2016-10-26 15:32:00

Kardinali Paulo Evaristo Arns; Baba wa maskini! Akumbukwa!


Kardinali Paul Evaristo Arns anamwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuadhimisha miaka 95 tangu alipozaliwa. Kardinali Arns, anayejulikana na wengi kama Baba wa maskini, ndiye peke yake anayeishi kati ya Makardinali walioteuliwa na Mwenyeheri Paulo VI, kunako mwaka 1973 ukimwondoa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI. Tangu mwaka 1966 hadi mwaka 1970 alikuwa ni Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la San Paolo, Brazil. Akateuliwa kuwa Askofu mkuu kuliongoza Jimbo hilo hadi kunako mwaka 1998 alipong’atuka kutoka madarakani.

Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani katika maadhimisho haya amemtumia Kardinali Paul Evaristo Arns ujumbe wa matashi mema na shukrani kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu Jimboni mwake. Akaonesha ari na moyo wa kichungaji, kiasi hata cha Mwenyeheri Paulo VI kumteuwa kuwa Askofu mkuu na baadaye Kardinali kama mshauri wa karibu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Kardinali Arns ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, aliyependa kuona kwamba, maamuzi ya Mababa wa Kanisa yanafanyiwa kazi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu. Kardinali Arns katika umri wa miaka 95 ndiye pekee kati ya Makardinali wote waliteuliwa na Mwenyeheri Paulo VI. Kwa hakika Kardinali Arns amekuwa ni sauti ya kinabii katika mchakato wa kulipyaisha Kanisa la Kristo, dhamana iliyovaliwa njuga na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Katika maisha na utume wake, daima alipenda kuona kuwa shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa zinajikita katika ari na moyo wa kimissionari ili kuwatangazia watu wa mataifa Habari Njema ya Wokovu. Alionesha kipaji cha ugudunduzi katika maisha na utume wake kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la san Paolo kiasi cha kutumia rasilimali na miundo mbinu iliyokuwepo kwa ajili ya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili, changamoto inayoendelea kutolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa viongozi wa Kanisa!

Mkazo ni umoja na mshikamano katika utekelezaji wa shughuli za Uinjilishaji anasema Kardinali Peter Turkson. Amekuwa ni kiongozi mahiri na mfano bora wa kuigwa katika kusimama kidete kuwalinda, kuwatetea na kuwahudumia maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na vita, nyanyaso na ubaguzi wa kina aina. Kardinali Arns alilitambulisha Kanisa kwa ajili ya maskini pamoja na maskini, ili aweze kuwapeleka wote mbinguni kwa Baba mwenye huruma.

Bado huu ni mwaliko unaoendelea kutolewa na Baba Mtakatifu Francisko hasa katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kusikiliza na kujibu kilio cha maskini, ili kuwatangazia na kuwashuhudia furaha ya Injili na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Kuna watu wanateseka anasema Kardinali Turkson kutokana na umaskini, ujinga, maradhi, njaa pamoja na kunyimwa haki zao msingi. Mambo yote haya yanakuwa ni kashfa kwa Jumuiya ya Kimataifa kwani, kwa hakika kuna chakula cha kutosha kuwalisha walimwengu, lakini kutokana na choyo na ubinafsi pamoja na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu, kuwa watu wanaendelea kufa kwa baa la njaa duniani. Kardinali Arns katika maisha na utume wake, alisimama kidete kuhakikisha kwamba, wananchi wanapewa haki zao msingi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.