2016-10-25 14:30:00

Siku kuu ya Deepavali: Jengeni matumaini kwa familia!


Wahindu na Wakristo wanahamasishwa kujenga matumaini kwa familia: ndiyo kauli mbiu inayoongoza ujumbe wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, kama sehemu ya maadhimisho ya Siku kuu ya Deepavali kwa waamini wa dini ya Kihindu duniani, itakayoadhimishwa hapo tarehe 30 Oktoba, 2016. Ni matumaini ya Baraza hili kwamba, Sherehe hizi sehemu mbali mbali za dunia zitasaidia kujenga na kuimarisha tunu msingi za maisha ya kifamilia pamoja na kuleta furaha na amani kwenye familia na jumuiya mbali mbali.

Ubora wa maisha ya kifamilia unategemea kwa kiasi kikubwa na mshikamano wa kifamilia, ingawa katika ulimwengu mamboleo, dhana ya familia inapata mwelekeo tenge mintarafu maana ya familia na tunu zake msingi kutokana na kutopea kwa Imani. Kutokana na mwelekeo kama huu, familia nazo zinajikuta zikipita katika mazingira magumu ya: kinzani, umaskini na uhamiaji, jambo ambalo kwa sasa limekuwa ni kitu cha kawaida kabisa duniani.

Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini linaendelea kusema, licha ya kasoro zote hizi, bado kuna alama kubwa za upyaisho wa matumaini ndani ya familia kutokana na ushuhuda unaotolewa na watu ambao wamesimama kidete katika misingi ya ndoa na familia, kwa kuenzi ustawi na maendeleo ya kila mtu na jamii katika ujumla wake. Kwa kuheshimu familia pamoja na kutambua changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo, Baraza linapenda kutafakari kwa pamoja, mambo msingi ambayo yanaweza kutumiwa na Wakristo pamoja na Wahindu ili kujenga matumaini ndani ya familia, ili hatimaye, jamii iweze kujikita zaidi katika ubinadamu.

Kimsingi familia ni shule ya kwanza ya ubinadamu na wazazi pamoja na walezi ni walimu wake wa kwanza. Watoto ndani ya familia wanaweza kujifunza vyema zaidi kutoka kwa wazazi, ndugu, jamaa na watu wazima, tunu msingi zinazoweza kuwasaidia kukua na hatimaye kuwajibika kikamilifu kama binadamu. Lakini, matumaini na mawazo ya vijana wengi wa kizazi kipya yanatoweka kama ndoto ya mchana kutokana na mazingira ya kifamilia wanayokumbana nayo kila siku. Kumbe, ni vyema zaidi, ikiwa kama wazazi na jamii katika ujumla wake, itasaidia kuwajengea watoto matumaini kwa kuwaongoza katika kesho iliyo bora zaidi, kwa kutafuta kilicho chema hata katika utofauti unaoweza kuwepo!

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, elimu na majiundo makini kwa watoto na vijana wa kizazi kipya ni dhamana nyeti inayopaswa kutekelezwa na wazazi pamoja na walezi; kwani inaakisi huruma ya Mungu inayokumbatia wote na kuwapatia maana ya maisha. Elimu na majiundo katika matumaini yawatie shime vijana wa kizazi kipya wenyewe kujitosa katika upendo na huduma kwa wengine na hivyo kuwa ni mwanga angavu kwa wale wanaoogelea katika giza.

Familia zinapaswa kuwa ni maabara ya matumaini, mahali ambapo watoto wanajifunza mifano bora kutoka kwa wazazi, walezi na ndugu zao nguvu ya matumaini inayoimarisha mahusiano ya kibinadamu, sanjari na kuwahudumia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na hivyo kuvuka mambo yote yanayosababisha ukosefu wa haki msingi za binadamu.

Itakumbukwa kwamba, mapambazuko na  maisha ya baadaye ya jamii yanapitia kwenye familia. Ikiwa kama binadamu wanataka kusonga mbele na kuishi kwa amani wanapaswa kukumbatia mchakato wa kurithisha matumaini kwa kuwatia shime watoto kuwa kweli ni warithi wa matumaini duniani. Mwishoni, Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, linahitimisha ujumbe kwa Siku kuu ya Deepavali kwa mwaka 2016 kwa kuwataka Wahindu na Wakristo kushikamana na watu wenye mapenzi mema ili kuunga mkono maisha ya ndoa na familia, ili hatimaye, familia ziweze kuwa ni shule za matumaini. Kwa njia hii, wataweza kupeleka mwanga wa matumaini kila pembe ya dunia, kwa kuwafariji na kuwaimarisha wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.