2016-10-26 10:43:00

Mshikamano wa upendo kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni muda muafaka wa kushuhudia imani tendaji inayomwilishwa katika matendo ya huruma na kwa namna ya pekee kwa kuwakaribisha wageni na kuwavika walio uchi! Matendo ya huruma yanawawezesha waamini kuwa macho na makini wanapoendelea kusafiri hapa duniani, tayari kukutana na Kristo hakimu mwenye haki atakayewauliza, ikiwa kama alipokuwa mgeni walimkaribisha na alipokuwa uchi walimvika!

Hii ni sehemu ya Katekesi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 26 Oktoba 2016 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Huduma kwa wakimbizi na wahamiaji ni changamoto kubwa katika ulimwengu mamboleo kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa, vita pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Yote haya ni mambo msingi yanayowalazimisha watu kukimbia nchi zao ili kutafuta usalama na maisha bora zaidi.

Lakini, wimbi la wahamiaji ni sehemu ya historia ya mwanadamu anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko na wala si jambo ambalo limeibuka wakati huu kama uyoga! Maandiko Matakatifu yana mifano hai ya watu waliohama au kukimbia nchi zao kati yao ni Babu wa imani, Mzee Ibrahim, Waisraeli na hatimaye, Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, iliyolazimika kukimbilia Misri ili kutoa hifadhi kwa Mtoto Yesu dhidi ya ukatili wa Mfalme Herode. Historia ya binadamu ni historia ya uhamiaji na kwamba, hakuna watu duniani wanaoweza kujidai kwamba, hawajawahi kuguswa na wimbi la uhamiaji!

Jumuiya ya Kimataifa kwa miaka mingi imeonesha mshikamano wa upendo hata kama wakati mwingine, kumekuwepo na kinzani za kijamii. Katika ulimwengu mamboleo, kumekuwepo na tabia ya ubinafsi, uchoyo na ukosefu wa ukarimu kiasi kwamba, watu wanataka kujenga kuta za utengano. Matendo ya wema na ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji yanayotangazwa na kushuhudiwa na watu wengi duniani yanazimwa na kunyamazishwa kutokana na sauti za watu wachoyo. Mambo haya anasema Baba Mtakatifu hayana tija wala mashiko kwa wahamiaji na wakimbizi na matokeo yake ni kuwatumbukiza katika dimbwi la biashara haramu ya binadamu. Njia ya muafaka ni mshikamano wa upendo!

Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, Kanisa, daima limekuwa mstari wa mbele kwa huduma kwa wakimbizi na wahamiaji. Mtakatifu Francesca Cabrini na wanashirika wenzake, walijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji waliokuwa wanakwenda nchini Marekani. Hata leo hii, ulimwengu unawahitaji mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu; watu watakaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji. Watu wanaokimbia vita, baa la njaa, dhuluma, nyanyaso na hali duni ya maisha.

Watu wote waoneshe moyo wa upendo na mshikamano kwa watu ambao wamepoteza utaifa, familia, kazi na utu wao kama binadamu! Kuwavisha walio uchi anasema Baba Mtakatifu ni kuwarudishia utu na heshima yao kama binadamu. Inasikitisha kuona kwamba, kuna wanawake na wasichana wanaotumbukizwa kwenye utumwa mamboleo kama ilivyo hata kwa watoto wadogo wanaodhalilishwa kingono.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, utupu wa mtu ni pamoja na kukosa fursa za ajira, makazi, mshahara wa haki; ubaguzi wa rangi au imani; vyote hivi ni vielelezo vya utupu wa mwanadamu, ambao Wakristo wanahamasishwa kujifunga kibwebwe ili kuweza kuwasaidia wahusika. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wasikubali kutumbukia katika ubinafsi, hali ya kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, kwani kwa kuwahudumia wengine, maisha yanachipuka upya na kusonga mbele, jamii inapata amani na watu wanapata utu mkamilifu! Baba Mtakatifu akizungumza na mahujaji pamoja na wageni amekumbusha kwamba, Ibada ya Rozari Takatifu ni muhtasari wa huruma ya Mungu. Kwa njia ya Tafakari ya Rozari Takatifu waamini wanasali na kutafakari pamoja na Bikira Maria maisha ya Kristo Yesu mwanga angavu wa huruma ya Mungu kwa waja wake; upendo na msamaha, changamoto kwa waamini kushuhudia imani yao kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.