2016-10-19 15:53:00

Changamoto zinazowakabili Wayesuit katika maisha na utume wao!


Changamoto inayowakabili Wayeuit katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo ni kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa upatanisho, haki na amani; wanaendelea kujenga na kudumisha mahusiano mema na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwamba, wao pia wanapaswa kutoka huko walikojificha tayari kwenda pembezoni mwa jamii, ili kuwatangazia watu huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao!

Kimsingi haya ndiyo mambo makuu ambayo yamefafanuliwa na Padre Arturo Sosa  Abascal, Mkuu wa Shirika la Wayesuit  ambaye alikuwa ameandamana na Padre Federico Lombardi, Katibu mkuu msaidizi wa Wayesuit pamoja na Padre Patrick Mulemi, Msemaji mkuu wa Wayesuit. Padre Sosa akizungumza na waandishi wa habari waliofika kwenye mkutano wake wa kwanza uliofanyika kwenye Makao makuu ya Wayesuit mjini Roma, Jumanne, tarehe 18 Oktoba 2016 amesema kwa sasa ili Shirika liweze kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara linapaswa kujikita katika mambo makuu yafuatayo: Majiundo makini ya kiakili ili kuweza kuhudumia imani na pili kuwa uelewa mpana zaidi wa tamaduni za watu, ili kuinjilisha kwa kutamadunisha.

Padre Sosa anakaza kusema, haya ni mambo makuu ambayo kimsingi yanatambulisha wito, maisha na utume wa Wayesuit ndani ya Kanisa. Kuna idadi kubwa ya Wayesuit inayofanya utume wake wa kufundisha kwenye Vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu nchini China. Huu ni utume unaojikita katika utamadunisho na wala hauna uhusiano wa moja kwa moja na shughuli za kichungaji katika maisha ya kiroho, tofauti na utume unaotekelezwa na Wayesuit wanaoishi na kufanya kazi zao za kichungaji huko Macao, Hong Kong na Taiwan.

Katika mwelekeo wa kimataifa, Wayesuit mara baada ya maadhimisho ya mkutano mkuu wa 36 wanataka kujielekeza zaidi katika mchakato wa upatanisho, majiundo makini ya kiakili na maisha ya kiroho; hususan katika maeneo ambamo watu wanateseka kutokana na kinzani, vita na uchafuzi wa mazingira, ili waweze kujipatanisha na Mungu, jirani pamoja na mazingira, kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi mwanadamu!

Wayesuit kimsingi, wamekabidhiwa utume wa kuhudumia imani kwa kujikita katika haki na amani; utamadunisho pamoja na majadiliano ya kidini bila kusahau kuendeleza mchakato wa huduma kwa wakimbizi na wahamiaji, hasa wakati huu ambako kuna wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, jambo ambalo limekuwa ni changamoto kubwa hata kwa Jumuiya ya Kimataifa.

Kwa njia ya elimu wanataka kupambana na baa la njaa na umaskini wa hali na kipato. Wataka kujielekeza zaidi katika kukabiliana na changamoto ya mawasiliano ya kijami kwa kujikita katika tafiti pamoja na kuendeleza vyombo vya mawasiliano vinavyoendeshwa na kusimamiwa na Shirika hili. Wayesuit wangependa kuona haki, amani na mshikamano wa kitaifa vinatawala nchini Venezuela ambako kwa sasa hali ya kisiasa inaendelea kuwa tete zaidi. Kwa kushirikiana na Kanisa mahalia, Wayesuit wanapenda pia kuchangia katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Venezuela.

Padre Sosa anasema kwamba, anafahamiana na Baba Mtakatifu Francisko tangu kunako mwaka 1983 wakati wa mkutano mkuu ulioleta mageuzi makubwa ndani ya Shirika la Wayesuit baada ya Padre Pedro Arupo kung’atuka kutoka madarakani na kumkabidhi Padre Peter Hans Kolvenbach na tangu hapo wameendelea kukutana katika matukio mbali mbali, lakini zaidi tangu mwaka 2014 alipoteuliwa kuwa Msahauri mkuu kwenye Makao makuu ya Wayesuit yaliyoko mjini Roma. Padre Sosa amempongeza na kumshukuru mtangulizi wake Padre Adolfo Nicolas ambaye ataendeleza utume wake nchini Ufilippini kuwa kiongozi wa maisha ya kiroho katika kituo kimoja cha maisha ya kiroho.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.