2016-11-10 07:00:00

Ninyi ni Mahekalu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu!


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, anaendelea kumwakilisha Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika, na sasa yupo nchini Zambia, ambapo siku ya Jumatano, tarehe 9 Novemba 2016, ameadhimisha Misa Takatifu katika Kanisa Kuu la Mtoto Yesu Jimboni Lusaka, siku ambapo Kanisa zima huadhimisha sikukuu ya Kutabarukiwa Kanisa Kuu la Yohane wa Laterani, lililopo Jimbo kuu la Roma Sikukuu hiyo hulenga kukumbuka kwamba Mungu anaishi kati ya watu, Mungu yumo ndani ya waamini wabatizwa na anawajaza waamini Roho wake Mtakatifu, ili wapate kumpeleka Roho huyo wa Bwana kwa watu wengine wahitaji.

Kristo alifanyika mwili ili afanye makao yake kati ya watu. Kristo anaishi na waamini katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, ambalo ni chemichemi na kilele cha maisha ya wakristo, ndani ya Ekaristi Takatifu, kuna kila mema ya kiroho kwa ajili ya Kanisa. Uwepo wa Kristo na nguvu ya Kristo inapatikana katika Sakramenti zake, na mwanadamu anapata maisha ndani yake. Kama vile maji yatililikavyo kutoka Hekaluni, uwepo wa Mungu katika Kanisa lake, kupitia Neno lake na Sakramenti, mwanadamu anawezeshwa kuzaa matunda ya furaha.

Baada ya kurudi kwa Baba, Yesu anamtuma Roho Mtakatifu ili akae na wanadamu, na zaidi sana aishi ndani ya waamini wabatizwa. Kwa sababu hiyo, kama asemavyo Mt. Paulo, wamekuwa Hekalu la Mungu, kwa kuwa Roho wa Bwana anaishi ndani yao. Kila siku wanaalikwa kupalilia uwepo wa Roho wa Mungu ndani yao, ili wachote hekima na nguvu na kuwasaidia wengine. Zawadi hiyo ya Roho Mtakatifu, ni zawadi ya kushirikishana na wengine pia, ili kujenga Jumuiya moja yenye upendo, imani na matumaini. Kardinali Filoni, kawakumbusha kwamba wao ni wamisionari wa Injili, na umisonari wao uanaanzia katika familia ambapo wanaonjeshana ukarimu na msamaha. Watajifunza kutoka katika familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, huku Mtoto Yesu akiwa ndiye msingi na mhimili katikati ya maisha yao.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.