2016-10-26 12:05:00

Hifadhi ya nyaraka kidigitali inapania kushuhudia: ukweli, haki na amani


Kamati tendaji ya Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina iliyokuwa ikiongozwa na Askofu mkuu Josè Maria Arancendo imeungana na Kamati ya Vatican chini ya uongozi wa Kardinali Pietro Parolin kufanya tathmini ya kina na mapana inayopania kuweka kumbu kumbu za kipindi cha utawala wa kidikiteta na kijeshi nchini Argentina kuanzia mwaka 1976 hadi mwaka 1983. Nyaraka hizi zinahifadhiwa kwenye kumbu kumbu za Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina, Sekretarieti kuu ya Vatican pamoja na kwenye Ubalozi wa Vatican huko Bueons Aires.

Utunzaji wa nyaraka hizi kwa mfumo wa kidigitali ni utashi wa Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mwendelezo wa kazi iliyokuwa imefanywa katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita na Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina na sasa imekamilika. Kwa sasa pande hizi mbili zinataka kuanzisha itifaki itakayozingatiwa, ili kuwaruhusu watu mbali mbali kuweza kujionea wenyewe hali ilivyokuwa wakati wa utawala wa kijeshi nchini Argentina.

Nyaraka hizi zitaweza kutumiwa na ndugu, jamaa na waathirika wa ukatili na unyanyasaji uliofanywa wakati wa utawala wa kijeshi nchini Argentina. Wafungwa, watawa na viongozi wa Mashirika ni kati ya walengwa wakuu wa nyaraka hizi ambazo kwa sasa zinakwenda kwa mfumo wa kidigitali. Kazi hii kubwa na nyeti imetekelezwa kwa ajili ya kusimama kidete kulinda, kutangaza na kushuhudia: ukweli, haki na amani; ili hatimaye, kusaidia mchakato wa majadiliano  katika ukweli na uwazi pamoja na ujenzi wa madaraja ya watu kukutana na kusaidiana.

Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina, anapenda kuiweka nchi ya Argentina chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa huruma wa Lujan pamoja na maombezi ya Mtakatifu Josè Gabriel wa Rozari takatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.