2016-10-12 13:38:00

Bara la Afrika kupewa kipaumbele cha kwanza na G20


Chancellor Angela Merkel wa Ujerumani katika ziara yake ya kikazi nchini Ethiopia, Tarehe 11 Oktoba 2016 amesema kwamba, Ujerumani itatoa kipaumbele cha kwanza kwa Bara la Afrika wakati wa mkutano wa Nchi G20 utakaofanyika mjini Berlin kati kati ya mwaka 2017; ameutaka Umoja wa Afrika kusimamia mchakato wa mageuzi ya kiuchumi na kisiasa ili kupambana na vitendo vya kigaidi sanjari na kujikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi kama njia ya kujenga na kudumisha demokrasia, amani, utulivu na maendeleo ya wengi.

Bi Angela Merkel amehitimisha ziara yake ya siku tatu Barani Afrika iliyomwezesha kutembelea: Mali, Niger na Ethiopia kama sehemu ya mchakato wa ushirikiano wa kimataifa kati ya Ujerumaini na nchi za Kiafrika katika kukuza maendeleo endelevu, kupambana na wimbi kubwa la wahamiaji kutoka Barani Afrika, ambao wengi wao wanakufa maji hata kabla ya kutua nanga ya matumaini Barani Ulaya sanjari na kupambana na vitendo vya kigaidi vinavyohatarisha maisha na usalama wa Jumuiya ya Kimataifa.

Bi Angela Merkel ameitaka Serikali ya Ethiopia kujenga na kudumisha majadiliano na vyama pamoja na vikundi vya upinzani ili kukuza na kudumisha demokrasia na kwamba, maandamano ya upinzani ni muhimu kuruhusiwa. Vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kuwa makini katika kudhibiti maandamano ya raia, kwani hadi sasa maandamano ya upinzani nchini Ethiopia yamekwisha sababisha watu zaidi ya 500 kupoteza maisha yao.

Amesema, Ujerumani inataka kuwekeza katika sekta binafsi, ili kusaidia kutengeneza fursa za ajira kwa vijana kutoka Barani Afrika, lakini jambo la msingi ni Umoja wa Afrika kuhakikisha kwamba, miundo mbinu inaboreshwa na vijana kutoka Afrika wanapata elimu, ujuzi na maarifa yatakayowawezesha kupata ajira. Bara la Afrika linakadiriwa kuwa na idadi ya watu zaidi billioni 1. 2 na limekuwa likikabiliwa na changamoto ya wimbi kubwa la wahamiaji, hali ambayo imeulazimisha Umoja wa Ulaya kuanza mchakato wa ushirikiano wa kiuchumi na Nchi zilizoko Kaskazini mwa Afrika ili kupambana na changamoto hii ambayo ni hatari kwa usalama na maisha ya watu!

Bi Angela Merkel ameutaka Umoja wa Afrika kusaidia mchakato wa mageuzi ya kidemokrasia nchini Libya ambayo kwa sasa imegeuka kuwa ni uwanja wa vita. Ujerumani na Ethiopia zimewekeana sahihi mkataba wa ushirikiano utakaoiwezesha Ujerumani kutoa mafunzo kwa Jeshi la Polisi la Ethiopia. Waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn amesikika akisema kwamba, Ethiopia imejizatiti kuendeleza demokrasia ya mfumo wa vyama vingi vya kisiasa. Hali ya hatari iliyotangazwa nchini humo ni tukio la dharura kuwahi kutokea nchini humo katika kipindi cha miaka 25 iliyopita. Lakini, Serikali itasimama kidete kupambana na watu wanaotaka kuleta fujo na kuvuruga amani na usalama.

Bunge la Ethiopia limepitisha muswada wa sheria utakaoruhusu ushiriki wa vyama vingi vya upinzani katika uchaguzi mkuu ujao. Ethiopia ni kati ya nchi chache sana duniani ambayo inabeba mzigo mkubwa wa wakimbizi wapatao 780, 000 hali ambayo imeilazimisha nchi hiyo kuomba msaada kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa ili kukabiliana na changamoto hii. Bi Angela Merkel akiwa nchini Ethiopia amezindua pia jengo la Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika lililofadhiliwa na Ujerumani kwa kiasi cha Euro millioni 27. Hapa panatarajiwa kuwa ni mahali pa kuratibu shughuli za ulinzi na amani Barani Afrika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.