2016-11-12 15:15:00

Upendo wa Mungu ni shirikishi unawaambata wote!


Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi hiki cha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ameendelea kukazia umuhimu wa huruma ya Mungu inayofumbatwa katika upendo shirikishi, ili kuwakirimia watu wanaoteseka na wanaoelemewa na mizigo pumziko kwa Kristo Yesu. Mwenyezi Mungu katika mpango wake wa upendo, hataki kumtenga mtu awaye yote, kwani upendo wake unawakumbatia na kuwaambata wote. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, waamini wanazaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu na hivyo kufanyika kuwa ni wana wa Baba wa milele.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 12 Novemba 2016 wakati wa katekesi yake amesema, huruma ya Mungu ni kipimo, mtindo wa maisha na utendaji wa Mkristo unaowashirikisha wote badala ya kujifungia katika mbinu za usalama wa kibinafsi. Yesu anawaalika wote wanaoelemewa na mizigo pamoja na masumbuko ya maisha kwenda kwake ili waweze kupata pumziko pamoja na kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha ya binadamu. Ni jukumu la waamini kujiaminisha na kufungua malango ya mioyo yao kwa Kristo Yesu, ili kupokea ujumbe wake wa upendo unaowaingiza katika Fumbo la Ukombozi.

Yesu amenyoosha mikono yake, ili kuwapokea na kuwakumbatia wote bila kuwabagua kutokana na hali yao ya kijamii, lugha, rangi, tamaduni au dini ya mtu. Mbele ya Wakristo wamwone mtu anayepaswa kupendwa kama anavyopenda Mwenyezi Mungu katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Ubaguzi wa aina yoyote ile ni kinyume cha mpango wa upendo wa Mungu kwa binadamu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, leo hii kuna watu ambao wamechoka na kuelemewa na mizigo huko majumbani, maofisini na mahospitalini wote hawa wanahitaji kuonjeshwa huruma ya Mungu katika maisha yao.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kufiriki na kutenda kama vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa kutambua kamba, historia ya wokovu ni kielelezo cha mpango mkubwa wa upendo wa Mungu kwa binadamu. Upendo huu unaheshimu: uhuru wa watu na wote wanaalikwa kujenga familia ya ndugu wamoja katika haki, mshikamano na amani, ili kujenga Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Mikono ya Yesu pale Msalabani ni kielelezo cha upendo unaowakumbatia wote katika huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka hata kwa wale wanaodhani kwamba, ni wadhambi waliotopea kabisa! Kwake yeye wote wanapata msamaha kwani wote wanahitaji kuona msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu, mwaliko kwa waamini kukumbatiana katika unyenyekevu na kiasi; mambo yanayowawezesha waamini kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Baba wa milele inayowaambata na kuwakumbatia wote.

Mama Kanisa anaendeleza mikono ya huruma ya Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa walimwengu wote. Baba Mtakatifu anawaalika wote kushiriki kikamilifu katika mchakato wa upendo na huruma ya Mungu inayowakumbatia na kuwaambata wote. Mwaka wa Jubilei ya huruma ya Mungu, uwasaidie waamini kupyaisha maisha yao, kwa kushuhudia huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kwani nguvu ya Injili ya huruma ya Mungu inayoleta mageuzi na kuwaingiza waamini katika moyo wa Mungu unaowawezesha kusamehe na kuuangalia ulimwengu kwa jicho la wema wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha katekesi zake kwa Jumamosi kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, akitumaini kwamba, waamini wataweza kuonja katika maisha yao msamaha, huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Amewashukuru watu kutoka katika mataifa mbali mbali waliojisadaka kwa majitoleo yao ya huduma wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, changamoto na mwaliko wa kuishi vyema matukio haya ya imani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.