Ndugu yangu msikilizaji wa Radio Vatican, katika Maandiko Matakatifu Yesu anatuambia, tufanyapo sherehe au karamu, yatupasa kuwaalika; maaskini , vilema, na hata wasiojiweza (Lk 14:13) kwa mtazamo huu kila mkristo anapaswa kutambua utume wake katika kuwajali maskini na wasiojiweza. Yesu ameshatuonyesha njia, hasa pale alipoanza utume wake kwa maneno haya: Roho wa Bwana yuu juu yangu, kwani amenipaka mafuta kuwahubiria maskini Habari Njema, wafungwa kufunguliwa kwao, kuwatangazia vipofu kuwa wanaweza kuona tena, kuwaweka huru wanaonewa na kutangaza mwaka wa bwana uliokubalika (Lk 18:19). Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, yametuwezesha kuwaona na kuwajali maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa kutambua kwamba, maskini ni lengo, amana na utajiri wa Kanisa kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.
Mtakatifu Francisko wa Assisi aliwahi kusema ‘Lengo la kuishi kwangu ni kuishi kama Yesu anavyoishi na kuhubiri kama Yesu anavyohubiri” matamanio haya yanatakiwa yatutafakarishe sana, tena tutafakari tukitambua kuwa Yesu ameshatupa njia, namana ya kuishi na namna kuhubiri. Hivyo kwa mifano na matedo ya Yesu tuwafikie sasa wale wote wanaoteseka , labda kwa njaa, vita, kukosa haki, kukosa elimu bora zaidi, wagonjwa, vilema, waliokataliwa na waliokosa matumaini. Kwani ni katika kuwafikia watu hawa na kuwatangazia Habari Njema watapata kushiba furaha nafsini mwao na watapata uponyaji wa kimungu nafsini mwao. Kwa maneno mengine, tunasukumwa na Mama Kanisa kuendelea kumwilisha imani katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama ushuhuda wa imani yetu kwa Kristo na Kanisa lake! Ikumbukwe kwamba, imani bila matendo, hiyo imekuwa na wala haina mvuto wala mashiko kwa watu!
Baba Mtakatifu Francisko, katika Waraka wake wa kitume Furaha ya Injili anatuambia, kila mkristo na kila jamii inaitwa kuwa dhana ya kimungu katika kuwahudumia na kuwasaidia maskini , na zaidi kuhakikisha kuwa wanakuwa sehemu ya jamii. Pia anaendelea kusema kazi ya upendo ielekeayo kwa jirani zetu ni mojawapo ya ukamilifu wa maonyesho ya ndani ya neema ya kiroho. Wakati huu pia, tukumbuke, ndiyo wakati uliokubalika ambapo Kanisa linaadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilee ya huruma ya Mungu, hivyo, tujitahidi zaidi na zaidi kuwasogelea na kuwasaidia maskini na wasiojiweza, na kwa kufanya hivyo tutajiongezea neema. Hakima ya biblia inatuambua; yeyote aliyemkarimu kwa maskini anaelekea kwa Bwana na Bwana atayazawadia matendo yake c( Methali 19:17).
Ndugu zangu, tuadhimishapo mwaka mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, tumtembelee Yesu katika maskini, wasiojiweza, wenye njaa, wanyonge,wagonjwa wahanga wa matetemeko, vita na majanga mengine ya maisha. Kwani kwa kufanya hivi ndiko kumtembelea Yesu kama mwenyewe alivyosema,; Maana nilikuwa na njaa nanyi mkanipa chakula; nilikuwa na kiu nanyi mkanipa maji; nilikuwa mgeni nanyi mkanikaribisha; nilikuwa uchi nanyi mkanivika, nilikuwa mgonjwa nanyi mkaja kunitazama, nilikuwa gerezani nanyi mkaja kunitembelea.(Mt 25 :35-36).
Huu ni wito wa kuwajali wengine katika Kristo na pia ni habari njema kwa watu wote. Ni mwaliko wa kuambata na Yesu pia katika Neno na Sakramenti zake, ili kuonja upendo unaobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na toba, msamaha na maondoleo ya dhambi yanayobubujika kutoka kwa Kristo chakula cha uzima na Uso wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Neema na baraka za Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ziendelee kutuambata na kutusindikiza katika maisha, ili kweli tuweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa watu wa nyakati hizi!
Na Padre Agapito Amani, O.S.S.
Shirika la Mapadre wa Kazi ya Roho Mtakatifu.
Roma.
All the contents on this site are copyrighted ©. |