2016-10-29 15:49:00

Mashuhuda wa imani kutoka Shirika la Wabenediktini!


Katika Kanisa Kuu la Almudena Jijini Madrid, wametangawa kuwa Wenye heri Wabenediktini wanne, walioifia dini wakati wa mateso ya Wakristo nchini Hispania kunako  mwaka 1936. Mapadri wafia dini hao ni José Antón Gómez, Antolin Pablos Villanueva, Juan Rafael Mariano Alcocer Martinez na Luis Vidaurrazaga Gonzales. Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza Wenye Heri na Watakatifu, amemwakilisha Baba Mtakatifu Francisko, katika tukio hilo takatifu siku ya Jumamosi tarehe 29 Oktoba, 2016.

Akizungumzia wafia dini hao, Kardinali Amato anasema, walionesha kutokuwa na woga wa kifo, bali wakamshuhudia Kristo, na kuonesha ujasiri wa kikiristo wakiwa na moyo mnyenyekevu na wa kusamehe. Kwa hakika ni mapadri walioifahamu vema Kanuni yao ya kibenediktini inayowaalika kutokulipa baya kwa baya, bali kuvumilia uonevu kwa subira, kuwabariki wanaowalaani na kukubali kuteseka kwa ajili ya haki.

Mateso ya wakristo yanakianika kitendawili kikubwa juu ya ubaya duniani, ubaya unaokatilisha na kuufanya mgumu moyo wa mwanadamu. Hali ya kijamii na kisiasa nyakati za miaka ya thelathini nchini Hispania, ilishuhudia hofu na chuki kubwa dhidi ya Kanisa Katoliki. Ni kati ya ishara chache zinazoonesha umiliki wa muda wa ufalme wa uovu, uliojaa chuki na uonevu dhidi ya ufalme wa Mungu, ambao ni ufalme wa haki, amani na upendo, anasema Kardinali Amato.

Kanisa hukumbuka wafia dini ikiwa ni alama hai ya harakati za utafutaji haki na ushuhuda wa wema. Katika matukio kama haya ya wafia dini, Kanisa linawaonya wote kutorudia matukio ya uonevu, chuki na mauji namna hii, badala yake kukumbatia ishara za uhai na maisha siku hadi siku. Ni nafasi nyingine tena za kupalilia utamaduni wa kukutana kwa upendo, ukarimu na maelewano.  Kwa mifano ya wafia dini, Kanisa linawaalika wote kuishi heri za Injili, kubariki dunia kwa maji ya msamaha, unyenyekevu, udugu na furaha ya kweli. Ni mwaliko wa kuwa jasiri na kujiaminisha kwa maneno ya Kristo mwenyewe anayesema: msiogiope wanoua mwili, lakini hawawezi kuiuwa roho (Rej., Mathayo 10, 28). Mapadri hawa wanne walikuwa wamonaki Wabenediktini waliotenda shughuli zao za umisionari na kumshuhudia Kristo, kila mmoja kadiri ya karama na vipawa alivyojaliwa na Mwenyezi Mungu:

Mwenyeheri Padre Josè Anton Gomez alizaliwa huko Hacinas, mnamo tarehe 26 Agosti 1878, akaweka nadhiri za kitawa mnamo tarehe 21 Novemba 1896, na kupata Daraja Takatifu ya Upadre huko Silos, Mexico, tarehe 31 Agosti 1902. Mwaka 1936 wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Hispania, alipofahamika kuwa ni Mtumishi wa Mungu, Padre Josè Gomez alikamatwa na kutiwa gerezani, kisha kuuwawa tarehe 25 Septemba 1936. Padre Gomez alikuwa mtu wa tabasamu, aliyejali watu, na katika Sakramenti ya kitubio, alifahamika kuwa mwalimu, baba na matakatifu katika kuwahudumia waungamaji.

Mwenyeheri Padre Antolin Pablos Villanueva alizaliwa tarehe 2 Septemba 1871 huko Villa de Lerma. Aliweka nadhiri za Umonaki tarehe 11 Septemba 1890 na kupata Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 19 Septemba 1896. Padre Villanueva alisomea Diplomasia na Historia huko Paris, Ufaransa. Baada ya masomo alitenda kazi za utume mjini Silos huko Mexico. Wakati wa mateso ya kidini, alikimbilia katika kisiwa cha Pinos, nchini Cuba, mwaka 1914 na baadae kurudi Hispania mwaka 1919. wakati wa vita nchini Hispania mwaka 1936, Padre Villanueva alitiwa gerezani na kuuwawa mnamo tarehe 8 Novemba 1936. Padre Antolin Villanueva alifahamika zaidi kwa utume wake katika Sakramenti ya Upatanisho, katika maktaba na waamini wengi walipenda kupata ushauri kutoka kwake.

Mwenyeheri Juan Rafael Martinez, alizaliwa Madrid tarehe 29 Oktoba 1889, na katika umri wa miaka ishirini aliingia Unovisi katika Abazia ya Silos, nchini Mexico. Tarehe 16 Aprile 1915 aliweka nadhiri za kitawa za kibenediktini, na kupata Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 25 Agosto 1918. Padre Martinez alikuwa Mwandishi na mwana Falsafa, elimu zilizomwezesha pia kubobea katika kipaji chake cha uongeaji. Wakati wa vita, baada ya Nyumba ya Wamonaki kuharibiwa, alipata hifadhi kwa rafiki yake, kama Wamonaki wengine walivyofanya. Hata hivyo alikamatwa na kuuwawa tarehe 4 Oktoba 1936. Padre Martinez, mbali na kuwa Mwandishi mzuri na maarufu, alipenda sana Liturujia, chemchemi ya maisha yake ya kiroho.

Mwenyeheri Luis Gonzales alizaliwa Bilbao mnamo tarehe 13 Septemba 1901. Baba yake mzazi alifariki dunia akiwa angali bado kijana, na hilo lilikuwa tukio lililoiyumbisha familia yao. Katika umri wa miaka kumi na miwili, aliingia katika Abazia ya Silos, Mexico, na kuanza safari ya malezi ya kitawa ya Wabenedktini. Tarehe 15 Septemba 1919 aliweka nadhiri za kitawa, na tarehe 19 Disemba 1925 akapata Daraja Takatifu ya Upadre. Alipangwa katika Monasteri ya Kogullada huko Zaragoza, na mwaka 1928 alihamishiwa Madrid. Yeye pia alikamatwa wakati wa vita mwaka 1936, na kuuwawa mwaka huo huo mnamo tarehe 31 Disemba, akiwa Padre kijana kabisa. Luis Gonzales ni Padre aliyekuwa mwaminifu na kujiheshimu sana. Alisifiwa kwa mahubiri yake mazuri, na alikuwa mhudumu wa juhudi sana wa Ekaristi Takatifu. Wabenediktini wafia dini hawa wanne, wanaongezeka katika namba ya wafia dini 1,600 wa Kihispania, waliotangazwa Watakatifu tangu mwaka 1987. kwa hakika ni umati mkubwa wa waamini waaminifu wa Kihispania, waliomwaga damu zao ili Ukristo usipotee, bali uzidi kushamili katika nchi yao.

 

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.