2016-10-24 09:28:00

Maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani kwa mwaka 2018


Maadhimisho ya Siku ya 9 ya Familia Duniani kwa mwaka 2018 yatafanyika Jimbo kuu la Dublin, Ireland kuanzia tarehe 22 – 26 Agosti 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Injili ya Familia: Furaha ya Ulimwengu”. Viongozi wakuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland wamewasilisha matumaini na matarajio ya familia ya Mungu nchini Ireland wakati wa maadhimisho haya.

Askofu mkuu Eamon Martin wa Jimbo kuu la Armagh pamoja na Askofu mkuu Diamuid Martin katika uzinduzi huu uliofanyika Jumamosi, tarehe 22 Oktoba 2016 wakati wa maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Mtakatifu Yohane Paulo II wanasema, litakuwa ni jukumu la Kanisa nchini Ireland kusaidia kuhamasisha kwa kina  na mapana umuhimu wa ujenzi wa Familia ya Kikatoliki, dhamana ambayo inapaswa kuchangiwa na wadau katika ngazi mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa. Mkazo utakuwa ni matayarisho mazuri ya wanandoa watarajiwa pamoja na Kanisa kuendelea kuwasindikiza katika hija ya maisha yao ya ndoa ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya familia inayojikita katika Injili ya uhai.

Maadhimisho haya yanakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na ukweli kwamba, si rahisi kuweza kuwaunganisha wananchi wote wa Ireland kusimama kidete, kulinda, kudumisha na kushuhudia Injili ya familia kutokana na mitazamo mbali mbali ya kijamii kuhusu maisha ya ndoa na familia. Kuna baadhi ya wananchi ambao wamepoteza kabisa dhana ya familia katika maisha yao.

Viongozi wa Kanisa Katoliki wanayo furaha na changamoto kubwa mbele yao kuwasilisha mwono sahihi wa dhana ya ndoa na familia: Habari Njema kwa binadamu kwamba, maisha ni matakatifu na yanapata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu aliyewaumba kwa sura na mfano wake.  Maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani kwa Mwaka 2018 ni mwendelezo wa maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu kuhusu familia zilizofanyika hivi karibuni mjini Vatican na hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko akachapisha Wosia wake wa Kitume kuhusu “Furaha ya upendo katika familia”

Baba Mtakatifu Francisko amechagua kauli mbiu “Injili ya Familia: Furaha ya Ulimwengu” kuwa ni mwongozo wa maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani kwa Mwaka 2018, ili kuwawezesha waamini kuwa na mang’amuzi na uzoefu binafsi kuhusu Injili ya familia, tayari kushirikishana uzoefu na mang’amuzi haya na watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili wote kwa pamoja waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya familia inayojikita katika Injili ya uhai.

Ni mwaliko wa kuendelea kujikita katika sala, kama ilivyokuwa kwa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu sanjari na kuwasaidia wanandoa watarajiwa ili kufahamu na hatimaye, kuliambata kabisa Fumbo la maisha ya ndoa na familia kama sehemu ya mchakato wa kutakatifuzana, ili kwamba, wanandoa hawa kwa pamoja waweze kufika mbinguni kwa Mwenyezi Mungu kwani walipokuwa hapa duniani, wameweza kutangaza na kushuhudia Injili ya familia inayofumbatwa katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Maisha ya ndoa na familia hayana budi kuwa ni mwendelezo wa matukio muhimu katika maisha ya waamini yaani: Sakramenti ya Ubatizo, Kipaimara, Ekaristi Takatifu bila kusahau nyakati za furaha, shida na matumaini katika maisha ya mwanadamu. Waamini watambue tena na tena umuhimu wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, kwani katika Ibada hizi, hata wale wanaodhani kwamba, wamesahauliwa na kutelekezwa na Mama Kanisa wanaonja tena ndani mwao ile dhamana ya Kanisa kama Mama na mwalimu anayefundisha, anayeonya ; Mama anayefariji, anayeganga na kuponya kwa mafuta ya huruma na msamaha

Maisha ya ndoa na familia yanakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, inayoambata pia tabia ya ukanimungu, utamaduni wa kifo pamoja na ndoa za watu wa jinsia moja, tatizo kubwa linaloendelea kupigiwa debe hata na viongozi wa Mataifa makubwa. Kanisa halina budi kusimama kidete kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili ya familia kwa walimwengu mamboleo.

Maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani kwa Mwaka 2018 hulo Dublin, Ireland ni fursa nyingine tena ya kuweza kupyaisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kwa watu wa kizazi hiki. Dhamana hii inapaswa kuungwa mkono na wadau katika medani mbali mbali za maisha, ili kukuza na kudumisha mafao ya wengi, kwani Jamii isiyotoa kipaumbele cha pekee kwa maisha ya ndoa na familia, mustakabali wake kwa siku za usoni uko mashakani!

Kanisa linataka kuwaunganisha watu, ili wajisikie kuwa ni sehemu kubwa ya familia ya Mungu inayowajibika, tayari kujielekeza ili hatimaye, kuzaa matunda ya utakatifu wa maisha kuanzia katika ngazi mbali mbali za familia ya Mungu ndani na nje ya Ireland.  Taarifa za awali zinaonesha kwamba, zaidi ya wajumbe 700 wanatarajiwa kushiriki katika maadhimisho haya. Ujumbe wa maadhimisho ya Siku ya 9 ya Familia Duniani kwa Mwaka 2018 umezinduliwa rasmi wakati Kanisa linaadhimisha kumbu kumbu ya Mtakatifu Yohane Paulo II ambaye kunako mwaka 1992 kama sehemu ya mikakati yake ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya familia, alianzisha maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani na kwa mara ya kwanza maadhimisho haya yakafanyika mjini Roma kunako mwaka 1994, Jumuiya ya Kimataifa ilipokuwa inaadhimisha Mwaka wa Familia.

Tangu wakati huo, maadhimisho haya yamekuwa yakifanyika kila baada ya miaka mitatu, muda wa sala, tafakari, majadiliano na ushirikishwaji wa furaha, shida na mang’amuzi yanayochimbuka kutoka katika Injili ya familia. Mara ya mwisho, maadhimisho haya yamefanyika Jimbo kuu la Philadelphia, Marekani, kunako mwaka 2015.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.