2016-11-07 15:13:00

Familia ya Mungu nchini Malawi, kiteni maisha yenu kwa Yesu!


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu kuanzia tarehe 3 - 7 Novemba 2016 amekuwa na ziara ya kitume nchini Malawi, ili kumwakilisha Baba Mtakatifu Francisko katika kutabaruku Kanisa la Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi, Jimbo Katoliki, Karonga. Amepata nafasi ya kuzungumza na Wakleri, watawa pamoja na waamini walei. Jumapili tarehe 6 Novemba 2016 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Parokia ya Mtakatifu Patrick, Jimbo kuu la Lilongwe, Malawi na kukazia umuhimu wa waamini kukita maisha yao kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kiini cha imani ya Kanisa katika Fumbo la Ufufuko.

Katika mahubiri yake, Kardinali Filoni ametumia fursa hii kuipongeza familia ya Mungu nchini Malawi, kwani amepata nafasi ya kuisikiliza na kuzungumza na kusali pamoja. Liturujia ya Neno la Mungu inaonesha maisha ya uzima wa milele na kwamba, Mwenyezi Mungu ni Mungu wa wazima na wala si Mungu wa wafu, dhana inayoonesha uhusiano wa kifamilia na Taifa teule. Kanisa kwa sasa ni familia ya Mungu na kwamba, jina la kila mmoja wao, linaonesha uhusiano wake na Mungu. Yesu Kristo ni Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, Mungu aliye hai anaendeleza mchakato wa mahusiano kwa sababu ni kiini cha Agano; Yeye ni ufufuko na uzima!

Kardinali Filoni anawakumbusha waamini kwamba, mshikamano na mafungamano yao na Kristo Yesu yawawezeshe kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha na amani; chachu inayomwezesha mwamini kukabiliana na magumu pamoja na changamoto za maisha kwa imani na matumaini. Yesu anatambua ni kwa jinsi gani familia ya Mungu nchini Malawi inavyopambana na umaskini, ukabila, chuki, kinzani na imani za kishirikina.

Ikiwa kama familia ya Mungu nchini humo itaweza kushinda kishawishi hiki inaweza kujikita katika umoja na mshikamano, kwani upendo wake unaponya na kuunganisha, ili kuendelea kuwa waaminifu. Huruma na upendo wake, daima vitaendelea kuiandama na kuifumbata familia ya Mungu nchini Malawi. Hii inatokana na ukweli kwamba, Yesu kwa njia ya Sakramenti za Kanisa na mahusiano ya kirafiki anaendelea kusafiri pamoja nao. Hii ni changamoto kwa waamini kujibidisha kukutana na Mungu aliye hai kwa njia ya Kristo Yesu, katika Neno, Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na kati ya watu wake. Nguvu ya Kristo iwaimarishe ili kukabiliana na changamoto za maisha pamoja na kuwashirikisha wengine upendo wa Kristo na kwamba, wanawajibika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayofumbatwa katika imani, matumaini na mapendo, ili kuendelea kushangazwa na huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.

Mara baada ya Misa Takatifu, Kardinali Fernando Filoni, amewataka waamini kuchuchumilia utakatifu wa maisha unaobubujika kutoka katika neema ya utakaso waliokirimiwa wakati wa walipobatizwa na kuimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara, changamoto ya kukuza na kudumisha mahusiano mema na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Neno, Sakramenti na Maisha ya Sala.

Amewataka kuwa waaminifu katika maagano yao ya ndoa, wito na maisha ya kipadre na kitawa. Walinde, wakuze na kudumisha utu na heshima ya Sakramenti za Kanisa, kwani wao ni sehemu ya viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Ameishukuru familia ya Mungu nchini Malawi, kwa kuendelea kuunga mkono mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Waendelee kujisadaka kwa ajili ya upendo kwa Mungu na jirani.

Viongozi wa Kanisa wajenge maisha na wito wao katika toba na wongofu wa ndani, ili kuwaendea wale ambao wako pembezoni mwa vipaumbele vya walimwengu kwa nyakati hizi. Wawe makini katika huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama sehemu ya mchakato wa mwendelezo wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ili kuendelea kukumbatia na kuambata huruma ya Mungu katika maisha yao ya kila siku. Waamini wawe kweli ni mitume na wamissionari wanaoshuhudia ukweli, uzuri na nguvu ya Injili inayoleta mabadiliko katika maisha; tayari kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma, upendo na ukweli; tunu msingi zinaosimamisha na kuimarisha familia ya Mungu nchini Malawi. Huruma ya Mungu iwasafishe na kuwatakasa, ili waweze kuwa kweli ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao, hasa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.