2016-10-25 09:11:00

Serikali ya mpito na umoja wa Kitaifa DRC: Uchaguzi mkuu, haki na huduma!


Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, DRC, linasema makubaliano yaliyofikiwa na vyama vya kisiasa nchini humo kuhusu uchaguzi mkuu, hauna budi kujikita zaidi katika ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi wa DRC badala ya kuangalia faida zinazoweza kupatikana kwa vyama husika. Hadi wakati huu, makubaliano haya hayajapanga wazi tarehe ambamo, mchakato wa uchaguzi mkuu utaanza kufanyika.

Wamekubaliana kimsingi katika tamko hili kwamba, wakati wa kipindi cha mpito kuelekea uchaguzi mkuu, kutaundwa serikali ya Umoja wa Kitaifa ambamo, Waziri mkuu atakuwa ni kutoka vyama vya upinzani wakati ambapo Rais Joseph Kabila ambaye anamaliza muda wake wa uongozi ataendelea kuliongoza taifa kama Rais. Itakumbukwa kwamba, tarehe 19 Desemba 2016, Rais Kabila atakuwa anahitimisha rasmi muda wake wa kuendelea kuwepo madarakani, lakini kutokana na makubaliano haya ya kisiasa, ataendelea kushika hatamu hadi pale serikali mpya itakapochaguliwa na wananchi wa DRC.

Wajumbe wa kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki DRC hivi karibuni walijitoa katika majadiliano kati ya Serikali na vyama vya upinzani, kwani hakukuwepo na uwakilishi mpana zaidi wa vyama vyote vya upinzani. Wapinzani wanaomuunga mkono Etienne Tshisekedi hawakushirikishwa katika majadiliano wala utiaji wa sahihi katika makubaliano haya ambayo yanaitaka Serikali ya mpito kuwemo madarakani hadi mwaka 2017.

Makubaliano haya ya kisiasa pamoja na mambo mengine, yanataka ufafanuzi wa kina kuhusu madaraka ya serikali na mambo msingi ambayo yatapaswa kuzingatiwa na Serika ya Umoja wa Kitaifa, Bunge na Tume itakayoundwa wakati huu wa kipindi cha mpito kuelekea uchaguzi mkuu. Baraza la Maaskofu Katoliki DRC linakaza kusema, hapa Katiba ya nchi ambayo ni sheria mama inapaswa kuheshimiwa na kuzingatiwa na wote kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi.

Mambo msingi yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na Serikali ya mpito ni: maandalizi ya uchaguzi mkuu; haki msingi za binadamu; maboresho ya maisha ya wananchi kwa njia ya huduma makini ya afya, elimu na uchumi. Tarehe 30 Oktoba 2017 iwe ni siku ya mwisho ya kuwasilisha majina ya wagombea uchaguzi mkuu nchini DRC, ili kuwawezesha wananchi kupiga kura ifikapo mwezi Aprili 2018. Baraza la Maaskofu Katoliki DRC linataka kujielekeza zaidi katika kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, maridhiano, umoja na mshikamano wa kitaifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.