2016-11-14 14:47:00

Hija ya huruma ya Mungu bado inaendelea katika nyoyo za watu!


Katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, milango mitakatifu ya Makanisa makuu na madhabahu imeanza kufungwa rasni hapo tarehe 13 Novemba 2016. Kwenye Kanisa Kuu la Bikira Maria mkuu, liliko mjini Roma, Jumapili iliyopita, mlango Mtakatifu wa Kanisa hilo umefungwa. Kardinali Abril Castello anasema: pamoja na kufungwa mlango huo mtakatifu, hija ya Kanisa bado inaendelea katika mioyo ya waamini na katika jumuiya zao, na Huruma yenyewe ya Mungu haifungwi wala kupungua. Kardinali Abril Castello, amemwakilisha Baba Mtakatifu Francisko, katika adhimisho la Misa Takatifu la kufungua mlango Mtakatifu katika Kanisa la Bikira Maria mkuu.

Hija ya mwanadamu duniani imejaa mahangaiko na mateso mengi, ambapo kupitia hayo yote anapata fursa ya kuutafakari upendo uliopo katika kujibu, maamuzi ya Mungu kukutana na mwanadamu na kumsamehe, ili kurudisha ndani yake hali ya kufuata mapenzi ya Mungu, katika historia ya wokovu. Upendo huo, lazima ushirikishwe kwa wengine kama ndugu. Yaani kila mwamini anapohangaikia mkate wake wa kila siku, yeye mwenyewe awe mkate wa kushirikisha wengine (Rej., 2Wathesalonike 3, 12).

Waamini wabatizwa ni hekalu la Roho Mtakatifu. Wanaalikwa kujihoji wakati wa mwaka mtakatifu wa Huruma ya Mungu, walifungua vipi milango ya mioyo yao kwa ajili ya wengine. Milango ambayo haipaswi kufungwa, hata kama mwaka mtakatifu wa Huruma ya Mungu unaelekea kileleni na milango mitakatifu kufungwa, kwani milango ya makanisa ni ishara tu, wakati milango ya mioyo ya waamini ni uhalisia wa mlango wa huruma, ambao unapaswa ubaki wazi na kushuhudia Huruma ya Mungu siku zote, Huruma ambayo haifungwi wala haifikii kikomo.

Katika hija ya waamini duniani, wajifunze kutoka kwa Bikira Maria, na waongozwe na mkono wake wa kimama, yeye mama wa huruma, atawasaidia kwa maombi kufungua mioyo yao kuelekea upendo na huruma ya Mungu, amesema Kardinali Abril Castello. Sikukuu ya Kristo Mfalme, tarehe 20 Novemba 2016 ndiyo itakuwa siku ya kilele ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, ambapo Baba Mtakatifu Francisko, ataadhimisha kilele hicho katika Kanisa kuu la Mt. Petro mjini Vatican na kuufunga Lango la Huruma ya Mungu katika Kanisa hilo, Lango lililofunguliwa katika maadhimisho ya Sikukuu ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili, tarehe 8 Desemba 2015.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.