2016-10-31 16:58:00

Ukimya wa Kanisa nyakati za madhulumu!


Katika miaka ya 1945 – 1965 Kanisa Katoliki lilipitia kipindi kigumu cha mateso ya Wakristo yaliyosababishwa na wakomunisti, hasa katika Ulaya ya Mashariki na ya Kati. Na jibu la Kanisa lilikuwa ni ukimya ambao ulitolewa ushuhuda kwa vifo dini vya waamini wengi. Hii ni mada iliyoandaliwa kutafakariwa na Taasisi ya Sheria za Kanisa mjini Venezia, Italia, hivi karibuni.

Tafakari hii ni muhimu katika harakati za kupatikana kwa uhuru wa kisiasa, tamaduni na kidini katika mataifa ya Ulaya ya Mashariki na Ulaya ya Kati, na dunia nzima. Ulaya ya Mashariki imepitia mahangaiko makubwa ya mabadiliko na ukuaji wa siasa za nadharia kuelekea uhuru wa kweli na uhalisia wa mwanadamu, uongozi na jamii. Kuna utajiri wa mambo mengi umepatikana duniani kutoka Ulaya ya Kati na pia Ulaya ya Mashariki. Kwa bahati mbaya, utajiri na uzuri wa sehemu hizi za Ulaya, umetawaliwa pia na kumbukumbu za maumivu ya mateso ya kiimani na vifo-dini vingi. Njia ya kuelekea uhuru wa kweli ni ya taratibu na mara nyingi inakuwa yenye mafarakano na umwagaji damu.

Nadharia za Utaifa na Utaasisi zinaweza kuwa mkono wa chuma na kuumiza raia. Katika hali kama hizi, Kanisa Katoliki huwa Kanisa la Ukimya, ambalo huweza kuongea kwa namna ya pekee tu kwa vifo-dini. Ile roho ya udugu na mshikamano huweza kupenya kwa taratibu sana kabla ya kufikia uhuru wa kweli. Hapa ndipo unapatikana uhusiano na mshikamano wa nguvu kati ya Baba Mtakatifu na Makanisa mahalia, na diplomasia ya Kanisa.

Siku hii ya tafakari juu ya Kanisa-Kimya, ni mwanga wa kufungua akili na mioyo ya watu leo, katika hali kubwa ya hofu inayotawaliwa na ugaidi, manyanyaso, uvunjwaji haki na mahangaiko ya wanadamu sehemu mbali mbali duniani, vinavyotokana na nadharia za kisiasa au dini. Kanisa-Kimya, kwa umakini wa kutosha pamoja na shughuli zake za kidiplomasia, linajibu zaidi kwa kuishuhudia Injili ya Kristo, linakuwa tayari kuyapitia yote, lakini likibaki kuwa mwaminifu kwa Mafundisho msingi ya Imani, na kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.  








All the contents on this site are copyrighted ©.