2016-10-13 12:02:00

Haki ya mtu haipotei hadi kieleweke!


Waswahili bwana wana mambo eti “Mnyonge, Mnyongeeni Haki yake mpeni.” Natumaini umewahi kuusikia msemo huo unaomhusu mtu aliyedhulumiwa haki yake. Hali hiyo inaweza kukutokea hata wewe unapokuwa katika mazingira ya kuonewa, kukosewa haki kuletewa maudhi kupita kiasi hata kushindwa kuvumilia, unakata tamaa na kuamua kulipa kisasi na kusema: “Uzalendo umenishinda.” Tatizo la kukata tamaa na kukosa uzalendo kwa mnyonge anayenyongewa haki yake, linaeleweka vizuri zaidi katika mazingira ya kihistoria ya jumuia ya Wakristo wa Asia ndogo.

Jumuiya hiyo ilikuwa inaishi katika mazingira magumu, kama tunavyosoma katika waraka wa Petro na katika kitabu cha Ufunuo. Wakristu hao walikosewa sana haki zao za msingi, walibaguliwa katika kazi, hawakuruhusiwa hata kufungua maduka na kuendesha biashara zao. Aidha walitupiwa lawama kwa kila ovu litokealo nchini. Kwa hiyo Wakristo hawa walishwawishika kukata tamaa na kukosa uzalendo dhidi ya hali hiyo.

Injili ya leo inatoa dawa ya kinga kwa mnyonge anayenyongewa haki yake ili asikate tamaa na kukosa uzalendo: “Bwana aliwaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu siku zote, wala wasikate tamaa.” Yaonesha kama vile ni mwaliko unaotudai kusali daima ili kutokata tamaa. Lakini hapa kutokata tamaa kwa kigiriki limetumika neno ekkakein lenye maana mbili katika kiingereza. Mosi, “to be out – eviling” yaani kukosa uzalendo na kuwa mbaya au mwovu. Pili “to-be being-despondent ” yaani kukosa matumaini na kukata tamaa kabisa. Hapa Yesu anataka kuonesha kuwa katika mazingira ya kukosewa haki, kama mnyonge anaacha kusali anaweza kukata tamaa na kukosa uzalendo. Sala ni kupanda hadi juu kwa Mungu na kujiunga na mawazo yake kwa njia ya Neno lake yaani Injili. Pendekezo hili la kusali daima linarudiwa sehemu mbalimbali katika Agano jipya. Mathalani “Katika dhiki, mkisubiri; katika kusali, mkidumu.” (Warumi 12:12).

Aidha, katika fasuli hii tunakuta mara nne neno hili “haki”. Halafu kuna wahusika watatu: Mosi, kuna Hakimu (Kadhi) anawakilisha mdhulumu au mtu anayenyima wengine haki yao. Pili, kuna Mjane anayewakilisha mtu mnyonge aliyedhulumiwa haki yake. Tatu, ni Yesu anayeipembua hali hii ya kadhi na mjane.

Kuhusu mhusika wa kwanza fasuli inasema: “Palikuwa na kadhi (hakimu) katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. Wajibu wa hakimu ni kutetea haki za wanyonge na wanaodhulumiwa. Kumbe hakimu huyu hakuwa mtu wa dini yoyote ile. Juu ya kukosa haki na kula rushwa Nabii Isaya alisema:“Ole wao wawekao amri zisizo za haki, na waandishi waandikao maneno ya ushupavu; ili kumpotosha mhitaji asipate haki yake, na kuwanyang’anya maskini wa watu wangu haki yao; ili wajane wawe mateka yao na kuwafanya yatima waliofiwa na baba zao kuwa mawindo yao!” (Isa 10:1-2). Aidha, “Wakuu wako Ee Israeli ni waasi, na rafiki za wevi; kila mtu hupenda rushwa, hufuata malipo; hawampatii yatima haki yake, wala maneno ya mjane hayawawasilii.” (Isaya 1:23). Hakimu huyu ametajwa hapa ili kuelezea hali halisi ya mazingira ya kukosewa haki anayolazimika mnyonge kuyaishi hapa duniani. Hii ndiyo jamii yetu ambayo hailingani na mpango wa Mungu. Kwa hiyo tunaalikwa kutafakari jinsi ya kuishi na kupata maana katika ulimwengu aina hiyo bila kukata tamaa na kukosa uzalendo.

Mhusika wa pili ni yule mnyonge anayedai haki yake: “Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane.” Katika Injili Yesu anawasema Waandishi jinsi wanavyowadhulmu wajane: “Wanatembea huku wamevaa kanzu ndefu. Wanapenda kusalimiwa na watu kwenye masinagogi. Wanawatoza wajane.” Yaonekana Waandishi hawa waliwatoza pesa wajane waliofika kuwaomba ushauri wa maisha. Mjane wa leo, alikuwa amedhulumiwa haki yake fulani. Aidha kuhusu kwenda kwa hakimu kwa kawaida ni wanaume ndiyo wanaenda mahakamani au kwa kadhi. Katika kesi hii anaenda Mjane labda kwa vile bwana wake alifariki. Hata hivyo hapa angeweza kwenda ndugu yake yeyote yule wa kiume kama vile kaka, mjomba, binadamu au hata rafiki nk.

