2016-10-28 09:15:00

Vatican na Vietnam kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi!


Katika kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa katika kikao cha tano cha Kikosi Kazi kati ya Viet Nam na Vatican, kumekuwa na kikao cha sita kuanzia tarehe 24 – 26, Oktoba 2016, mjini Vatican, chini ya Usimamizi Shirikishi wa Bwana Bui Thanh Son, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje ya nchi kwa upande wa Viet Nam, na Monsinyo Antoine Camilleri, Katibu Msaidizi wa Mahusiano ya Kimataifa kwa upande wa Vatikani.

Kati ya mambo msingi yaliyojadiliwa ni pamoja na suala la Uhuru wa Kuabudu kwa Jumuiya ya Wakatoliki wanaoishi nchini Viet Nam. Kwa upande wake Viet Nam wameihakikishia Vatican kuwa Wakatoliki mpaka sasa wanaendelea kupata Uhuru wa kutosha kutenda shughuli zao za Kiimani, na zaidi wanapata nafasi kushiriki katika maendeleo ya kijamii nchini Viet Nam. Vatikani imetoa shukrani zake kwa ushirikiano huo, ambao umeonekana hata hivi karibuni katika taasisi ya Elimu ya kikatoliki ya Viet Nam, na katika maadhimisho-hadhara ya Ibada mbali mbali za kikatoliki nchini Viet Nam.

Pande zote mbili zimeafikiana kuendelea na uhusiano huo kwa kuzingatia taratibu na kanuni sheria, ili maendeleo ya watu wa Viet Nam yaweze kusonga mbele kwa ushirikiano wa Wakatoliki, na Wakatoliki nchini humo waweze kushuhudia vema Injili kadiri ya mazingira na tamaduni za watu wa Viet Nam. Baada ya kikao, Uwakilishi wa Viet Nam ulimtembelea Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican pamoja na Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican na pia Uwakilishi huo ulipata nafasi kutembelea baadhi ya taasisi za kidini za Vatican. Kikao cha saba cha Ushirikiano huu kati ya Viet Nam na Vatikani, kimeafikiwa kufanyikia mjini Ha Noi, nchini Viet Nam.

 

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.