2016-11-11 11:54:00

Machoni pako kuna neno langu! Ni kitabu chenye utajiri mkubwa!


Jarida la “Civiltà Cattolica” linalohaririwa na Shirika la Wayesuit tangu kunako mwaka 1850 limekuwa na uhusiano wa pekee na Vatican na limekuwa likiandika na kuchapisha mahojiano maalum na viongozi wakuu wa Kanisa. Padre Antonio Spadaro, SJ. Mkurugenzi wa Jarida hili amekuwa mstari wa mbele kufanya mahojiano na Baba Mtakatifu Francisko katika tema mbali mbali ambazo zimesaidia kwa kiasi kikubwa kufahamu tasaufi ya maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko.  “Machoni pako kuna neno langu”.

Hiki ni kitabu ambacho kinakusanya sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko alipokuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Buenos Aires, Argentina kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2010. Hii ni zawadi kwa Baba Mtakatifu Francisko anapomshukuru Mungu kwa zawadi ya miaka 80 tangu alipozaliwa. Kitabu hiki ni maabara ya maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko anayejielekeza zaidi kama shuhuda na chombo cha furaha ya Injili; Huruma ya Mungu na kiongozi anayejipambanua na wengine kutokana na ushuhuda wa maisha yake kwa kuwa ni Baba wa maskini.

Haya yamesemwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Alhamisi, tarehe 10 Novemba 2016 alipokuwa anazindua kitabu cha mahubiri ya Baba Mtakatifu Francisko “Machoni pako kuna neno langu”. Maneno ya Baba Mtakatifu yanaonesha utajiri mkubwa katika maisha na utume wake unaobubujika kutoka katika majiundo thabiti ya shule ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola inayopata mwanga angavu kutoka katika tafakari ya Neno la Mungu. Mahubiri ya Baba Mtakatifu, kisimingi yanamwezesha mwamini kupata mang’amuzi ya Kiinjili katika maisha yake.

Baba Mtakatifu Franciko anajisikia kutoka katika undani mwake, umuhimu wa kumwangalia mwamini machoni pake hata kama mbele yake kuna karatasi ya mahubiri. Anataka ujumbe wa Neno la Mungu uguse akili, moyo na maisha ya mwamini, ili aweze kutubu, kuongoka na kuambata huruma na upendo wa Mungu katika hija ya maisha yake. Kitabu hiki ni mkusanyiko wa shuhuda mbali mbali ambazo Baba Mtakatifu Francisko amekutana nazo katika maisha na utume wake. Ni kiongozi anayethamini wazee kwani hawa ni amana na utajiri wa jamii, unaopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa.

Baba Mtakatifu Francisko katika kitabu hiki anajadili kwa kina na mapana changamoto zilizotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu mageuzi katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa “Sacrosanctum Concilium”. Lengo ni kuendeleza kipaji cha ugunduzi ili waamini waweze kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Kitabu hii kina mpangilio unaomwezesha  msomaji kuzama katika Liturujia ya Mwaka wa Kanisa; Sherehe za Kitaifa kisiasa na Kikanisa. Mahubiri haya yalikuwa ni kwa watu wa makundi mbali mbali na wote hawa walipewa Neno la Mungu kadiri ya hali, maisha na wito wao ndani ya jamii. Alionesha upendeleo wa pekee kwa maskini na watu wasiokuwa na ajira, kwa kuwataka wanasiasa na watunga sera kutoa kipaumbele cha pekee kwa mahitaji msingi ya binadamu yatakayowawezesha kutekeleza dhamana na wajibu wao katika maisha ya familia na jamii katika ujumla wake. Alipenda kufanya majadiliano na wanasiasa, ili kuwafunda tunu msingi za Kiinjili, ili kweli siasa iweze kuwa ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na wala si kichaka cha watu kujinufaisha wenyewe!

Baba Mtakatifu anagusia tema kama vile: Utandawazi, mshikamano, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kwa jicho la imani na uhalisia wa maisha ya watu. Mahubiri yakiandaliwa vyema yanaweza kuwa msaada mkubwa hata kwa wanasiasa, ili kujenga na kudumisha utamaduni wa haki, amani, upendo na mshikamano wa kweli unaofumbatwa katika Amri kuu ya upendo kwa Mungu na jirani; lengo ni mafao ya wengi. Kardinali Pietro Parolin anasema, sehemu kubwa ya kitabu hiki inapambwa na ujumbe, mahubiri na mahojiano na walezi pamoja na makatekista. Yote haya yalipania kutoa majiundo ya awali na endelevu ya maisha ya kiroho na kiutu kama sehemu ya katekesi endelevu katika maisha ya waamini. Alikuwa na mvuto wa pekee kwa vijana watukutu, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu, chachu ya toba na wongofu wa ndani. Vijana wajengewe ari na moyo wa kujifunza, kujadili na hatimaye, kuwa na msimao wa maisha.

Kitabu hiki, kinahitimishwa na mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 28 Machi 2013, mahubiri aliyokuwa ameandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Sakramenti ya Kipaimara Jimboni mwake! Ya Mungu mengi anasema Kardinali Parolin, Baba Mtakatifu hakupata nafasi tena ya kurejea Jimboni mwake. Mafuta ya Krisma Takatifu ni yale wanayopakwa wagonjwa, maskini wa roho, wafungwa na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Huu ndio mwelekeo ambao Baba Mtakatifu Francisko anauonesha kama sehemu ya utajiri mkubwa wa maisha yake ya kiroho!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.