2016-10-26 11:18:00

Kanisa linaendelea kujizatiti kutangaza na kushuhudia Injili ya familia!


Ulimwengu mamboleo na maendeleo ya sayansi na teknolojia umeendelea kusababisha changamoto ambazo zinapaswa kuvaliwa njuga na Mama Kanisa pamoja na watu wote wenye mapenzi mema ili kuweza kutangaza na kushuhudia Injili ya familia kati ya watu wa mataifa. Baadhi ya changamoto hizi ni ubaridi wa imani na kutopea kwa imani; kutukuza na kumezwa na malimwengu; uchoyo na ubinafsi pamoja na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani.

Lakini ikumbukwe kwamba, familia ni kitovu cha Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, ndiyo maana Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo linataka kuwekeza zaidi katika Injili ya familia, ili kushuhudia furaha ya Injili inayobubujika kutoka katika familia za Kikristo, licha ya changamoto, kinzani na vikwazo vinavyoendelea kujitokeza kila kukicha!

Haya yamebainishwa hivi karibuni na Kardinali Oswald Gracias, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bombay, India wakati wa maadhimisho ya Kongamano la Tume ya Maisha, Jimbo kuu la Bombay inapoadhimisha Jubilei ya miaka 25 tangu ilipoanzishwa. Maadhimisho haya yanaongozwa na kauli mbiu “Mwaliko wa uhuru na haki ndani ya familia na jamii: wasiwasi za kichungaji kimaadili.

Zote hizi ni changamoto za kichungaji ambazo hazina budi kuvaliwa njuga na Mama Kanisa pamoja na watu wote wenye mapenzi mema. Familia haina budi kurutubishwa kwa njia ya Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma, kielelezo cha imani tendaji. Kanisa liwe macho na makini kusoma alama za nyakati kwa kuangalia changamoto zote hizi ili kuweza kuzifanyia kazi kwa wakati muafaka kama alivyofanya Mtakatifu Yohane Paulo II na kwa sasa Baba Mtakatifu Francisko kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maisha na tunu msingi za kifamilia.

Changamoto hii ameivalia njuga kwa kuitisha Sinodi mbili za Maaskofu na hatimaye, kuchapisha Wosia wa kitume “Furaha ya upendo ndani ya familia” “Amoris laetitia” Ikumbukwe kwamba, ustawi na maendeleo ya jamii kwa sasa na kwa siku za usoni unapata chimbuko lake katika familia. Kutokana na ukweli huu, Kanisa kwa kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema, halina budi kujifunga kibwebwe ili kupambana na changamoto hizi.

Baraza la Maaskofu Katoliki India, kuanzia tarehe 31 Januari hadi tarehe 7 Februari 2017 litafanya mkutano wake wa mwaka huko Bhopal, ili kupembua kwa kina na mapana mchango wa vyama na mashirika ya kitume yanayojihusisha kikamilifu katika mchakato wa utangazaji na ushuhuda wa Injili ya familia nchini India. Katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Tume ya Maisha Jimbo kuu la Bombay, familia ya Mungu Jimboni humo imefanya maandamano makubwa kwa ajili ya kuenzi Injili ya uhai inayofumbatwa katika ushuhuda wa Injili ya familia. Kardinali Garcia katika maandamano hayo amesema, yalikuwa ni kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai na familia. Pili ilikuwa ni fursa ya kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini. Mwishoni, maandamano haya yalipania pia kulinda na kutunza mazingira, nyumba ya wote. Uchafuzi wa mazingira na athari zake ni kati ya mambo yanayoendelea kutishia Injili ya uhai na familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.