2016-10-19 11:53:00

Mapadre kuweni mashuhuda na vyombo vya haki, msimezwe na malimwengu


Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri, Jumanne, tarehe 18 Oktoba 2016 amezindua rasmi maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu Chuo kikuu cha Kipapa cha Mexico kilichoko hapa mjini Roma kilipoanzishwa kama mahali pa kuwafunda Wakleri kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa nchini Mexico. Amewashukuru walezi wote waliojisadaka kwa ajili ya kuwafunda majandokasisi kutoka Mexico katika kipindi chote cha miaka 50 iliyopita.

Chuo hiki kimekuwa ni chemchemi ya: Sala ya Kanisa; Shule ya umoja na majadiliano katika ukweli na uwazi; mambo msingi katika ukuaji na ukomavu wa mtu kiroho na kimwili. Kardinali Stella, amewataka majandokasisi na wakleri kuhakikisha kwamba, wanaendelea kujikita katika majiundo awali na endelevu katika maisha na utume wao kama Mapadre, daima wakijitahidi kuiga mfano wa Kristo mchungaji mwema, ili kweli waweze kuishi na kutenda mintarafu matakwa ya Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa kutekeleza matashi yake.

Wito wa Upadre, kimsingi hautegemei juhudi za mtu binafsi, akili, nguvu wala uweza na ufahamu wake wa Mafundisho tanzu ya Kanisa, bali katika mahusiano ya kina na yenye mvuto na mashiko yanayojikita katika Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, kielelezo na utambulisho wa maisha na utume wa Padre. Mapadre wamepakwa mafuta ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, changamoto ni kuhakikisha kwamba, kweli Mapadre wanajitahidi kuishi wito wao kwa upendo na hamasa kubwa.

Kardinali Stella anawataka Wakleri kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuwafunda, kuwaongoza na kuwasindikiza katika maisha na wito wao, dhamana ambayo kimsingi ni endelevu, ili kushinda tamaa na malimwengu, kwa kutambua kwamba, wao ni Kristo mwingine. Wakleri wanapokumbana na udhaifu katika maisha na utume wao, daima wajitahidi kukimbilia huruma na upendo wa Mungu, ili aweze kuwaganga na kuwaponya, ili hatimaye, waweze kufurahia amani ya ndani; ukweli na uwaminifu; upole na kiasi.

Mapadre wakumbuke kwamba, wito, maisha na utume wao unakumbana na changamoto nyingi katika ulimwengu mamboleo. Ili kweli waweze kuwa ni Mapadre kadiri ya Kristo mchungaji mwema wanapaswa mosi: kuwa ni watu wa haki na mapendo wanaokita maisha yao katika tunu msingi za Kiinjili kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Pili, Mapadre wasikubali hata kidogo kumezwa na malimwengu kwa kuwa na uchu wa mali, fedha, madaraka na heshima; vishawishi ambavyo vinaweza kuwaponza Mapadre, wakajikuta wamebwaga manyanga katika maisha ya kiroho na kiutu! Tatu, Mapadre wawe kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa kuonesha ule moyo wa Msamaria mwema.

Kardinali Stella anawakumbusha viongozi wa Kanisa kwamba, wao kimsingi ndio walezi wakuu wa miito mitakatifu ndani ya Kanisa. Wanapaswa kusaidia kulea, kukuza na kudumisha miito mitakatifu, ili kweli Kanisa liweze kupata majembe ya nguvu, yaani Mapadre wema, waadilifu, wachapakazi na watakatifu; watu wenye mvuto na mashiko katika maisha na utume wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.