2016-11-11 10:08:00

Subira ni tunda la huruma ya Mungu!


Mwanadamu anapokikabili kifo huonesha hali ya hofu na mashaka. Pamoja na kwamba tunao uhakika ya kwamba hapa duniani tunapita tu, yaani kuna siku ya mwisho wa maisha yetu, bado siku hiyo inapotukabili mara nyingi tunasongwa na hofu na mashaka mengi. Moja ya tungo za Kanisa inatutaja sisi wanadamu kama wasafiri hapa duniani ikisema: “hapa wewe msafiri, simama na tazama, nimekufa leo, kesho ni zamu yako”. Pia ipo tungo nyingine katika muziki wa kawaida wa kijamii inatuambia kwamba “dunia tutapita na ipo siku itabakia, binadamu hatutaishi milele”. Hizi na nyingine nyingi hazitusaidii kujiuliza tufanye nini ili kuupokea huo mwisho wa siku zetu hapa duniani.

Pengine hofu hizo huchagizwa na kutokujiandaa kwetu au kusongwasongwa kwetu na uzuri wa mambo ya kidunia. Somo la Injili ya leo linaanza kwa kutuonjesha upande huo wa kibinadamu ambao hautuunganishi na huruma ya Mungu: “Watu kadha wa kadha walipokuwa wakiongea habari za hekalu, jinsi lilivyopambwa kwa mawe mazuri na sadaka za watu”. Ndiyo! Wana haki kabisa kuzungumzia juu ya uzuri huo wa jengo la hekalu la Mungu lakini onyo hapa ni kuepa kusalia katika uzuri huu wa nje bila kuangalia uzuri wa ndani, katika moyo wa kila mmoja ambaye amefanywa kuwa hekalu la Roho Mtakatifu.

Uzuri wa hekalu letu binafsi unatuhitaji kila mmoja kuudhihirisha kwa matendo yake. Huku ndiko kule kuufanya hai uzima wa Mungu unaowekwa ndani mwetu ambao ni uthibitisho wa huruma yake kwetu sisi. Katika somo la pili Mtume Paulo anasisitiza kwamba wao walifanya kazi “makusudi ili tufanye nafsi zetu kuwa kielelezo, mtufuate” Wosia huu wa kitume ni ukumbusho kwa ule wajibu tunaopewa wa kujiweka kama kielelezo kwa wengine kwa mfano wa maisha mema ya kikristo. Tunapofanywa wakristo tunapokea wajibu wa kuidhihirisha mbegu hiyo ya kikristo iliyopandwa ndani mwetu kwa kila mmoja wetu kwa wito na nafasi yake. Huu ndiyo umisionari wa ndani wa kuwaonjesha wengine huruma ya Mungu tuliyoipokea.

Huu ni mwaliko wa kuacha kuwa watazamaji tu na kutoa hukumu, kuepa kuwa kama hawa anaowataja kuwa “hawana shughuli zao, lakini wanajishughulisha na mambo ya wengine”. Ni kundi la wale ambao wapo katika hatari ya kubaki kuangalia na kukosoa au kusifia wengine; kwamba wametenda hivi, wana kasoro hii n.k Hawa ndiyo wanaofanana na hao tunaowasikia katika somo la Injili wakisifia uzuri wa hekalu huku wakisahau kulijenga na kulipamba hekalu litakalodumu yaani wao wenyewe. Tukisalia katika hali hii tu ndipo tutajikuta mara nyingi tunaingiwa na hofu, woga na mashaka mengi tunapoukabili mwisho wetu.

Wito wa Mtume Paulo anayesema: “Basi twawaagiza hao na kuwaonya katika Bwana Yesu Kristo, watende kazi kwa utulivu na kula chakula chao wenyewe”, ndiyo unatuiningiza katika fundisho la Dominika hii ya leo. Tunakumbushwa kwamba mwisho wa maisha haya ni hakika, mwisho huo unatia hofu lakini kwa huruma ya Mungu tunayo matumaini tele. Tunapoufanyia kazi wokovu wetu kwa kuikumbatia huruma ya Mungu basi tutayaona matunda ya kazi zetu kwa kuukabili vema mwisho wa ulimwengu bila ya kuwa na hofu na mashaka.Tunapolijenga na kulipamba hekalu hili la nafsi zetu tunalifanya kuwa tayari na kuwa na subira hata kuweza kukabiliana na hali zote hadi siku ya mwisho. Subira ni tunda la huruma la Mungu. Subira hii ndiyo wito wa maisha yanayoakisi muunganiko na Mungu tungali bado hapa duniani. Mwanadamu anapoungana na Baba yetu mwenye huruma daima anajisikia ukaribu naye na hamu ya kumuona uso kwa uso. Huyu hawezi kuuogopa mwisho wa maisha yake hapa duniani kwani ana uhakika wa kwenda kuungana na Yeye aliyekuwa yote katika maisha yake yote hapa duniani.

