2016-10-26 14:54:00

Papa Francisko: Usiogope kusamehe!


Usiwe na hofu ya kusamehe kwani Kristo mwenyewe amekuwa mfano bora wa kusamehe, nasi tulio wafuasi wake tunaalikwa kuiga mfano huo. Ni ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko alioutoa katika utangulizi wa kitabu Usiogope Kusamehe, kitabu cha Padre Luis Dri, akishirikiana na Andrea Tornielli na Alver Metalli. Kitabu amabcho kipo tayari kununuliwa katika maduka ya vitabu tangu tarehe  25/10/2016. Wito wa Baba Mtakatifu kwa mapadri waungamishi ni kuwa tayari muda wote na bila kusita kuwaonesha waungamaji mikono ya huruma ya Mwenyezi Mungu wanapofika kwa Sakramenti ya Kitubio.

Kila mwamini aendaye kuungama hufika pale kupitia njia tofauti tofauti: yupo aliye na mazoea ya kujipatanisha mara kwa mara; yupo anayefika baada ya muda mrefu bila kuungama; yupo anayefika kwa kuguswa na tukio fulani maishani; wakati mwingine ni hatua ya mwisho baada ya mateso ya muda mrefu. Kwa ufupi, kwa Mwenyezi Mungu hakuna mpango wa bahati, Yeye ndiye mwenye kusamehe, na ni Yeye ndiye mwenye kuwatafuta wanae wapotevu. Hivyo,  mbele ya kila Muungamaji, Padre anapaswa kuwa na mwitikio wa Baba mwenye huruma na upendo kama Baba wa mwana mpotevu.

Baba Mtakatifu anatoa mfano wa Mt. Leopoldo Mandic’, Padre aliyejua kuwatuliza na kuwafariji waungamaji kwa maneno na ishara za upendo na huruma ya Mwenyezi Mungu. Mt. Leopoldo alipenda kuwahakikishia waungamaji kuwa hata yeye alikuwa mdhambi kama wao, hivyo wasihofu, bali wawe na Imani na kujiaminisha kwa Mungu mwenye huruma. Siku chache kabla ya kifo chake, Mtakatifu Leopoldo alisema kuwa: ni miaka hamsini tangu amekuwa akiungamisha, na hajilaumu hata mara moja kwa mara zote alizowaondolea dhambi waungamaji katika Sakramenti ya Upatanisho, lakini aliumia pengine kwa mara tatu au nne ambapo hakufanikiwa kuondolea dhambi, kwani alihisi hakufanya la kutosha kumwezesha muungamaji kutubu kwa dhati dhambi zake.

Padre Luis katika kitabu chake anaeleza kuwa: palipo na huruma kwa kawaida kuna hisia za ubinafsi, za kujitetea, uwekaji wa mipaka katika kuvumilia na maumivu ya uharibifu, hata hivyo kuna msingi pia wa Upatanisho unaowezesha huruma kushinda. Huruma ni ya Mungu, na anaionesha kwa namna ya pekee katika Fumbo la Umwilisho, anapojifanya Mtu ili kumkomboa mwanadamu. Ni huruma hiyo hiyo Mungu anapenda mwanadamu ajifunze na kuifuata, ili manufaa yake yaonekane katika jamii nzima. Hivyo kila ishara ya urafiki, ya salamu, ya upatanisho, hata kama haisemwi sana au kujaliwa na watu, bado inafaa katika kuleta matunda bora katika jamii.

Katika kitabu chake Padre Luis Dri: Usiogope kusamehe, Padre Luis anatoa mfano wa mchoro wa Baba wa mwana mpotevu. Anaeleza jinsi utofauti wa mikono ya Baba huyo katika mchoro, wa kulia ukiwa ni wa kike, ishara ya kuwa Mungu katika huruma yake anaonesha upendo wa wazazi wote wawili, Baba na mama; Macho yanaonekana kama ya kipofu, kuonesha namna alivyosubiri kwa muda mrefu mwanae kurudi hata macho yakaishiwa nguvu, hakika ni upendo wenye subira kweli kweli; ndevu zake hazionekani kunyolewa wala kutunzwa vema, kuashiria kuwa hamu yake ya kumwona mwanae mpotevu katika subira ilifanya ashindwe hata kujali usafi wake binafsi, ni upendo wa kina kwa hakika, unaothamini zaidi mwingine kuliko kujijali binafsi.

Padre Luis Dri, alikuwa muungamishi wa Papa Francisko, wakati akiwa Askofu Mkuu wa Buenos Aires, Argentina. Katika masimulizi yake, anaeleza vizuri juu ya dhambi na wokovu, kwa namna ya pekee, anatumia mfano wa hisia na tunu hizo kwa Papa Francis katika mazingira ya ufukara wa watu wa Bara la Amerika kusini na tamaduni zao. Ni masimulizi ya kugusa moyo kwani yanatafakarisha sana maisha ya mwanadamu, falsafa na siasa za leo, bila kusahau useja wa watu wa Mungu unaopelekea hata kutengwa na jamii. Ni kitabu kinachosaidia kufungua mwanga wa Ukarimu, Huruma na Upendo wa kujali wengine bila ubaguzi.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.