2016-10-28 15:14:00

Watawa huchangia ustawi, maendeleo na utakatifu wa Kanisa!


Maisha ya wakfu ndani ya Kanisa mahalia; Uanzishwaji wa mashirika mapya ya kitawa na kazi za kitume; uhusiano shirikishi kati ya watawa na viongozi wa Kanisa ni kati ya mambo msingi ambayo yamepembuliwa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 28 Oktoba 2016 wakati akizungumza na wajumbe Kongamano la Kimataifa kwa ajili ya wawakilishi wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki pamoja na Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume. Kongamano hili linahitimishwa rasmi, Jumamosi, tarehe 29 Oktoba 2016.

Baba Mtakatifu anawaalika wajumbe wa mkutano huu kuhakikisha kwamba, wanawasaidia Maaskofu mahalia kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wao barabara mintarafu maisha ya kuwekwa wakfu, ili Kanisa la Kristo liweze kukua na kukomaa kwa kutambua kwamba, maisha ya wakfu ni zawadi kwa Kanisa, inayozaliwa na kukomaa ndani ya Kanisa lenyewe. Maisha ya wakfu yanachangia katika Ukuhani wa Daraja na Ukuhani wa Ubatizo kama sehemu ya utume wa Kanisa.

Maisha ya kitawa ni nguzo muhimu sana inayochangia ustawi na maendeleo ya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa; dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa ari, moyo mkuu na furaha katika maisha, utume na utakatifu wake. Watawa wana uhuru wao kamili katika utekelezaji wa maisha na utume wao, lakini wanakumbushwa kwamba, hawajajitenga wala kutelekezwa pembezoni mwa Kanisa kama gari bovu! Watawa waishi vyema uhuru wao, kwa kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa mahalia.

Baba Mtakatifu anakaza kusema ni Roho Mtakatifu anayelifanya Kanisa kuwa moja katika ushirika na huduma, na kulifadhili karama mbali mbali za kiherakia na za kikarama ambazo huliongoza na kulipamba kwa matunda yake. Viongozi wa Kanisa wanaalikwa kuheshimu tofauti hizi zinazoliunda na watawa wakumbuke kwamba, wao ni utajiri unaofumbatwa katika maisha na utume wa Kanisa na Kristo ndiye kiini chake!

Mashirika Mapya ya kitawa na kazi za kitume yanayoendelea kuibuka ndani ya Kanisa ni matunda ya kazi ya Roho Mtakatifu na maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Ni wajibu wa Askofu mahalia kusoma alama za nyakati ili kutambua ukweli na uhalisia wa karama hizi, ili kuweza kuanzisha Shirika lenye hadhi ya Kijimbo kwa kuzingatia uhalisia, mwelekeo wa kinabii katika maisha ya Kanisa mahalia sanjari na umoja wa Kanisa la Kiulimwengu.

Karama hii inapaswa kuangalia mchango wake katika mchakato wa Uinjilishaji na mwelekeo wake wa kijamii; ukomavu wa maisha ya mwanzilishi wa Shirika kwa kuzingatia umoja na Kanisa. Maaskofu wanahimizwa anasema Baba Mtakatifu Francisko, kuwasiliana daima na Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume mintarafu Sheria za Kanisa namba 579 kwa ufafanuzi wa kina. Viongozi wa Kanisa wanapotekeleza wajibu huu nyeti watambue kwamba, wanafanya hivi kwa niaba ya Kanisa mahalia na Kanisa la Kiulimwengu, kwani ukuaji wa Shirika hili unaweza kuvuka hata mipaka ya Jimbo husika. Hekima na busara inatakiwa kwa ajili ya majiundo ya kina  kwa watakaji na kwamba, Askofu mahalia atoe nafasi ya kusaidiwa na watu ambao wana mang’amuzi mapana zaidi katika maisha ya kitawa na kazi za kitume.

Baba Mtakatifu anaendelea kukazia uhusiano shirikishi kati ya watawa na viongozi wa Kanisa kwa kuzingatia: sheria na kanuni kama zilivyobainishwa na waraka juu ya “Mahusiano shirikishi” “Mutuae relationes” wa Mwaka 1994 ambao kwa sasa unapitiwa upya. Lengo na kujenga mahusiano bora zaidi yanayosimikwa katika majadiliano na heshima; kusikilizana na ukarimu; kukutana, kufahamiana, ujenzi wa udugu pamoja na mafao ya wengi. Huu ni wajibu fungamanishi kwa viongozi wa Kanisa na watawa katika ujumla wao wanaohamasishwa kuwa wajenzi wa madaraja ya umoja unaoheshimu na kuthamini utofauti unaopata chimbuko lake kutoka kwa Roho Mtakatifu.

Baba Mtakatifu anawataka watawa wa Mashirika ya tafakuri, kutafakari kwa kina na mapana Waraka wake wa kitume “Kuutafuta uso wa Mungu” “Vultum Dei quaerere” unaohimiza: ukimya mtakatifu unaochanua matunda ya moyo wa sala, neema ya huruma na utakatifu wa maisha. Hata Makanisa mahalia yanahitaji minara hii inayoonesha bandari salama katika maisha na mapito ya binadamu! Baba Mtakatifu anawataka viongozi wa Kanisa kuwaheshimu na kuwathamini kama wanawake wakomavu kwa kuwachia fursa ya kutekeleza dhamana na wajibu wao kikamilifu kadiri ya Waraka uliopita.

Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba yake kwa kusema, viongozi wa Kanisa wawe na mwelekeo mpana zaidi katika maisha ya kitawa na kazi za kitume. Wajenge na kuimarisha umoja wa Kikanisa, ushirikishwaji wa karama, uhuru kamili na dhamana ya watawa katika Kanisa mahalia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.