2016-10-24 08:30:00

Sakramenti za Huruma ya Mungu: Ekaristi Takatifu & Upatanisho!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu imekuwa ni fursa makini ya kutafakari na hatimaye kumwilisha huruma ya Mungu katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Waamini wamepata nafasi kuguswa na utume wa Kristo Yesu, Sura ya ufunuo wa Mungu kwa mwanadamu na kwamba, hiki kimekuwa ni kipindi cha kurejea katika mambo msingi yanayogusa imani ya Kikristo, ili hatimaye, waamini waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu inayofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa linayo dhamana na jukumu la kutangaza na kushuhudia huruma ya Mungu kwa kutambua kwamba, Kanisa ni tunda la upendo wa Kristo na kwamba, linatumwa kuwashirikisha walimwengu wote kwa njia ya huduma makini inayotolewa kwa wote pasi na ubaguzi. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Padre Wojciech Adam Koscielniak, mmoja wa Wamissionari wa huruma walioteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anasema, Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho ni Sakramenti za huruma ya Mungu zinazomkirimia mwamini upendo, huruma na msamaha.

Anasema, Sakramenti ya Upatanisho ni mahakama ya huruma ya Mungu inayomwezesha mwamini kutafiti dhambi zake, kutubu, kuungamana na kutimiza malipizi, tayari kuanza maisha mapya yanayomwezesha mwamini kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka, Kisima cha huruma ya Mungu. Hapa waamini wanaponywa na kupewa neema ya kuendelea na mapambano ya maisha ya kiroho, hadi kuufikia uzima wa milele. Waamini wajenge utamaduni wa toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata huruma ya Mungu inayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Upatanisho.

Padre Wojciech Adam Koscielniak anaendelea kufafanua kwamba, maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu yanawapatia waamini nguvu kutoka katika Neno la Mungu pamoja na kupokea Mwili na Damu Azizi ya Kristo inayowawezesha kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa njia ya huduma. Hapa waamini wanaalikwa kuwa ni Ekaristi, mkate unaomegwa kwa ajili ya huduma kwa jirani. Kumbe, waamini wakishiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho, wanaweza kuwa kweli ni mashuhuda wa huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.