2016-10-22 08:52:00

Kanisa la Kimissionari, shuhuda wa huruma!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni mchakato unaopania kutambua na kuiambata huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu, tayari kuishuhudia kwa kuimwilisha katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Tarehe 23 Oktoba 2016, Mama Kanisa anaadhimisha Siku ya 90 ya Kimissionari Duniani inayoongozwa na kauli mbiu “Kanisa la Kimissionari, shuhuda wa huruma”. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia huruma ya Mungu mintarafu, wito na hali ya kila mwamini, ili kushiriki katika utume wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu inayojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Takwimu za maisha na utume wa Kanisa hadi kufikia tarehe 31 Desemba 2014 kumekuwepo na ongezeko la Wakatoliki duniani wapatao 18, 355, 000. Ongezeko hili kwa Bara la Afrika ni waamini 8, 535, 000. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 0.38%. Wakati idadi ya waamini inaongezeka Barani Afrika, lakini idadi ya Mapadre wanaowahudumia inaendelea kupungua. Majimbo makuu yaliyoundwa kwa mwaka 2014 yalikuwa ni 9 na moja ni kutoka Barani Afrika. Idadi ya Maaskofu imeongezeka na kufikia Maaskofu 5, 237 na Barani Afrika imepata ongezeko la Maaskofu 5.

Takwimu zinaonesha kwamba, idadi ya Mapadre duniani inaendelea kuongezeka na Bara la Afrika limebahatika kupata majembe 1, 089, wakati idadi ya Mapadre Barani Ulaya, Amerika na Oceania inaendelea kupungua mwaka hadi mwaka. Idadi ya Watawa wasiokuwa Mapadre inaendelea kupungua mwaka hadi mwaka. Idadi ya wamissionari walei na makatekista inaendelea kuongezeka Barani Afrika. Idadi ya Majandokasisi inaendelea kupungua sehemu mbali mbali za dunia, lakini takwimu zinaonesha kwamba, idadi ya waseminari Barani Afrika inaongezeka.

Kanisa Katoliki ni mdau mkubwa katika huduma za elimu kuanzia ngazi ya chini kabisa hadi elimu ya juu na vyuo vikuu. Kanisa lina shule za awali 73, 580 zinazowahudumia watoto 7, 043, 634; kuna shule za msingi 93, 283 zinazotoa huduma ya elimu kwa wanafunzi 33, 516, 860. Shule za Sekondari ni 46, 339 zinazowahudumia wanafunzi 19, 760, 924 na wengine 2, 477, 636 wanahudumiwa kwenye shule zenye kidato cha nne na cha tano. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna wanafunzi 2, 719, 643 wanaosoma katika taasisi za elimu na vyuo vikuu sehemu mbali mbali za dunia.

Kanisa Katoliki limeendelea kujipambanua katika huduma kwenye sekta afya kwa kumiliki na kuendesha hospitali, vituo vya afya na zahanati; vituo vya watoto yatima, nyumba za wazee pamoja na vituo vya huduma kwa waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi na Ukoma, ili kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya maisha inayofumbatwa katika huruma ya Mungu. Zote hizi ni juhudi za Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha waamini wote kwamba, wanapaswa kuchangia kwa hali na mali katika shughuli za Uinjilishaji. Sadaka na matoleo yote ya Siku ya Kimissionari Duniani, tarehe 23 Oktoba 2016 yatapelekwa kwa ajili ya kusaidia mchakato wa Uinjilishaji hadi miisho ya dunia, kielelezo makini cha umoja na mshikamano wa Kikanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.