2016-10-15 10:36:00

Makardinali kufunga Malango ya Huruma ya Mungu tarehe 13 Novemba 2016


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu imekuwa ni fursa kwa familia ya Mungu kulitafakari kwa kina na mapana Fumbo la huruma ya Mungu, chemchemi ya furaha, utulivu na amani ya ndani. Baba Mtakatifu Francisko anasema, huruma ni neno linalowafunulia waamini Fumbo la Utatu Mtakatifu na kwa njia ya huruma hii, Neno wa Mungu amefanyika mwili na kielelezo cha juu kabisa cha huruma ya Baba.

Huruma ni sheria msingi katika maisha ya binadamu inayomfungulia malango ya kupendwa daima na Mwenyezi Mungu. Hiki kimekuwa ni kipindi ambacho Mama Kanisa amewataka watoto wawe wawe kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa njia ya matendo ya huruma, kielelezo cha imani tendaji! Itakumbukwa kwamba, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yalizinduliwa kunako tarehe 8 Desemba 2015, Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mama wa mlango wa huruma ya Mungu na wale wote waliobahatika kupitia lango hili wameonja mapendo ya Mwenyezi Mungu anayefariji, anayesamehe na anayewapatia waja wake matumaini mapya!

Baba Mtakatifu Francisko amewatea Makardinali watatu watakaoshiriki katika Ibada ya Kufunga Malango ya Mwaka wa Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu katika Makanisa makuu ya Kipapa Jimbo kuu la Roma hapo tarehe 13 Novemba 2016. Kardinali Agostino Vallini atafunga Lango la Huruma ya Mungu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano hapo tarehe 13 Novemba 2016 kwa Ibada ya Misa Takatifu.

Kardinali Santos Abril Y Castellò, Kiongozi mkuu wa Kanisa kuu la Bikila Maria Mkuu, atamwakilisha Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa hilo kama Ibada ya kufunga Lango la huruma ya Mungu, Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma. Kardinali James Michael Harvey, Kiongozi mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo nje ya kuta, atamwakilisha Baba Mtakatifu katika Ibada ya kufunga Lango la huruma ya Mungu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, nje ya kuta za Roma.

Lakini ikumbukwe kwamba, Baba Mtakatifu Francisko atakunja jamvi la maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu hapo tarehe 19 Novemba 2016 kwa Ibada ya kuwasimika Makardinali wateule, mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kutoka katika Makanisa mahalia sehemu mbali mbali za dunia. Kilele cha maadhimisho haya ni tarehe 20 Novemba 2016, Sherehe ya Kristo Mfalme wa Ulimwengu ambaye ufalme wake ni ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na neema; ufalme wa haki, mapendo na amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.