Maneno ya Kristo: “walakini hautapotea hata unywele mmoja wa vichwa vyenu” ni yenye kututia nguvu na kuoionesha thamani tunayokuwa nayo tunapodumu katika Kristo. Kifungu hiki kinaturudisha katika kuitathimini hadhi yetu tunayopewa na Mungu. Tumeumbwa mwili na roho na Mungu anatuthamini katika ukamilifu huo. Hakuna ambacho kitapotea hata kama itaonekana kudhalilishwa katika ulimwengu huu wa leo. Tusihangaikie kujilinda sana pengine hata kuipoteza thamani yetu tunayoipokea kutoka kwa Mungu kwa kuitwa watoto wake. Huu ni ukumbusho wa kuwa tayari hata wakati mwingine kujitoa sadaka iwe ni kwa kumwaga damu au katika namna ya kisaikolojia au kijamii kwa ajili ya kumtukuza Mungu tukiwa na chagizo kwamba vyote tulivyonavyo na hivi tulivyo tu mali ya Mungu na Yeye mwenyewe atatutetea.

Kristo anahitimisha katika Injili hii ya leo kwa kusema: “Nanyi kwa subira yenu mtaziponya nafsi zenu”. Subira hii inapendekezwa kwetu kwa sababu Kristo anayo hakika kwamba tunao uwezo wa kustahimili. Ametupatia tena uzima wa kimungu kwa kifo na ufufuko wake na kuturudishia hadhi yetu ambayo tuliipoteza sababu ya dhambi na ametumiminia Roho Mtakatifu ambaye ni kielelezo cha uwepo wake katika kuidhihirisha huruma ya Mungu kwetu. Ndiyo maana anasema pia: “Basi, kusudieni mioyoni mwenu, kutofikiri-fikiri kwanza mtakavyojibu; kwa sababu mimi nitawapa kinywa na hekima ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga”. Wito Kristo wa udumifu katika kumtegemea na imani kwake ni kule kututia nguvu na kutufunulia huo uwezo wa kimungu ambao tunao ndani mwetu, uwezo huo unao tufanya kuwa kweli wana wa Mungu na kutuunganisha sote kama ndugu katika ukweli. Hata inapoonekana kusalitiwa au kutengwa na wazazi au ndugu zetu sababu ya ukweli huo katika Kristo hatupaswi kupoteza matumaini.

Ni ukumbusho kwetu kwamba mahusiano ya kawaida ya kibinadamu yanapoikosa chachu ya Injili mara nyingi hugeuka kuwa ni mahusiano bandia, yasiyo na cheche za kimbingu na mwisho wake mara nyingi huwa ni wa mashaka. Hili linajidhihirisha katika mambo mengi ya kawaida ya maisha ya kibinadamu. Tuchukulie mathalani uhalisia wa maisha ya familia katika ulimwengu wa leo: Kwa bahati mbaya sana wengi hawajengi katika Upendo wa kimungu bali katika matamanio na mielekeo ya kidunia. Kati ya wanafamilia hakuna udumifu katika Mungu na mwisho wake wengi huwa ni kuvunjika kwa mahusiano katika familia. Wengi leo hii wanaogopa kuingia katika familia kwa sababu wanaona giza, wanaingiwa na hofu na wanakosa matumaini. Familia ambayo inapaswa kuwa taasisi ya kibinadamu ya kustawisha mahusiano inapoteza ladha yake kwa sababu tu wanaikosa subira inayosababishwa na Kristo, subira ambayo ni tunda la huruma ya Mungu.

Hivyo tujikumbushe leo hii juu ya uhakika wa mwisho wa maisha yetu hapa duniani. Lakini pamoja na uhakika huo tutambue kwamba maisha yanapaswa kudhihirishwa na si kuyakimbia na hivyo tunapokuwa tayari kuishi vema na kubaki waaminifu kwa Mungu, pale ambapo tunapoyaunganisha maisha yetu na Mungu tutaweza kuuona mwisho wetu kuwa ni rafiki au kama alivyoona Mtakatifu Francisko wa Assisi na kudiriki kukiitwa kifo kama “dada mpendwa”. Somo la kwanza la Dominika hii linatuthibitishia ukweli wa ujio wa siku hiyo. Ni uchaguzi kwetu kwani “watu wote wenye kiburi, nao watendao uovu, watakuwa makapi ... lakini kwenu ninyi mnaolicha jina langu, jua la haki litawazukia, lenye kuponya katika mbawa zake”.

Kutoka studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.