Kwa hiyo, hapa tunaalikwa kumwangalia mjane katika mwanga wa kibiblia ili kuelewa ni kwa nini anaenda mjane. Katika Biblia picha ya kwanza ya mjane inaiwakilisha Taifa la Waisraeli lilipotekwa utumwani, linanyenyekeshwa, linaonewa na kudharauliwa na mataifa mengine. Taifa hilo likaitwa mjane. Picha ya pili ya mjane inahusu mji wa Yerusalemu (Kitabu cha Maombolezo). Mjane huyu anawakilisha jumuia ya mwinjili Luka iliyokuwa inadhulumiwa inaweza pia kuwakilisha hali ngumu inayomkumba mnyonge wa kila siku.

Mjane huyu alienda kwa hakimu (kadhi) kumwomba ampatie haki na adui wake. Kuomba huko maana yake ni kusali. Kwa hiyo sala (maombi) ni mbinu au njia ya kujipa nguvu ya kutokata tamaa na ya kukosa uzalendo. Asiyesali yuko katika hatari ya kukata tamaa na kukosa uzalendo. Mjane anamsisitizia hakimu: “nipatie haki na adui wangu.” naye hakimu hakutaka kumsikiliza. Baada ya kitambo fulani, hakimu akajifikiria na kusema: “Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kunijia daima.” Kwa Kigiriki neno hili ananiudhi, ni hupopiaze likimaanisha: “king’anganizi, kukamatika yaani kukera sana.

Hakimu yule aliamua kuingilia kati shauri hilo wala siyo kwa hoja ya kumwogopa Mungu. Aidha wala hakuwa na nia ya kuongoka na kuanza kufuata dini fulani, la hasha, kwake yeye haikumjalisha kuishi maisha mabaya. Lakini kwa vyovyote alikuwa na wasiwasi fulani unaogusa maslahi yake, na wa mambo yanayoweza kumvunjishia heshima na kumpotezea jina lake katika jamii anayoishi. Hivi akaona afadhali amtendee haki  mjane huyu. Kwa hiyo yawezekana pia kwamba haki hii ilikuwa kama rushwa ya kutetea maslahi au cheo chake, au kuomba kura kama wafanyavyo wagombea uongozi wa nchi wakati wa kampeni za kupiga kura kwa kuwagawia wanyonge pesa na vitu. Maana yake, hakumu hakusukumwa na mchocheo wowote ule wa kidini au wa kumwogopa Mungu katika kumtekelezea mjane huyu haki yake. Kwa hiyo hakimu huyu anaonesha kwamba kama kuna kitu fulani katika ulimwengu huu kinabadilika, ujue kinabadilika kutokana na matamanio tu ya mtu binafsi siyo lazima kuwe na mchocheo wa kidini au wa Kimungu. Huo ndiyo ulimwengu usiomwamini Mungu ambao Jumuiya ya Kikristo inabidi ijipange namna ya kuishi.

Mtu wa tatu ni Yesu (Bwana) anayeingilia kati na kutoa hukumu juu ya hali hii anaposema: “Mmesikia alichosema yule kadhi (hakimu) dhalimu” Huyu kadhi anatoa haki ili tu kujiridhisha mwenyewe binafsi. Kwa hiyo hapa unaona kwamba, wakati fulani na katika mazingira fulani, kunapatikana mwanya fulani unapoweza kuona haki inatendeka katika jamii lakini kwa motisha za kibinafsi tu au za kisiasa au kiulimwengu tu wa kibinadamu. Katika mwanya kama huo mfuasi wa Kristo hana budi awe na jicho kali sana la kuchunguza ili kupata mwanya wa kuingiza roho mpya ya fikra za ulimwengu wa Kimungu. Ndiyo maana Yesu anasema: “Na Mungu, Je, hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao?” Wateule wake wanaomlilia katika sala usiku na mchana kwa sababu wanataka ulimwengu mpya. Kama hawasali watakata tamaa na kukosa uzalendo. Hali hiyo inawapofushwa macho hata wasiweze kuona na kuupokea wakati ule unapokuja ule mwanya wa mabadiliko ya ulimwengu mpya yaani kunapotokea hali nzuri ya maisha ya haki katika jamii.

Yesu anahitimisha: “Nawaambia, atawapatia haki upesi.” Kwa Kigiriki En takei, yaani kamwanya fulani kamabadiliko ya haki katapatika tu. Hapo mfuasi wa Kristo budi achangamkie maswala, awe macho na kuutumia mwanya huo ili kuingiza ulimwengu mpya wa Mungu. Kwa hiyo Yesu anasema, hata kama itabidi kuusubiri mwanya huo kwa muda mrefu, dawa pekee inayoweza kutuponya na kutokata tamaa na kugeuka kuwa waovu ni sala yaani, daima kuwa na fikra za Mungu, kutafakari maneno ya Injili, kuwa na sala itakayotuwezesha kuuona mwanya huo.

Mwisho “Walakini atakapokuja mwana wa Adamu, Je, ataiona imani duniani?” Kwa vyovyote Yesu atakuja tu kuuchukua ulimwengu mpya kwa vile ametoa mwanya wa kutendeana kwa haki. Lakini kama husali hutaweza kuwa tayari kuupokea, na pengine huwezi hata kuona, kwa sababu utakuwa umepoteza kichwa, umekata tamaa na uzalendo umeshakushinda.

 

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.