2016-09-21 15:14:00

Viongozi wa dini wahitimisha Siku ya Dunia ya kuomba amani


Jumanne,  majira ya jioni huko Assisi ,viongozi wa dini na mila mbalimbali walikamilisha siku tatu za tafakari na maombi kwa ajili ya amani ya dunia.

Hitimisho la Mkutano huu wa kuomba amani duniani, limerudia kutaja dhamira ya mkusanyiko huo wa wanaume na wanawake wa dini mbalimbali, katika mji wa Asssisi, kwamba, kama ilivyokuwa wakati wa kuanzishwa kwa  Siku hii  mwaka 1986, kwa mwaliko wa Papa Yohana Paulo II, hata leo hii kama viongozi wa dini wanaendelea kuienzi siku hii ya kuomba amani kwa makini zaidi, kwa ajili ya  kuthibitisha dhamana isiyoweza kutenganishwa, mema yanayofanikishwa na uwepo wa amani na  dhamiri halisi ya dini.

Na kwamba, tukio hili lililoanzishwa na kuwa sehemu ya historia ya hija ya kila mwaka kwa ajili ya kuomba amani duniani,  sasa ni  tukio linalogusa  miji mingi duniani, likiwaunganisha  bila fujo, watu  wengi  zaidi katika meza ya mazungumzo na maombi kwa ajili ya amani, umoja  na kudumisha urafiki imara zaidi  kati ya  madhehebu na dini licha ya kutofautiana kiimani, wakitafuta njia inayofaa zaidi kufanyakazi kwa pamoja, hasa katika kuizima migogoro inayojitokeza.

Viongozi wa dini wamesema,  hiyo ndiyo roho inayowahamasisha wao kukutana kwa ajili ya mazungumzo ya amani. Wanapinga aina zote za ukatili na unyanyasaji , unaotafuta  dini itumike kama kigezo cha  kuhalalisha vita na ugaidi.  Tamko linaonyesha kujali kwamba, katika kipindi cha miaka hii thelathini iliyopita,  bado kuna watu wanaotumia jina la dini kunyanyasa,  kutesa na kujeruhi wengine kivita na kigaidi. Watu ambao wameziba  kwa makusudi ufahamu wao katika kuelewa kwamba ,  vita ni  mbaya. Vita huacha urithi wa uchungu na chuki.  Na hivyom Viongozi wa dini wamerudia kutangaza kwa kishindo zaidi kwa watu wote kwamba,vita ni nuksi,  vita havina manufaa yoyote.

Kwa sababu hiyo, viongozi wa dini wanaona umuhimu wa kukusanyika pamoja na kutoa  maombi yao kwa  Mungu, kuomba  zawadi amani duniani. Na kwamba,  wanatambua haja ya kuomba mara kwa mara kwa ajili ya amani, kwa sababu maombi huilinda dunia na a,amani humulikia  njia inayofaa wote  kutembea  pamoja. Wametoa onyo  kwa wote  wanaotumia jina la Mungu kuhalalisha ugaidi na fujo  na  kivita kwamba , kufanya hivyo ni kuwa nje ya njia ya Mungu.  Kufanya vita kutumia  jina la dini, ni kuendesha vita dhidi ya dini yenyewe.  Viongozi wa dini wameeleza na kuonyesha kushawishika kwao  kwamba, vurugu na ugaidi  ni kinyume na  roho halisi ya dini.

Tamko la viongozi linaendelea kusema , wamekubali mwaliko wa kukusanyika pamoja Assisi, kwa kuwa wanaguswa na sauti ya kilio cha maskini, kilio cha watoto na kizazi kipya cha vijana, sauti za  wake kwa waume wengi, wanaokabiliwa na mateso ya  vita na uchungu wa kupoteza wapendwa wao, hivyo, wamefika Assisi kulia pamoja nao wote , kusema hapana kwa vita. Na kwamba hawezi kuziba masikio yao kwa kilio hiki uchungu na maumivu, kinachotoka kwa watu wengi wasio na hatia.

Na hivyo, viongozi hao wa kidini wametoa ombi lao kwa viongozi wa kisiasa wa mataifa, wafanye kila linalowezekana kusitisha nia zote zinazotaka kueneza vita. Na wametaja sababu msingi ya ndani yenye kuzua fujo na mapigano kwamba, kiundani ni tamaa inayodai kujilimbikizia  fedha na mamlaka, huo ni uroho wa wafanya biashara wa silaha na watu wanaotafuta maslahi kwa manufaa yao binafsi , na baadhi ni kumezwa na roho ya ulipizaji visasi,  kwa yaliyofanyika nyuma. Viongozi wa dini wameomba  uwepo wa dhamira thabiti zaidi katika kuondoa sababu za msingi zinazozua  migogoro, kama  hali ya umaskini, dhuluma na kukosekana kwa usawa, unyonyaji na upuuzaji wa maisha ya binadamu.

Viongozi wa dini walihitimisha ombi lao kwa kuomba Mwenyezi Mungu, awezeshe kufungua wakati mpya, ili dunia ya utandawazi iwe  kweli dunia yenye   familia moja tu ya binadamu,kwa kutekeleza wajibu wake msingi wa  kujenga amani ya kweli, dunia  iliyo ni makini na mahitaji halisi ya watu na ubinadamu wote. Kwa namna hiyo , itaweza zuia aina zote za migogoro na badala yake,  kujenga ushirikiano katika kushinda chuki na kuondoa vikwazo vinavyo zuia watu kukutana na kuwa na majadiliano kwa amani.  Wamesema , hakuna kinachoweza shindikana katika mazungumzo ya kweli, na hivyo wanayaelekeza maombi yao kwa Mungu , ili wote waweze kuwa wajenzi wa amani. Tokea mji huu mdogo wa Assisi, lakini maarufu katika fadhila na huruma, wanarudia upya  kutangaza dhamira yao katika kujenga dunia ya amani , kwa msaada wa Mungu, pamoja na wanaume na wanawake wote wenye mapenzi mema .








All the contents on this site are copyrighted ©.