2016-10-20 09:32:00

Simameni kidete kulinda na kuwatetea watoto wadogo!


Baba Mtakatifu Francisko katika barua aliyomwandikia Kardinali Raymundo Damasceno Assis wa Jimbo kuu la Aparecida, nchini Brazil wakati huu, Kanisa katoliki nchini Brazil linapoadhimisha Juma la Watoto nchini humo, anawataka viongozi wa Kanisa kuwa mstari wa mbele katika kuwalinda na kuwatetea watoto, ili kusaidia mchakato wa ukuaji wa jamii nzima ya Brazil.

Baba Mtakatifu anawataka viongozi kutenga muda wa kuweza kukaa, kuwasikiliza, kusali na kucheza pamoja na watoto na kuacha mtindo wa sasa ambao, hautoi nafasi kwa viongozi wa Kanisa kuwa pamoja na watoto katika malezi na makuzi yao. Ujumbe wa Baba Mtakatifu umesomwa kwa niaba yake na Kardinali Raymundo Damasceno Assis wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria wa Aparecida, msimamizi wa nchi ya Brazil, kama sehemu ya maadhimisho ya ufunguzi wa Mwaka wa Jubilei ya Bikira Maria wa Aparecida.

Hii ni kumbu kumbu ya miaka 300 tangu Sanamu ya Bikira Maria wa Aparecida ilipopatikana kwenye maji ya mto “Paraiba do sul”. Baba Mtakatifu Francisko anaunga mkono kampeni ya Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil katika mapambano dhidi ya unyanyaswaji, udhalilishwaji na utumikishwaji wa watoto wadogo katika kazi za suluba.

Hizi ni juhudi zinazofanywa na Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil kwa kushirikiana na Serikali pamoja na wadau mbali mbali katika mapambano dhidi nyanyaso hizi, ili hatimaye, kutoa fursa kwa watoto kupata elimu bora itakayowahakikishia ustawi na maendeleo kwa sasa na kwa siku za usoni. Baba Mtakatifu bado anakumbu kumbu hai ya uzinduzi wa Sanamu ya Bikira Maria wa Aparecida, uliofanywa mjini Vatican, hapo tarehe 3 Septemba 2016. Ikumbukwe kwamba, watoto ni alama ya matumaini na kiashiria cha ubora wa maisha ya familia, jamii na ulimwengu katika ujumla wake. Pale watoto wanapopokelewa na kupendwa; wanapolindwa na kuendelezwa na familia yenye hekima, jamii inaboreka na ulimwengu unakuwa na utu zaidi, changamoto kwa watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete kuwalinda, kuwatunza na kuwaendeleza watoto.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba mchakato wa usitishwaji wa kazi za suluba miongoni mwa watoto wadogo utakuwa ni matunda makubwa ya ushiriki wa wadau mbali mbali kwa ajili ya ustawi na mafao ya watoto. Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa Baraza la Maaskofu wakati wa maadhimisho ya Juma la kulinda watoto wadogo nchini Brazil kwa kuwapatia baraka zake za kitume, huku akiwaomba kumkumbuka na kumsindikiza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.