2016-10-22 16:52:00

Mtakatifu Yohane Paulo II, Jembe la huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi, tarehe 22 Oktoba 2016 akizungumza na mahujaji kutoka Poland waliofika kwa wingi mjini Vatican kama sehemu ya mwendelezo wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 1050 ya Ukristo nchini Poland, anamshukuru Mungu aliyewakirimia zawadi ya imani kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo pamoja na wema wote aliowatendea vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka 2016, Jimbo kuu la Cracovia.

Baba Mtakatifu anaungana na Familia ya Mungu kutoka Poland, ili kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani, aliyemwezesha kutembelea na kuifahamu nchi ya Poland, mahali alipozaliwa Mtakatifu Yohane Paulo II, ambaye Kanisa limeadhimisha kumbu kumbu yake tarehe 22 Oktoba 2016. Akiwa nchini Poland anasema, alibahatika kutembelea maeneo mbali mbali yanayogusa maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Paulo II shuhuda na mtume wa huruma ya Mungu. Ni kiongozi aliyejitambulisha na wale wote waliokuwa wanateseka na kusukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu Francisko anamshukuru Mungu kwa kumkirimia nafasi ya kukaa kimya na kutafakari kwenye kambi za mateso za Auschwitz- Birkenau. Katika kimya hiki kikuu, ujumbe wa huruma ya Mungu unapata umuhimu wa pekee kabisa. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua nafasi hii kuishukuru familia ya Mungu nchini Poland kwa mapokezi makubwa ya kukata na shoka waliyomwonesha wakati wa hija yake ya kichungaji nchini Poland. Ni maadhimisho ambayo yalikuwa na maandalizi makubwa ya kisanaa na katika maisha ya kiroho; matukio ambao yameadhimishwa kwa imani kubwa.

Miaka 30 iliyopita kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kwa mara ya kwanza ilisikika sauti ya Papa Yohane Paulo II akiwataka watu wote duniani kutokuwa na woga, bali wamfungulie Kristo malango ya maisha yao. Maneno haya yakawa ni mwanzo wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, kiongozi aliyejikita katika maisha ya kiroho, akawarithisha walimwengu utajiri wa historia na utamaduni wa wananchi wa Poland uliofumbatwa katika imani kizazi baada ya kizazi.

Urithi huu kwa Yohane Paulo II, ulikuwa ni chemchemi ya matumaini, nguvu na ujasiri uliokuwa unamsukuma kuwahamasisha watu wa mataifa kumfungulia Kristo malango ya maisha yao. Mwaliko huu, ukawa ni kauli mbiu ya mwendelezo wa maadhimisho ya huruma ya Mungu hadi kwa watu wa nyakati hizi; tukio linalofumbatwa katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu anaitakia familia ya Mungu nchini Poland neema na baraka ya kuendelea kudumu katika imani, matumaini na mapendo waliyorithi kutoka kwa wazazi wao; urithi ambao wanaulinda kwa nguvu zao zote.

Wananchi wa Poland waendelee kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma, ili kuwawezesha watu wengi zaidi kuwa ni mashuhuda pia wa huruma ya Mungu kwa maskini na wahitaji wote. Baba Mtakatifu anawaomba kuendelea kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala! Hija za maisha ya kiroho wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ziwe ni kielelezo cha imani, mang’amuzi ya msamaha na huruma ya Mungu kwa watu wote, lakini zaidi kwa maskini na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi! Waamini waendelee kulisindikiza Kanisa kwa sala na sadaka ili liweze kutekeleza dhamana na wajibu wake wa Uinjilishaji wa kina sehemu mbali mbali za dunia, lakini zaidi kwenye nchi za kimissionari.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.