2016-08-11 10:08:00

Injili ya familia: Majiundo makini na endelevu ni muhimu!


Baraza la Maaskofu Katoliki Togo, hivi karibuni limehitimisha mkutano wake wa mwaka uliojadili pamoja na mambo mengine kuhusu malezi na majiundo ya Majandokasisi wa Seminari za Majimbo nchini humo; utekelezaji wa Wosia wa Kitume “Furaha ya upendo ndani ya familia” “Amoris laetitia” uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kama dira na mwongozo wa utume wa familia ili kuweza kukabiliana na changamoto za maisha ya utume wa familia, tayari waamini kusimama kidete kutangaza na kushuhudia Injili ya familia inayofumbata Injili ya uhai na huruma ya Mungu.

Baada ya mkutano huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Togo, linasema katika maadhimisho ya mkutano wao, wamepata nafasi kama wachungaji wakuu wa familia ya Mungu nchini Togo yak usali, kutafakari na kushirikishana mafanikio, changamoto na matatizo katika maisha na utume wa Kanisa. Wamesikiliza furaha na machungu yaliyosimuliwa na walezi wanaotekeleza dhamana yao kwenye Seminari za Majimbo na kukaza kwamba, hapa malezi yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kwa kujikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Walezi ili waweze kutekeleza vyema dhamana yao, wanapaswa pia kupata majiundo makini na endelevu ili kuweza kukabiliana na changamoto za maisha na utume wa kipadre katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kumbe, walezi wafundwe vyema ili wayafahamu mafundisho, maadili na maisha ya kiroho, tayari kuwashirikisha majandokasisi katika safari yao ya malezi, kuelekea Daraja Takatifu la Upadre, ili hatimaye, waweze kuwekwa wakfu na hivyo kushiriki utume wa Kristo Yesu kwa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu!

Walezi wametakiwa kuwa makini katika utekelezaji wa shughuli zao, ili kuhakikisha kwamba, Majandokasisi wanafundwa barabara pamoja na kusaidiwa kutambua: uzuri na utakatifu wa wito na maisha ya Upadre; magumu na changamoto zake. Wakurugenzi wa miito majimboni, wawasaidie vijana wanaojisikia kuwa na wito wa kipadre ili waweze kutimiliza lengo hili. Maaskofu kwa namna ya pekee wametoa kipaumbele cha kwanza kwa majiundo endelevu kwa walezi seminarini pamoja na kuboresha hali yao ya maisha, ili kweli waweze kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya majiundo ya viongozi wa Kanisa kwa sasa na kwa siku za usoni!

Maaskofu Katoliki Togo wanasema, Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, Furaha ya upendo ndani ya familia unahimiza kwa namna ya pekee, umuhimu wa kuwaandaa wanandoa watarajiwa katika medani mbali mbali za maisha; ili kutambua na kuthamini: uzuri na utakatifu wa Sakramenti ya Ndoa, tayari kujenga familia itakayokuwa ni shuhuda na chombo cha kutangaza Injili ya familia kwa jirani. Waamini waoneshe huruma na upendo kwa familia zinazokabiliwa na hali ngumu ya maisha pamoja na mipasuko, ili kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, waweze pia kuonja huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Wosia huu ni sehemu ya mchakato wa mwendelezo wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ambamo waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa na Mama Kanisa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Ili wanandoa watarajiwa waweze kuwa na msingi thabiti wa maisha  ya ndoa na familia, kuna haja ya kuwa na jopo la wawezeshaji wa semina za ndoa walioandaliwa barabara ili kusaidia safari ya ujenzi wa maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu kwa mwanadamu. Hapa pia Maaskofu wamekazia umuhimu wa kuboresha utume wa familia katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa kuzingatia: Mapokeo, Sheria za Kanisa na Kanuni maadili.

Baraza la Maaskofu Katoliki Togo lilikuwa likisubiri mwongozo uliotolewa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM katika mkutano wake wa kumi na saba uliofanyika nchini Angola kuanzia tarehe 18- 25 Julai 2016 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Familia Barani Afrika: Jana, Leo na Kesho kadiri ya mwanga wa Injili”. Waamini wanahamasishwa kuwajibika kikamilifu katika haki na ukweli. Familia ya Mungu nchini Togo haina budi kusimama  kidete kulinda na kutetea ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kujikita katika kanuni maadili na utu wema. Juhudi hizi hazina budi kwenda sanjari na majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho, mambo msingi yanayoweza kuimarisha umoja wa kitaifa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Togo, limeamua kwamba, Sherehe ya Ekaristi Takatifu kwa mwaka 2017 iadhimishwe kwa Ibada, uchaji na moyo mkuu, ili kutambua ukuu na utakatifu wa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, ili kuwajengea waamini utamaduni wa kumkimbilia Kristo mbele ya Sakramenti kuu, ili kumwabudu, kumwomba, kushukuru na kumtukuza. Maadhimisho haya ambayo kwa mwaka 2017 yatafanyika hapo tatehe 18 Juni, yatapaswa kuandaliwa vyema zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.