2016-10-26 15:09:00

Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani


Tarehe 31 Oktoba 2016 huko Lund na Malmo nchini Uswiss, Kanisa Katoliki na Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani yataadhimisha Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kufanya hija ya kitume nchini Uswis ili kushiriki katika maadhimisho haya ya kihistoria katika maisha na utume wa Kanisa.

Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo kwa kushirikiana na Dr. Martin Junge, Katibu mkuu wa Shirikisho la Makanisa la Kiinjili ya Kiluteri Duniani kwa pamoja wanapenda kuangalia mambo msingi yaliyojiri katika kipindi cha miaka 50 tangu Kanisa lianzishe mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa haya mawili katika ngazi ya kimataifa! Martin Luther kunako mwaka 1517 alilaani kwa nguvu zake zote vitendo vilivyokuwa vimejitokeza vya kuuza rehema kwa kuzingatia msingi ya maisha ya kiroho na kitaalimungu, changamoto ambayo ilileta mageuzi makubwa katika medani za kisiasa, kiuchumi, kiroho na kijamii.

Martin Luther hakuwa na wazo la kuanzisha Kanisa jipya, lakini kutokana na matukio hayo akajikuta analazimika kuanzisha Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani, hali iliyosababisha machafuko na kinzani kubwa ndani ya Kanisa. Maadhimisho ya kumbu kumbu hii, kwa muda wa miaka mingi yamekuwa ni kurasa chungu za misigano kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani. Lakini kwa mwaka huu, mambo yamegeuka kabisa, Wakristo wanataka kujikita zaidi katika mambo yanayowaunganisha badala ya kuogelea katika mambo yanayowagawa, ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko ameamua kushiriki kikamilifu katika tukio hili la kihistoria.

Lengo ni kuiangalia Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri kwa jicho la matumaini pamoja na kuendelea kuimarisha mafanikio yaliyokwisha kupatikana kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kiekumene katika kipindi cha miaka 50 iliyopita! Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walikazia kwa namna ya pekee maridhiano kati ya waamini wa Makanisa haya mawili na kwamba, Sakramenti ya Ubatizo ni kiini cha imani yao kwa Kristo na Kanisa lake na hivyo wote ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo yaaani Kanisa.

Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri ni fursa ya kukuza na kuimarisha mahusiano mazuri yaliyofikiwa baina ya Makanisa haya mawili katika Uekumene wa huduma ambao unashuhudiwa na waamini wa Makanisa haya sehemu mbali mbali za dunia. Waamini hawa wanaunganishwa na Uekumene wa damu unaojikita katika dhuluma, nyanyaso na mauaji dhidi ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia. Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita kumekuwepo na mafanikio yaliyofikiwa na kutiwa sahihi kwenye Waraka wa pamoja kuhusu Mafundisho ya “Kuhesabiwa haki ndani ya Kanisa” yaliyotiwa sahihi kati ya Makanisa haya kunako mwaka 1999.

Dhana ya kuhesabiwa haki ilikuwa ni kiini cha mpasuko kati ya Makanisa haya katika Karne ya XVI. Hapa waamini wanataka kuachana na utamaduni wa kifo ili kuambata hija ya kiekumene ili kujenga umoja wa Kanisa. Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri yanaongozwa na kauli mbiu “Kutoka katika kinzani kuelekea kwenye umoja. Tumeungana katika matumaini”. Kipaumbele cha kwanza ni umoja unaojengeka katika majadiliano ili kuvuka hali ya kinzani na misigano iliyojitokeza katika historia ya Kanisa.

Makanisa haya mawili, bado yanaendelea kuchangamotishwa ili kuhakikisha kwamba, yanaendeleza majadiliano ya kiekumene ili kuwa na ufahamu mpana zaidi kuhusu: Kanisa, Utume na Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Liturujia ya pamoja inakazia pia umuhimu wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya Neno la Mungu na kwa uwepo wake wa daima katika Kanisa lake. Ni wakati wa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Mageuzi kwa Makanisa haya.

Ni wakati wa toba na majuto kutokana na mpasuko wa Makanisa hali ambayo bado inasababisha machungu katika umoja, maisha na utume wa Kanisa. Toba kutokana na machafuko yaliyojitokeza wakati wa malumbano kati ya Wakatoliki na Waluteri sehemu mbali mbali za dunia kiasi cha kufumuka kwa vita ya kidini kati ya karne XVI na XVII Barani Ulaya. Sasa ni kipindi cha kushikamana kwa dhati ili kumshuhudia Kristo Mfufuka, kwa kuonesha furaha inayobubujika kutoka katika Injili ya Kristo na nguvu ya imani inayoleta mageuzi makubwa katika maisha ya waamini sanjari na kuendelea kujikita katika Uekumene wa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii sanjari na kuchuchumilia  huruma ya Mungu inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake!

Mambo haya makuu matatu yatakaziwa zaidi wakati wa maadhimisho ya Liturujia ya Kiekumene huko Lund pamoja na Hati ya pamoja itakayotiwa mkwaju kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Askofu Munib Younan, Rais wa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani. Uekumene wa huduma ni changamoto ya ushuhuda wa pamoja kutoka kwa waamini wa Makanisa haya mawili kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia, hali inayotaka mshikamano wa dhati kabisa! Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri ni changamoto na mwaliko kwa waamini kuangalia ya mbeleni kwa imani na matumaini zaidi, ili kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene ili kujenga umoja wa Kanisa. Itakumbukwa kwamba, Mageuzi haya yalipelekea kuibuka pia kwa Makanisa mengine yanayochota utambulisho wake kwa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani.

Wakristo wanahamasishwa kushikamana ili kushuhudia imani yao katika Fumbo la Utatu Mtakatifu; imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, tayari kuendeleza majadiliano ya kiekumene kwa kuachana na utamaduni wa kifo ambao wakati mwingine uligubikwa kwa masuala ya kidini yaliyopelekea majanga makubwa kwa watu na mali zao, ili kujikita katika hija ya pamoja ambayo imesheheni matumaini, upatanisho, upendo na huduma makini. Maadhimisho haya yawasaidie Wakatoliki na Waluteri kushikamana ili kushuhudia imani yao kwa pamoja katika ulimwengu ambamo kuna majeraha na makovu makubwa ya chuki, uhasama na utengano. Ni wakati wa kujielekeza zaidi katika majadiliano ya kiekumene, ili tofauti msingi ziweze kupatiwa ufumbuzi, ili hatimaye, waamini wote waweze kupokea na kusherehea matunda ya umoja, upendo na mshikamano!

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.