2016-11-10 15:34:00

Jiandaeni vyema kukunja jamvi la mwaka wa huruma ya Mungu!


Mpendwa Msikilizaji  wa Radio Vatican, tukumbuke mwaka wa  huruma ya Mungu ni mwaka wa kipekee uliotangazwa na   Baba Mtakatifu  Francisko , kwa lengo la kupata kueleza  namna ya  kuishi  huruma ya Mungu, katika maisha halisi  ya mwanadamu.  Katika  kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, tunatambua na kutafakari kwa kina jinsi  Mungu amekuwa karibu  katika kumhurumia na kumwinua  mwanadamu toka kuumbwa kwa ulimwengu  hadi sasa na kuendelea.

Mwaka huu wa huruma ya Mungu, ulitangazwa  rasmi  na kuanza  tarehe 8/12/2015, ambapo ilikuwa ni sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya Asili.  Sambamba na kuanza,  mwisho haukuwa mbali, mwaka huu wa huruma ya Mungu unakaribia au unaelekea kileleni , ambapo utafungwa rasmi na Baba Mtakatifu  tarehe 20/11/2016,  katika Dominika ya Bwana Wetu Yesu Kristo Mfalme. Ndani ya mwaka wa huruma ya Mungu, mengi yamefanyika na yanaendelea kufanyika, ili  tuu kujipatia  neema  zitokanazo na  huruma ya Mungu. Katika hili, wengi wamefanya hija katika makanisa yaliyoteuliwa;  kwa kuingilia mlango mtakatifu, kuadhimisha sakramenti ya upatanisho na Ekaristi Takatifu, jambo ambalo humpatia mhujaji rehema.  Hivyo Mungu anatualika wote sasa kujichotea  neema na rehema  kwa matendo ya huruma kwa kipindi kilichbakia.

Mpendwa msikilizaji, tukaribiapo katika adhimisho  la kilele  cha mwaka huu wa huruma ya Mungu, ni vyema  tukajikumbusha  na kutafakari  mambo muhimu ambayo yameahinishwa  katika ule waraka muhimu  wa Uso wa huruma au kwa kilatini Misericodiae vultus,, ambapo ni katika waraka huu baba Mtakatifu  alitangaza  mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu.,   Ebu sasa tutafakari kidogo ila kwa kina: Katika waraka huu wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko. Baba Mtakatifu alihimiza  na  kusisitizia umuhimu wa Kanisa kurudi kwenye misingi yake  ya huruma na kichungaji  na aka-kaza kwa  kusema “Kanisa litaishi uhalisia wa maisha yake endapo tu litaungama na kutangaza huruma na msamaha”, kitu ambacho ndiyo hulka haswa ya Mungu muumbaji na Mwana Mkombozi. Kwa kufanya hivyo Kanisa litawaleta watu wengi zaidi karibu na Chemchemi ya Huruma, ambaye ni Kristo Mwenyewe.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema ndani ya Misericordiae vultus, Kanisa limedhaminishwa kutangaza huruma ya Mungu,  ambayo ndio mdundo wa moyo wa Injili ambayo kwa namna yake Injili lazima izame katika mioyo na mawazo ya kila mtu. Mchumba wa Kristo (yaani Kanisa) lazima lijiunde, ili tabia yake iendane na ile ya Mwana wa Mungu aliyetoka na kujitoa kwenda kwa kila mtu bila ubaguzi. Katika siku zetu hizi ambapo Kanisa linajikita katika shughuli  ya uinjilishaji mpya, tena ya huruma, kanisa  linahitaji kukumbushwa tena na tena, kwa ari mpya na katika mtindo mpya wa Kichungaji. Huruma ni muhimu sana kwa Kanisa na kwa ajili ya unadhifu wa ujumbe ambao Kanisa lenyewe linaufundisha, linauishi na kuushuhudia. Lugha yake na matendo yake lazima vioneshe huruma ili kuweza kugusa mioyo ya watu wote na kuwaangazia ili waweze kuona njia iwapelekayo kwa Baba.

