2016-10-27 16:16:00

Waonesheni upendo na ukarimu, lakini ndoa za mashoga ni marufuku Kanisani!


Waraka wa Viongozi wa Shirikisho la Makanisa ya Anglikani Kusini mwa Dunia “Global South Anglican” katika mkutano wa kimataifa uliohitimishwa hivi karibuni nchini Misri unakazia umuhimu wa kuonesha ukarimu, upendo na mshikamano kwa waamini wote licha ya mapungufu yao ya kimaadili. Lakini, viongozi hawa wanasema, ni marufuku kufungisha ndoa za watu wa jinsia moja katika Makanisa yao kwa kufanya hivi ni kwenda kinyume cha mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu!

Viongozi wa Makanisa wahakikishe kwamba, wanabainisha sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya watu wenye mielekeo ya ushoga ili waweze kupokelewa na kusaidiwa jinsi walivyo. Tamko hili limepokelewa kwa mikono miwili na waamini wa Kanisa ya Anglikani sehemu mbali mbali za dunia. Shirikisho la Makanisa Anglikani Kusini mwa Dunia ni muungano wa Majimbo 24 ya Makanisa Anglikani kati ya Majimbo 38 yanayounda Kanisa ya Anglikani kwa ujumla. Haya ni Makanisa ambayo yako Barani Afrika, Amerika ya Kusini na Asia.

Waraka huu unakaza kusema, ndoa za watu wa jinsia moja si jambo ambalo linakubalika na Kanisa kwani linapingana na mpango wa Mungu mintarafu wito na maisha ya ndoa na familia. Wakuu hawa wa Kanisa la Anglikani wanakaza kusema kila mwanadamu anapendwa na Mwenyezi Mungu na hivyo hata wao wanalazimika kuwapenda wengine kama Mwenyezi Mungu anavyofanya licha ya mapungufu na madhaifu yao katika masuala ya ndoa na familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.