2016-11-03 15:40:00

Malawi: Iweni ni mashuhuda wa furaha ya Injili na maisha adili!


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, kuanzia tarehe 3- 7 Novemba 2016 anafanya ziara ya kichungaji nchini Malawi, kama mwakilishi maalum wa Baba Mtakatifu Francisko katika sherehe za kutabaruku Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu, Jimbo Katoliki Karonga. Akiwa nchini Malawi, Alhamisi, tarehe 3 Novemba, 2016 amekutana na kuzungumza na Wakleri pamoja na watawa waliokuwa wamekusanyika Jimbo kuu la Lilongwe, Malawi.

Katika hotuba yake, Kardinali Filoni amewashukuru wadau mbali mbali waliondaa na kuratibu hija yake ya kichungaji nchini Malawi pamoja na Wakleri na Watawa wote wanaohamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa katika maisha na utume wao; kwa kuonesha imani na upendo wao kwa Mungu na jirani; kikolezo muhimu sana cha ushuhuda na utangazaji wa Injili ya Kristo.

Kardinali Filoni, amewataka wakleri na watawa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Furaha ya Injili, kwa njia ya toba na wongofu wa ndani; Sala na tafakari ya Neno la Mungu; mambo msingi yanayojenga uhusiano wa karibu na Mwenyezi Mungu. Kanisa linawahitaji watangazaji na mashuhuda wa Injili ya Kristo kwa maisha yenye mvuto na mashiko kwa watu wanaowazunguka na wala si kwa njia ya wongofu shuruti. Kama watoto wa Baba wenye huruma, wawe ni chachu ya furaha katika dhamana ya Uinjilishaji na huduma kwa familia ya Mungu nchini Malawi.

Kardinali Filoni amekazia umuhimu wa Wakleri na Watawa kuboresha maisha yao ya kiroho kwa kuchuchumilia utakatifu unaofumbatwa katika mapendo kamili na kwamba, utakatifu wa maisha yao, unapata chimbuko kutokana na Sakramenti ya Ubatizo, Daraja Takatifu na Wakfu wao mbele ya Mungu unaofumbatwa katika nadhiri yaani: Ufukara, Utii na Usafi kamili. Wakleri watambue kwamba, Upadre ni mtindo wa maisha na zawadi kutoka kwa Kristo kwa ajili ya Mungu na Kanisa. Huu ni wito unaojikita katika: Sala, Neno la Mungu na maisha adili, ili kuiga mfano wa Kristo mchungaji mwema.

Watawa wamfuase Kristo kwa njia ya ushuhuda wao wa kinabii na kukabiliana kikamilifu na changamoto katika ulimwengu mamboleo, daima wakiwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake.

Wakleri na watawa wawe ni mfano bora wa kuigwa katika maisha adili na kwa namna ya pekee kabisa kwa kutunza na kudumisha zawadi ya maisha ya useja. Wito na maisha yao ya kipadre na kitawa, yawasaidie kukuza na kudumisha urafiki, upendo na udugu katika Kristo Yesu; huku wakiendelea kusaidiana na kutaabikiana, daima wakijisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Kamwe wasikubali kumezwa na malimwengu, bali wawe ni mfano bora wa maisha ya kinabii. Wakleri na watawa wanahamasishwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya utume wao kwa familia ya Mungu nchini Malawi, ili kukuza na kudumisha ari na moyo wa kimissionari; kwa kuwafunda makatekista ili waweze kutekeleza vyema dhamana yao pamoja na kushirikishi kikamilifu katika azma ya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Wawe ni wahudumu wa Injili ya upendo miongoni mwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wasimame kidete kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu, hasa wale wanaotumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Walinde na kudumisha haki msingi za wakimbizi na wahamiaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.