Ukweli msingi kabisa wa Kanisa ni upendo kwa Kristo. Kanisa lazima lijifanye lenyewe kuwa ni mtumishi wa upendo huo na liupeleke kwa watu wote; upendo ambao husamehe na hujionesha zaidi katika kujitoa kwake. Hatimaye, kwa vyovyote vile ambavyo Kanisa lipo, upendo wa Baba hujidhihirisha, Katika familia zetu, katika jumuia zetu, na katika vyama mbalimbali vya kitume na  hata vikundi vya sala: kwa ufupi  popote pale walipo Wakristo, kila mmoja lazima aonje chemchemi  ya huruma ya Mungu; anasema Baba Mtakatifu.

Ni mwaliko wa Baba Mtakatifu kuimwilisha na kuiishi huruma ya Mungu ili kweli sisi tuaminio katika jina la Kristo tuonekane kwa namna yetu ya kuishi. Huwa inakuwa bahati mbaya pale ambapo wale tunaolitaja jina la Kristo na kuitwa Wakristo, japo tunapenda kuhurumiwa na kusamehewa, sisi wenyewe tunakwepa kuwa na huruma na kuonesha huruma kwa wenzetu, Katika mantiki hii Baba Mtakatifu anasema hatuidhihirishi huruma ya Mungu, bali tunajitafutia  kujitukuza sisi wenyewe.

Baba Mtakatifu  anaendlea  kusema, Mbinu za kuidhihirisha huruma ya Mungu ni pamoja na kuwa tayari kujifahamu na kujipokea; halafu kuwa tayari kuwafahamu wengine jinsi walivyo na kuwapokea kama walivyo, ni hivyo tu tutaweza kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu. Jitihada zetu za kuimwilisha huruma ya Mungu zinahujumiwa na tabia yetu ya kutaka wangine wote wafikiri kama sisi, waongee kama sisi, watende kama sisi, watamani tunayotamani sisi, wayaseme tunayotaka kuyasikia sisi au waishi kama sisi. Kama wakiwa kinyume nasi, basi hao hawafai na ni maadui zetu!! Hasha, maisha ya safari ya imani siyo hivyo!

Maisha ya imani yanahitaji sadaka sana. Na sadaka mmoja wapo ni kuwapokea wale ambao wanafikiri, kutenda na na kuishi kinyume nasi. Hapa mpendwa msikilizaji mwaliko ni kwamba: tuwape na wengine nafasi ya kuwa wao. Ila sisi kama tunaomwamini Kristo, imani yetu inayomwilishika katika matendo mema ya upendo na huruma ndivyo viwafanye hao wenzetu, waitambue huruma ya Mungu tunayoisadiki, kuifundisha na kuiishi, na wakitaka watatufuata kutokana na mwenendo wetu mwema wa maisha ya kiimani na kijamii. Tunalirudia kwa hekima neno lile: huruma na upendo wa Mungu si swala la maneno-maneno, bali ni matendo halisi katika maisha. Mwito wa pekee kwa mwaka huu mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni kuitambua zaidi huruma ya Mungu, kuipenda zaidi huruma ya Mungu, kuishukuru zaidi huruma ya Mungu, kuimwilisha zaidi huruma ya Mungu na kuitangaza zaidi huruma hiyo ya Mungu kwa maneno na matendo ya maishani.

Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican tunakushukuru kwa kuitegea sikio kipindi hiki. Katika kipindi hiki kifupi kilichobakia  mwaka  wa Jubilee ya Huruma ya Mungu, tuendelee kusali na kuomba huruma ya Yesu tukisema: Ee Yesu mwenye moyo mpole na mnyenyekevu, ufanye mioyo yetu ifanane na Moyo wako Mtakatifu. Amina.

Na Padre Agapito Amani.








All the contents on this site are copyrighted ©.