2016-11-14 15:22:00

Malango ya huruma ya Mungu nchini Italia!


Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu unapoelekea kileleni, milango mitakatifu katika Makanisa makuu ya majimbo imefungwa rasmi, Jumapili iliyopita 13 Novemba 2016. Nchini Italia baadhi ya maaskofu wameadhimisha Misa Takatifu katika makanisa makuu, na kuwahasa waamini juu ya baadhi ya mambo msingi ya neema zilizosheheni ndani ya huruma ya Mungu.

Kardinali Angelo Scola, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Milano, amewaalika waamini kuelimika ili kufuata mtazamo na hisia za Kristo, kupitia matendo ya Huruma. Jimbo kuu la Milan lenye madhabahu ya Kiambrosiani limeanza tayari kipindi cha majilio. Naye Kardinali Angelo Scola, kawaalika kukiishi vema kipindi hicho cha matumaini, sababu watu wengi barani Ulaya wanaonekana kuishi kwa kuchoka na kukata tamaa. Amewatahadharisha pia wote kuwa makini na vishawishi, hadaa, udanganyifu, ibada za sanamu, mateso ya nje na mahangaiko ya ndani, wazingatie kifo dini cha ndugu wengine katika imani, na umuhimu wa kumfanya Kristo afahamike duniani kote.

Kardinali Gualtiero Bassetti, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Perugia, akiadhimisha Misa Takatifu kwa ajili ya kufunga mlango mtakatifu wa Kanisa kuu la Perugia, kawaalika waamini kukumbuka matokeo mengi yaliyotokea katika mwaka huu mtakatifu wa Huruma ya Mungu, na mengine yanayoendelea kutokea. Matukio hayo ikiwa ni pamoja na machafuko, vita, magonjwa, matetemeko ya ardhi, wahamiaji na wakimbizi na kadhalika. Matukio na tabia za baadhi ya wanadamu leo, vinaashiria utabiri wa nyakati za mwisho. Pamoja na matokeo hayo yote, Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika kulinda na kutetea haki za watu, kutafuta amani, kufariji na kuwasaidia wahitaji. Hivyo Kardinali Gualtiero Basseti, anawaalika waamini kuendelea na moyo wa ukarimu na wema, ili wao pia waweze kufaidika na Huruma ya Mungu, kwa namna ya pekee siku ya hukumu, kwani kwa wale wema na waaminifu, jua la haki litang’ara juu yao, na dunia itafanywa upya kwa ajili yao.

Kwa upande wa Jimbo la Macerata, waamini wamealikwa kujitambua katika umoja wao na mahusiano yao na Mungu. Katika Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu, walijikosoa makosa yao, wakajipatanisha, na Mungu akawasamehe. Hivyo ishara ya kufunga mlango mtakatifu, iwe ishara ya kufunga mambo ya kale, makosa na dhambi za kabla, ili kuanza hija ya imani kuelekea kutenda na kuishi yale tu yaliyo mema.

Kwa Jimbo kuu la Spoleto-Norcia, Askofu mkuu Renato Boccardo, amewaalika waamini kutoka kwenye mlango mtakatifu wa Kanisa kuu, ili kukutana na watu kwa ishara zenye upendo wa Huruma na kujali. Kwa namna ya pekee, kawaalika kuifungua mioyo yao kila mmoja kujali mahitaji ya wahanga wa tetemeko la ardhi lililowakumbuka maeneo hayo mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2016. Amewaalika kutambua kwamba, matukio haribifu ya asili na matukio mengine yanayomtesa mwanadamu, yasiwafanye kukata tamaa, bali yawe ni fursa ya kuwafanya kukomaa kiimani. Changamoto za dunia ya leo, haziwezi kukabiliwa kwa maendeleo ya sayansi na teknolojia peke yake, bali ni muhimu kuishi maisha stahiki ya kikristo, ikiwa ni pamoja na ukarimu na upendo, amesema Askofu mkuu Renato Boccardo. Kwa ufupi, kufunga milango mitakatifu katika makanisa makuu, sio mwisho wa kuishi na kunufaika na Huruma ya Mungu, bali ni mwanzo wa kuzama kwa kina katika kushuhudia upendo na huruma ya Mungu kila siku, wakati huo huo kujikita katika hija, upatanisho, tafakari ya Neno la Mungu, maisha ya Sala na Sakramenti.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.