2016-08-08 09:24:00

Upepo wa maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu Amerika ya Kusini


Kanisa Amerika ya Kusini na Visiwa vya Caribbean linaadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kuanzia tarehe 27- 30 Agosti, 2016 huko Bogotà, nchini Colombia, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Upepo wa utakatifu ni changamoto kubwa wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa Kanisa Barani Amerika” Haya ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko aliyoyatoa kunako mwaka 2015 alipotembelea Chuo kikuu cha Kipapa cha Marekani kilichoko hapa mjini Roma.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yameandaliwa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Visiwa vya Caribbean pamoja na Tume ya Kipapa ya Amerika ya Kusini. Hili ni tukio ambalo litaishirikisha familia ya Mungu kutoka katika maeneo haya pamoja na wawakilishi wa mashirika ya misaada kutoka katika Nchi 22 zinazounda Shrikisho hili. Kunatarajiwa kuwepo kwa wawakilishi kutoka Vatican na Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani.

Lengo la maadhimisho haya ni kuendeleza mchakato wa kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu, kiini cha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Huruma. Walengwa zaidi ni watu wanaoishi pembezoni mwa jamii: kiroho na kimwili; watu wanaopaswa kushirikishwa matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kumbe, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu huko Bogota ni mwaliko kwa Kanisa huko Amerika ya Kusini kuunganisha sauti yake na ile ya maskini, ili kuwahudumia maskini kwa hali na mali.

Wakati wa maadhimisho haya, wajumbe watapata nafasi ya kutafakari kwa kina na mapana juu ya dhana ya huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu; matendo ya huruma: kiroho na kimwili na jinsi ya kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha ya maskini: kiroho na kimwili. Itakuwa ni nafasi kwa wajumbe kutembelea maeneo ya pembezoni mwa jamii mjini Bogota, ili kushuhudia hali halisi ya umaskini wa watu kiroho na kimwili na jinsi ambavyo Kanisa linajitahidi kujibu kilio cha maskini kwa njia ya huduma ya upendo na mshikamano. Maadhimisho haya yatafunguliwa kwa Ibada ya Misa Takatifu na hatimaye, kuhitimishwa kwa maandamano kuelekea Kikanisa cha Muujiza cha La Calera, kielelezo makini cha Mtakatifu Francisko na mwaliko wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.