2016-10-18 14:30:00

Kanisa linawapongeza na kuwashukuru Mapadre waaminifu na wachapakazi!


Kila mwaka ifikapo tarehe 18 Oktoba, Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Luka, Mwinjili na mwandishi wa kitabu cha Matendo ya Mitume kinachofafanua imani ya Kanisa la mwanzo. Kitaaluma alikuwa ni daktari na mmissionari mwenza wa Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa. Ni mwinjili anayeelekeza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wote, lakini akitoa upendeleo wa pekee kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili wote hawa waweze kushuhudia na kuonja huruma ya Mungu katika maisha yao.

Luka ni mwinjili pekee anayesimulia maisha ya utoto wa Yesu katika familia takatifu. Kwa namna ya pekee, Mwinjili Luka anaguswa na mahangaiko ya wagonjwa na maskini, ndiyo maana Injili hii inaitwa Injili ya faraja inayojikita katika sadaka ya Kristo Yesu Mkombozi wa ulimwengu! Luka kwa njia ya Kitabu cha Matendo ya Mitume analionesha Kanisa ambalo limefuata mafundisho ya Mitume ili kukuza na kudumisha: umoja na upendo unaopata chimbuko lake katika maadhimisho ya Sala ya Kanisa na Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa!

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku kuu ya Mwinjili Luka, wakati wa mahubiri yake, kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, amewapongeza na kuwashukuru wachungaji wema na watakatifu wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumfuasa Kristo Yesu bila kusukumwa na uchu wa mali, madaraka au sifa! Licha ya hata kuweza kutelekezwa na wote, lakini wanatambua kwamba, Kristo Yesu daima anaaambatana nao katika maisha na utume wao.

Mtakatifu Paulo kama ilivyokuwa kwa Mitume wengine wengi, mwishoni mwa maisha na utume wake, alijkuta akikabiliwa na upweke baada ya kutelekezwa na wengi. Hii ndiyo hali inayojitokeza hata wakati mwingine kwa Mapadre ambao wanajikuta katika utupu, wakitangatanga kutafuta riziki yao ya kila siku, lakini jambo la msingi wanapaswa kukumbuka kwamba, Kristo Yesu, daima yuko pamoja nao katika raha na mahangiko! Licha ya shida na magumu, lakini Mtakatifu Paulo alikuwa imara na mwenye amani na utulivu wa ndani katika maisha yake.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, hivi ndivyo ilivyokuwa hata kwa Yohane Mbatizaji, akajikuta akitupwa gerezani, akiteseka katika hali ya upweke; lakini alikuwa na matumaini kwa ushuhuda uliokuwa unaoneshwa na Yesu kuwa ndiye Masiha aliyekuwa anatazamiwa. Yohane Mbatizaji akakatwa kichwa kutokana na ahadi za Mfalme Herode zisizotekelezeka. Hivi ndivyo ilivyokuwa hata kwa Mtakatifu Marximilliano Maria Kolbe aliyeuwawa kikatili, kielelezo kwamba, mitume waaminifu na wa kweli daima hatima ya maisha yao ni Msalaba, unaoonesha uwepo wa karibu wa Kristo Yesu kwa wafuasi wake.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hii ndiyo Sheria ya Injili kwamba mbegu isiyokufa ardhini haiwezi kuzaa matunda na kwamba, baada ya mateso na kifo, kuna ufufuko wa wafu. Ikumbukwe kwamba, damu ya mashuhuda wa imani ni mbegu ya Ukristo. Sehemu ambazo kumekuwepo na dhuluma na nyanyaso kiasi cha Wakristo kumwaga damu yao, hapo Ukristo umekomaa na kuenea. Lakini pale ambapo wachungaji wanamezwa na malimwengu kutokana na uchu wa mali, madaraka na sifa, mara nyingi wanaishia pabaya.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, mara nyingi anapotembelea nyumba za Mapadre wazee anakutana na wachungaji ambao wamejisadaka bila ya kujiachilia kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, lakini sasa hawana nguvu tena, wako hoi vitandani, lakini bado hata katika hali kama ile, wanalo tabasamu la kukata na shoka, tayari kumshirikisha Baba Mtakatifu matumaini yao kwa Kristo na Kanisa lake. Mtume Paulo mwisho wa maisha yake anasema, wengine wote walimwacha isipokuwa Kristo Yesu ameambatana naye hadi dakika ya mwisho!

Mchungaji mwema hana budi kuwa na uhakika wa usalama katika maisha yake kwani daima Kristo Yesu ataambatana pamoja naye! Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuwaombea Mapadre wagonjwa na wale ambao wako kufani, huku wakiwa na matumaini ya kukutana na Kristo Yesu, ili wasijisikie wapweke, bali daima waonje uwepo endelevu wa Kristo Yesu hata katika hatua ya mwisho wa maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.