2016-11-11 10:26:00

Amewafumbua macho ili kuona vituko vya walimwengu!


Mara nyingi tunasikia na hata kushuhudia vihoro na vitisho vinavyotokana na mitetemeko ya ardhi, mafuriko, radi, vita, mauaji, na madhulumu mbalimbali. Lugha ya biblia kwa vituko hivyo huitwa Ufunuo. Kwa kiingereza ni Revelation au Apocalypse lenye asili ya maneno mawili ya lugha ya Kigiriki: Apo maana yake kufunua na Calupto ni kufichika. Hivi apokalipto ni kitendo cha kuondoa, kufunua, kufichua kitu kilichokuwa kimefunikwa au kufichika. Kwa hiyo matukio ya vihoro na vitisho hayana mahusiano yoyote na kiyama au mwisho wa dunia. Tafsiri sahihi ya kiswahili ya Biblia, kitabu cha Revelation au Apocalypse ni Ufunuo. Maana yake kufunua au kuonesha, kutambulisha au hata kuielewesha akili kitu kilichofichika na kisichoeleweka.

Lugha ya ufunuo ilizungumzwa Palestina na Mashariki ya mbali miaka mia mbili (karne mbili) kabla ya Kristu hadi miaka mia mbili (karne mbili) baada ya Kristu. Wakati huo ulimwenguni kulipamba vita, utumwa, kuoneana na kudhulumiana. Kulikuwa pia mitetemeko ya ardhi, mafuriko na kupatwa kwa jua nk. Kwa hiyo watu wa ufunuo wakaona kuwa Mungu aliwania kuubomoa ulimwengu huo na kuanzisha ulimwengu mpya.

Katika Injili ya leo Yesu anatumia lugha ya Ufunuo ili kutufunulia pazia linalotuzuia kuona matukio ya vihoro na vitisho kwa jicho la Kimungu. Hebu tuone kwanza mazingira yaliyompelekea Yesu kutumia lugha hiyo.

Yesu na wafuasi wake wamefika Yerusalemu na kuelekea moja kwa moja hekaluni. Hekalu la Yerusalemu lilijengwa kwa kiufundi na ustadi mkubwa sana hadi Talmud ya Wababiloni inasema: “Asiyewahi kuona hekalu la Herode, huyo hajaona kitu katika maisha yake.”  Wanateknolojia nao walisema kwamba katika ulimwengu wa kale kulikuwa na maajabu saba. Waisraeli waliongeza maajabu mawili zaidi yahusuyo Hekalu la Yerusalemu. Mosi, mjengo wake wa mbele, na pili, mjengo wa sehemu ya kibra ya Hekalu. Kadhalika Hekalu la Yerusalemu lilikuwa tajiri sana kama benki kuu ya dunia ya wakati huo. Ukweli huo unaushuhudia miaka sabini baada ya Kristu hekalu lilipobomolewa na Kaisari Titus. Kinara cha Menora (kinara cha mwanga) kilipohamishwa toka Hekaluni kilikuwa na uzito wa kilo sabini za dhahabu mtupu. Athari ya kuhamishwa kwa Menora kulishusha thamani ya dhahabu ya nchi nzima ya Siria kwa vile kiwango cha utajiri kilitegemea dhahabu hiyo.

Kwa hiyo Yesu na wafuasi wake wanapoingia tu hekaluni wakashuhudia jinsi watalaii na wahaji mbalimbali wanavyolishangaa hekalu hilo kama ilivyoandikwa: “Watu kadha wa kadha walipokuwa wanalishangaa na kuliongelea hilo hekalu lilivyo la ajabu.”

 Hapohapo Yesu akawakatisha tamaa akasema: “Haya mnayoyatazama siku zitakuja ambapo halitasalia jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa.” Lugha hii ya Yesu ilikuwa kufuru kwa waliomsikia, kwa sababu Hekalu lilikuwa makao ya Mungu hivi lisingeweza kubomoka hadi siku ya kiyama. Kwa hiyo, watu walitaka kujua kiyama hicho kingetokea lini na ishara zake ni zepi: “Mwalimu, mambo hayo yatakuwa lini, nayo ni nini ishara ya kuwa mambo hayo ya karibu kutukia?”

Yesu hasumbuliwi na tarehe za tukio kwani kwake ufunuo hauna maana ya kiyama, badala yake anaongea juu ya maana ya ishara hizo za vihoro na vitisho. Yesu anataka kuzungumzia vituko vya kutisha vinavyotokea katika kipindi cha mpito kutoka ulimwengu wa zamani na ulimwengu mpya. Lengo lake ni kuwaelewesha wafuasi wafanye nini kinapofika kipindi hicho cha misukosuko mikali mitetemeko ya ardhi, mafuriko, vita kwa sababu ulimwengu wa kale na sera zake zinapoanguka na kuingia ulimwengu mpya.

