2016-10-25 07:07:00

Papa akutana na Rais Maduro wa Bolivia ya Venezuela mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu jioni, tarehe 24 Oktoba 2016 amekutana na kufanya mazungumzo ya faragha na Rais Nicolàs Maduro Moros wa Bolivia ya Venezuela. Mazungumzo haya yamefanyika wakati kuna hali tete sana ya kisiasa, kijamii na kiuchumi nchini Venezuela. Wananchi wengi wameathirika kutokana na hali hii kiasi hata cha kukata tamaa ya maisha.

Baba Mtakatifu Francisko ambaye anakumbatia ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi nchini Venezuela, anatamani kuendeleza mchakato utakaosaidia kurejesha tena utawala wa kikatiba sanjari na kuchangia hatua mbali mbali zitakazochangia kutatua shida na kinzani zinazokwamisha majadiliano ya kisiasa, ili hatimaye, makundi yanayohusika yaweze kujenga moyo wa kuaminiana.

Baba Mtakatifu anamwalika Rais Maduro wa Venezuela kuonesha ujasiri zaidi kwa kujikita katika mchakato wa majadiliano unaojikita katika ukweli na uwazi, ili kuondoa mateso na mahangaiko ya wananchi wa Venezuela, lakini zaidi kwa maskini. Baba Mtakatifu amemshauri Rais Maduro kujenga mazingira yatakayosaidia kupyaisha mchakato wa mafungamano ya kijamii, ili wananchi waweze kuwa na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.