2016-08-11 09:27:00

Makanisa ya Mashariki yanapaswa kujipyaisha daima!


Kardinali Leonardi Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki anasema, kuna haja ya kwa Makanisa ya Mashariki kusimama kidete kuhakikisha kwamba, elimu inayotolewa kwa vijana wa kizazi kipya ni bora na inakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa. Kwa miaka mingi, Kanisa limejenga utamaduni wa kuwa na waalimu waliofundwa wakafundika, tayari kurithisha elimu, maadili na utu wema kwa vijana wa kizazi kipya.

Lakini leo hii anasema Kardinali Sandri, hali inaonekana kubadilika kabisa na kuanza kuchukua sura tofauti. Wamonaki ambao walikuwa wanaheshimika sana kwa elimu, ujuzi na maarifa leo hii wanaonekana kurudi nyuma kwa kasi ya ajabu! Kutokana na mwelekeo huu, Ulaya ya Mashariki inaokena kukosa waalimu na majaalimu waliotayarishwa vyema kwa ajili ya kurithisha elimu, ujuzi na maarifa kwa vijana wa kizazi kipya!

Kardinali Sandri ametoa changamoto hii hivi karibuni alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa kawaida wa Shirika la Wamissionari wa Mtakatifu Basil wanapojiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 400 tangu kuanzishwa kwa Shirika lao, maadhimisho ambayo yatafanyika kunako mwaka 2017. Hii ni changamoto ya kurejea katika kisima cha asili yao, ili kujipyaisha kwa kusoma alama za nyakati ili hatimaye, kujibu changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Wamonaki wa Mtakatifu Bazili katika historia, maisha na utume wao, walitambua umuhimu wa elimu, wakawekeza katika sekta hii na kuwa kweli ni mfano wa kuigwa katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina kwa njia ya huduma makini ya elimu iliyomwilishwa kwa namna ya pekee miongoni mwa wakimbizi na wahamiaji kutoka Ulaya ya Mashariki waliokuwa wanaishi nchini Canada na Brazil. Wamissionari hawa wakawasaidia waamini kupata elimu bora sanjari na kudumisha maisha bora ya kiroho hata ugenini.

Kardinali Sandri anakaza kusema, katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo kuna haja ya kupyaisha mikakati ya shughuli za kichungaji, kimissionari na kijamii ndani ya Kanisa; mambo ambayo kimsingi ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa maisha wenye mvuto na mashiko. Mtakatifu Basil Mkuu alikuwa ni kiongozi mwenye upeo mpana katika maisha na utume wa Kanisa, awasaidie watoto wake kusoma alama za nyakati kwa kuinua kiwango cha ubora wa elimu inayotolewa kwa vijana wa kizazi kipya, ili iweze kuwasaidia kupambana na changamoto za maisha katika ulimwengu mamboleo.

Kardinali Sandri anawataka watawa wa Shirika la Mtakatifu Basil kuchote tena nguvu, hekima na busara za kichungaji kutoka kwa Mtakatifu Basil mkuu, aliyetambua alama za nyakati, akajifunga kibwebwe kupambana na changamoto za kijamii na maisha ya kiroho; akasimamia mafao ya wengi, ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo. Elimu iwe ni nyenzo itakayowasaidia vijana wa kizazi kipya kuambata na kuchuchumilia utakatifu wa maisha.

Watawa walioandaliwa vyema: kiroho na kimwili, hao wataweza kujikita vyema katika mchakato wa maisha ya kiroho na huduma kwa jirani katika jamii inayobadilika kwa kasi kubwa zaidi. Changamoto kubwa kwa wakati huu majiundo awali na endelevu kwa ajili ya watawa na wamonaki, ili kuweza kukabiliana na changamoto za usasa wa maisha. Shirika la Wamonaki wa Mtakatifu Basil limechangia kwa kiasi kikubwa katika maisha na utume wa Makanisa mahalia sehemu mbali mbali za dunia, mwaliko kwa sasa ni kuendelea kujipyaisha, ili wasipitwe na wakati, daima wakiwa mstari wa mbele kusoma alama za nyakati kama wanavyokaza kusema Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.