2016-11-10 07:15:00

Umuhimu wa maridhiano katika masuala ya elimu na uhuru wa kujieleza!


Monsinyo Janusz Urbanczyk, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Shirikisho la Ushirikiano wa Kimataifa, Usalama na Maendeleo, OSCE, hivi karibuni katika mkutano uliofanyika huko Berlin, Ujerumani kuhusu maridhiano na utofauti, amekazia kwa namna ya pekee, umuhimu kwa Jumuiya ya Kimataifa kuheshimu na kuthamini utofauti unaojikita katika maisha ya binadamu kama njia makini ya kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi.

Ni chachu ya maendeleo na mafungamano ya kijamii katika Jumuiya ya Kimataifa, mwaliko na changamoto ya kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi, utu na heshima ya binadamu, mambo ambayo yamepewa kipaumbele cha pekee na ujumbe wa Vatican kwenye mkutano huo. Lakini, jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, kumekuwepo na wimbi kubwa la ubaguzi, kinzani na nyanyaso zinazodhalilisha utu na heshima ya binadamu; mafungamano ya kijamii, haki na amani.

Hapa kuna haja kwa wajumbe wa OSCE kujizatiti zaidi ili kuhakikisha kwamba, mataifa yanaendelea kujielekeza zaidi katika mchakato wa kudumisha maridhiano na utofauti kama njia ya kujenga na kudumisha amani. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna uwezekano mkubwa kwa watu kushuhudia utambulisho wao bila ya kuhatarisha amani na haki za watu wenye mawazo, imani na mielekeo tofauti ya maisha. Imani na tamaduni za watu ni urithi mkubwa unaopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi na kamwe kisiwe ni chanzo cha kinzani na vurugu.

Maridhiano yanakwenda sanjari na uhuru wa kuabudu, msingi unaofumbata haki msingi zote za binadamu! Uhuru wa vyombo vya habari unapaswa kuzingatia ustawi na mafao ya wengi na wala usiwe ni sababu ya machafuko na kinzani za kijamii kwani uhuru bila mipaka, anasema Monsinyo Janusz Urbanczyk ni kinyume cha ustaarabu. Uhuru wa kujieleza wakati mwingine, umekuwa ni chanzo cha vitendo vya ubaguzi, chuki,uhasama pamoja na misimamo mikali ya kidini ambayo imepelekea daima maafa kwa watu na mali zao

Maridhiano na utofauti yanapaswa pia kujikita katika sekta ya elimu kwa kufundisha umuhimu wa kuheshimu na kuthamini tofauti za kitamaduni, kikabila na kidini zinazojionesha miongoni mwa wanafunzi, ili kuondoa hali ya kudharauliana na kubezana kwa baadhi ya wanafunzi kudhani kwamba, wao ni maarufu zaidi kuliko wengine kutokana na tamaduni, kabila au dini yao. Elimu iwasaidie wadau mbali mbali kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa jamii inayoheshimiana na kusaidiana, ili kujenga madaraja ya haki, amani, ustawi na maendeleo. Kuna haja kwa nchi wanachama wa OSCE kuaanda mwongozo utakaodhibiti wimbi la ubaguzi na nyanyaso dhidi ya Wakristo!

Monsinyo Janusz Urbanczyk anahitimisha hotuba yake kuhusiana na mchakato wa maridhiano na utofauti kwa kukazia: umuhimu wa kudumisha maridhiano katika uhuru wa kujieleza kama njia ya kupambana na ubaguzi unaofanywa kwenye mitandao ya kijamii, hali ambayo inavuruga kabisa uhuru wa kujieleza sanjari na uhuru wa vyombo vya habari. Kanisa linafundisha kwamba, Jamii inayo haki ya kupata habari zinazofumbatwa katika ukweli, uhuru, haki na mshikamano.

Vyombo vya mawasiliano ya kijamii vinayo dhamana na wajibu wa kuelimisha na kudumisha misingi ya imani, upendo na  mshikamano ndani ya jamii, daima vikilenga kudumisha utu, heshima na mafao ya wengi. Mitandao mingi ya kijamii imeanza kutumiwa na wapinga amani na maendeleo duniani jukwaa la kupandikiza mbegu ya: ubaguzi, chuki na uhasama badala ya kuwa ni jukwaa linalowakutanisha watu ili kujenga umoja na mshikamano. Hapa kuna haja ya kuwa na kanuni maadili zinazoongoza mitandao ya kijamii, ili kudhibiti ubora wa habari zinazotolewa na mitandao hii. Juhudi hizi hazina budi kwenda sanjari na maridhiano ya kidini, ili kujenga na kuimarisha haki, amani na mshikamano wa kitaifa na kimataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.