2016-10-21 14:47:00

Kanisa linawahitaji Mapadre: wakomavu, watulivu, hodari na wakarimu!


Miito: “Akamwangalia kwa huruma, akamchagua” “Miserando atque eligendo” ni maneno ya kauli mbiu ya Kongamano la kimataifa kuhusu miito yaliyochukuliwa kwenye Nembo la Kiaskofu ya Baba Mtakatifu Francisko, kama kumbu kumbu endelevu ya maisha ya wito wake alipokuwa kijana, pale Mwenyezi Mungu alipomwangalia kwa huruma na kumchagua. Shughuli za kichungaji kuhusu miito ni mchakato wa kukutana na Kristo Yesu, tayari kumchagua na kumwambata katika maisha. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 21 Oktoba 2016 alipokutana na kuzungumza na washiriki wa Kongamano la kimataifa kuhusu miito lililoandaliwa na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri.

Shughuli za kichungaji kuhusu miito ni mwaliko wa kujifunza mtindo wa maisha ya Yesu anayefanya hija katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu, bila haraka, kwa kuwaangalia watu kwa jicho la huruma linalowawezesha kukutana na Mwenyezi Mungu. Habari Njema ya Wokovu inaonesha jinsi ambavyo Yesu katika maisha na utume wake alivyotembea na kukutana na watu waliokuwa wanateseka na hivyo kuwawezesha kuonja uwepo wa Mungu kati yao, ili kuwapatia chachu ya mageuzi inayopania kuwapatia mwelekeo mpya wa maisha.

Yesu katika maisha yake alijikita katika mambo makuu matatu: alitoka, akaona na kuita, mchakato unaojionesha kwa namna ya pekee katika maisha ya Mathayo mtoza ushuru. Ili kutoka, Kanisa halina budi kujielekeza na kuambata huruma ya Mungu katika utekelezaji wa dhamana na wajibu wake katika kukuza na kudumisha miito mitakatifu ndani ya Kanisa badala ya kutegemea nguvu za kibinadamu au woga usiokuwa na mashiko wala mvuto. Huduma za kichungaji zinahitaji ujasiri, ubunifu na mikakati mipya na makini ili kufikia malengo yanayokusudiwa mintarafu: miundo mbinu, mtindo wa maisha na njia za uinjilishaji unaotekelezwa na Jumuiya husika. Waamini wajifunze kutoka katika ugumu wa mioyo yao tayari kushuhudia na kutangaza Furaha ya Injili badala ya kuendelea kutumbukia katika mambo yanayogumisha mchakato huu!

Baba Mtakatifu anawakumbusha Wakleri na viongozi wa Kanisa kwamba, wao ni wahusika wakuu wa miito mitakatifu ndani ya Kanisa, dhamana wanayopaswa kuitekeleza kwa dhati, ili kuleta mageuzi katika maisha ya watu kwa kuguswa kwanza kabisa na uzuri wa upendo wa Mungu katika maisha. Viongozi wa Kanisa wawe na ujasiri wa kutoka ili kukutana, kuwasikiliza na kuwasaidia vijana kufanya mang’amuzi ya kina kuhusiana na wito katika maisha yao.  Wachungaji wajitahidi kuwa kati ya watu kwa ajili ya watu pamoja na watu, ili kujenga huduma ya kichungaji inayojikita katika mchakato wa watu kukutana, ukarimu na hasa zaidi kwa kuwasikiliza vijana wa kizazi kipya.

Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa kuona kwa kuangalia kwa makini pasi na haraka ya maisha kama alivyofanya Kristo Yesu, ili kukutana na watu na kuwapatia fursa ya kuweza kusikia sauti ya Kristo ndani mwao. Wachungaji waoneshe uso wa huruma unaofumbata upendo wa dhati, tayari kumpatia mwamini nafasi nyingine tena ya kuangalia maisha yake na tayari kuanza safari mpya bila ya kuhukumu wala kumshutumu mtu. Jicho la kichungaji lisaidie kuwaonesha watu uzuri wa Injili kwa kuwachangamotisha vijana kuwa na mwelekeo mpya wa maisha. Hili ni jicho la mang’amuzi, linalomsindikiza mtu kukutana na neema ya Mungu. Hili ni jicho makini na angavu linaloendelea kujitakasa.

Baba Mtakatifu anawataka viongozi wanaohusika na uteuzi wa vijana kuingia Seminarini kuwa na jicho tambuzi na angalifu; kwa kukazia mambo msingi. Maaskofu wawe makini na busara, kwani Kanisa linawahitaji Mapadre wakomavu na watulivu; wachungaji hodari na wakarimu; wanaoweza kuwakaribia watu, kuwasikiliza na kuwahurumia.

Tendo la tatu katika huduma za kichungaji ni kuita kunakompatia mwamini fursa ya kuchagua mwelekeo mpya wa maisha kama alivyofanya Yesu kwa Mathayo mtoza ushuru, akaacha yote na kumfuasa. Vijana ni hazina kuhimu sana ambayo Mwenyezi Mungu anapenda kuwakabidhi viongozi wa Kanisa ili kulinda, kuitunza na kuiendeleza pasi na kukata wala kukatishwa tamaa hata pale mavuno yanapokuwa haba. Vijana waulizwe maswali msingi na kuanza hija ya maisha mapya ili kugundua Furaha ya Injili.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hii ni dhamana nyeti na wakati mwingine mavuno ni haba, lakini viongozi wa Kanisa hawana budi kujizatiti daima kutoka kwa ajili ya kuwatangazia watu Injili kwani Yesu daima yuko pamoja nao ili kuwapatia ujasiri wa kutweka hadi kilindini, hata pale wanapoonekana kuwa wamechoka na kukata tamaa bila ya kupata mavuno! Kwa namna ya pekee, Maaskofu watoke, ili kupandikiza Neno kwa jicho la huruma kwani wao wamekabidhiwa dhamana hii wanayopaswa kuitekeleza kwa kuwa na mang’amuzi, sala pamoja na kutumia mbinu muafaka katika Uinjilishaji pamoja na kukuza miito mitakatifu ndani ya Kanisa.

Watangaze Injili pasi na woga, wakutane na kuwaonesha vijana dira ya maisha ya Kipadre na kitawa, kwa njia ya ushuhuda unaosimikwa katika furaha ya kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani pamoja na kuendelea kujiaminisha mbele ya Mungu kwa kumwomba ili aweze kupeleka watenda kazi katika shamba lake. Maaskofu waendeleze dhamana hii kwa njia ya sala. Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba yake kwa kusema kwamba, huduma za kichungaji ni msingi wa Kanisa dhamana inayotekelezwa na Wakleri pamoja na waamini walei. Huu ni utume wa dharura ambao Mwenyezi Mungu anawataka kuutekeleza kwa ukarimu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.