makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO kutafanyika kongamano linaloongozwa na kauli mbiu “Ukiukwaji wa haki msingi za binadamu katika sekta ya uvuvi pamoja na uvuvi haramu". Haya ni mambo yanayochangia uharibifu na uchafuzi wa mazingira pamoja na uharibifu wa mazalia ya samaki.

Kongamano hili limeandaliwa na FAO kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum pamoja na mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Mashirika ya Chakula na Kilimo ya Umoja wa Mataifa mjini Roma. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican na Kardinali Antonio Maria Vegliò, Rais wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum ni kati ya viongozi wakuu wa Kanisa wanaotarajiwa kutoa hotuba katika maadhimisho ya kongamano hili!

Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum linasikitika kusema kwamba, sekta ya uvuvi ni kati ya sekta zinazokabiliwa na idadi kubwa ya ajali kazini na kiwango kikubwa cha vifo vya wavuvi; hali ya kunyanyaswa na kudhulumiwa haki zao msingi. Hii ni sekta ambayo ina idadi kubwa ya waathirika wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; watu wanaolazimika kufanya kazi za shuruti kwenye meli za uvuvi duniani, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete ili kuvunjilia mbali mnyororo wa umaskini, utumwa na nyanyaso dhidi ya utu na heshima ya binadamu! Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha walimwengu kwamba, biashara ya binadamu ni uhalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu, changamoto kwa watu wote wenye mapenzi mema kujifunga kibwebwe ili kupambana na tabia hii, kwa kuwapatia haki ya kimataifa na usalama waathirika wa matukio haya dhidi ya utu wa binadamu.

Mama Kanisa anawapongeza na kuwashukuru viongozi wa maisha ya kiroho; utume wa bahari wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wavuvi na familia zao. Wanahamasishwa kuendeleza utume wao katika sekta ya uvuvi, ili kuwasaidia wavuvi na waathirika wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Wasaidie kutoa elimu kwa wavuvi ili wasitumbukie wala kutumbukizwa kwenye biashara haramu ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.