2016-09-22 08:09:00

Papa alaani mauaji ya kikatili ya Mapadre wawili Mexico


Kanisa Nchini Mexico limegubikwa na huzuni kubwa ya kuomboleza  vifo vya mapadre wawili waliouawa kikatili, baada ya kutekwa nyara.  Mapadre hao Alejo Nabori na Jose Alfredo , walikutwa wameuawa  huko Poza Rica, katika mkoa wa Mashariki wa Veracruz.  Taarifa inabaini watu wenye silaha waliwateka mapadre hao wakiwa katika eneo lao Kanisa la Mama Yetu wa Fatima, la Mjini Poza,  siku ya Jumapili, na miili yao ilipatikana Jumatatu ikiwa na majeraha makubwa ya risasi, na mtu wa tatu aliyekuwa  pamoja  nao akiwa bado hai.

Kwa taarifa hiyo, Papa Francisko, siku ya Jumanne, kwa huzuni kubwa,  alituma kwa salaam za rambirambi kwa familia na waamini wa Jimbo la Papantla kupitia Askofu Trinidad Zapata wa Jimbo la Papantla. Papa  ameonyesha mshikamano wake katika msimba huu akisema kwamba, kiroho yu pamoja nao.  

Telegram ya Papa ilitumwa na Katibu wa Vatican, Kardinali Pietro Parolini kwa niaba ya Papa, akilaani vikali tendo hili la kinyama dhidi ya maisha na utu wa binadamu. Licha ya unyama huo, Papa amehimiza Askofu, Mapadre na jamii kwa ujumla, kutokatishwa tamaa na uovu huu, bali wasonge mbele na juhudi zao za kutetea haki za binadamu  licha ya matatizo na hatari zinazowakabili. 

Kwa mujibu wa  mwandishi wa habari Andreas Beltramo, sababu za mauaji hayo, inaweza kuwa, mshikamano wa kanisa kwa sheria kwa sheria inayokataza biashara haramu ya dawa za kulevya , ambayo inapingwa vikali na makundi yanayoendesha biashara hiyo haramu.  Kanisa linachukiwa na wafanyabiashara hao , kwa kuwa  linaunga mkono juhudi za serikali kupambana na biashara hiyo. Na pia katika miezi ya hivi karibuni utawala wa kisiasa wa Veracruz , umekosolewa vikali kwa vitendo vya rushwa na kuifanya hali ya  maisha ya kijamii kuwa mbaya zaidi katika eneo hilo la Mexico. . 








All the contents on this site are copyrighted ©.