Yesu anatudokezea mambo mawili ya kufanya wakati wa kipindi hicho cha mpito ambacho ni kigumu:- Mosi Msidanganyike. Anasema: “Angalieni, msije mkadanganyika, kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, ‘Mimi ndiye.’” Mara nyingi wadanganyifu wengi wanaibuka wakati wa mabadiliko kutoka ulimwengu wa kale na kuanza ulimwengu mpya. Mfano halisi ni hekaheka, mikurupushano ya wakati wa uchaguzi mkuu wa nchi, wanasiasa wanapojinadi kuwa wao ni wakombozi wa Taifa, kwamba ulimwengu mpya umefika ambapo wananchi watapata maendeleo. Kumbe ni uwongo na wizi mtupu.

Kadhalika katika maadili, mmoja anajitokea na kusema kuwa ulimwengu tulio nao ni wa kale unatubana tusiwe huru kufanya tunachotaka, hivi tunataka uhuru. Kumbe, lengo ni kutotaka kuwajibika. Kudanganyika huko ni hatari kwani siyo ulimwengu mpya, bali ni mitindo inayopita, na ni matangazo  tu ya kisasa na ya kiuchumi na ni mwendelezo wa ulimwengu wa kale.

Pili Msitishwe, msifadhaishwe, msibabaishwe, msizubaishwe. Anasema: “Nanyi mtakaposikia habari za vita na fitina, msitishwe. Taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na matetemeko makubwa ya nchi; na njaa na tauni mahali mahali; na mambo ya kutisha na ishara kuu kutoka mbinguni.” Yesu anatumia picha hizo za ufunuo ili kuwafunulia na kuwaelewesha wafuasi wake kwamba wasitishike na vituko hivyo kwani ni kipindi cha mpito tu na ni mwanzo wa ulimwengu mpya aliouanzisha Yesu wa Nazareti katika Pasaka yake, wakati ulimwengu wa kale ungali na ukali wake.

Huo ulimwengu wa kale uliwakilishwa na nguvu za kidini zilizojionesha katika sura na picha ya uwongo; kwamba Mungu anatakiwa awekwe sawa kwa kumtolea sadaka, kufanyiwa madhehebu ya pekee, kumfukizia ubani ili asikasirishwe na dhambi zetu asije akatuadhibu. Kumbe ulimwengu mpya na wa kweli alioanzisha Yesu ni ule wa kutoa sadaka impendezayo Mungu ambaye matendo yake ni ya upendo. Kwa hiyo, Yesu anawatabiria madhulumu yatakayowapata waana wa ulimwengu mpya kama yalivyompata mwenyewe. Mwanzoni mwa Injili Luka anasema: “Ole wenu pale ambapo watu watawasemea vizuri,” Hii ni tahadhari kwa wafuasi wake, endapo watu wataongea vizuri juu yao, ni dhahiri kwamba wameshachepuka njia na kufuata sera za ulimwengu wa kale ndiyo maana hawadhulumiwi, badala yake wanaongelewa vizuri.

Kisha Yesu anasema: “Msiandae mtakachoenda kuongea. Roho atawapatia neno la kusema.” Kishawishi cha kutaka kushinda kipo katika wafuasi wake, ambacho ni kile cha kutayarisha majibu kabla kadiri ya vigezo vya ulimwengu huu. Yesu anaagiza kutoa jibu kadiri anavyopendekeza Roho juu ya ulimwengu mpya, kadiri ya Mwana wa Mungu anayetoa maneno ya matumaini, furaha na upendo.

Kisha anawatabiria kwamba: “Mtachukiwa na wote kwa jina langu.” Hapo kuna fundisho kubwa kwa wafuasi wa Kristo. Kwamba daima Mfuasi wa anapodhulumiwa yabidi ajiulize ni kwa sababu gani anadhulumiwa. Yawezekana anadhulumiwa kutokana na kuchagua kufuata ulimwengu mpya wa Injili, au ni kwa sababu anaishi kivyakevyake na kadiri ya mtindo wa ulimwengu wa kale. Ili kuelewa ninachomaanisha hapa, tuchukue mfano wa Injili, Yesu anaposema kuwa “Ninyi ni chumvi ya ulimwengu. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake hutupwa na kukanyagwa na watu.” Yawezekana mmoja unakanyagwa au anadhulumiwa kwa vile umepoteza radha. Kwa hiyo budi kujiuliza kama udhulumu huo unatokana na kuchagua ulimwengu mpya au kwa sababu umepoteza radha ya ulimwengu mpya wa Injili ya Kristo.

Hatima ya leo inatutuliza sana pale Yesu anaposema: “Wala unywele wa kichwa chako hautapotea kwani kwa uvumilivu wenu mtaokoa maisha yenu.” Mkifuata ulimwengu mpya, mnaweza kudhulumiwa, lakini maisha yenu ya kweli, haki na upendo hakuna atakayethubutu kuyagusa kwa sababu hayo ni maisha ya watoto wa Mungu ambao wanajenga maisha ya kweli, ya haki na ya upendo utakaobaki na kudumu milele.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.