2016-08-08 13:43:00

Changamoto za UN: Sheria za Kimataifa na Haki msingi za binadamu!


Askofu mkuu Bernadito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa mataifa wakati akichangia hoja kuhusiana na haki msingi za binadamu hivi karibuni alikazia kwamba, Umoja wa Mataifa ulianzishwa kwa ajili ya kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu!Umoja wa Mataifa unaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwake na miaka 50 tangu kupitishwa kwa tamko la haki msingi za binadamu. Tangu wakati huo, kumekuwepo na mafanikio makubwa katika mchakato wa kudumisha sheria za kimataifa sanjari na haki msingi za binadamu!

Utu na mshikamano wa kibinadamu ni mambo ambayo yanafumbatwa katika sheria na haki msingi za binadamu, amana ya Jumuiya ya Kimataifa inayopaswa kulindwa na kudumishwa na wote. Lengo ni kudumisha utu na heshima ya binadamu jambo ambalo ni wajibu wa kimaadili unaopaswa kuimarishwa na watu, jamii na serikali mbali mbali.

Askofu mkuu Auza anasema majadiliano haya yanafanyika wakati ambapo kuna uvunjwaji mkubwa wa haki msingi za binadamu kutokana na vita: biasharara haramu ya binadamu na viungo vyake; utumwa mamboleo; dhuluma na nyanyaso za kidini, kikabila na kisiasa pamoja na utamaduni usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu kuendelea kushika kasi miongoni mwa watu kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Matokeo yake ni wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji linalokabiliwa na changamoto mbali mbali katika nchi wahisani.

Utu na heshima ya wakimbizi na wahamiaji vinapaswa kulindwa na kuheshimiwa kwa kuzingatia haki msingi za binadamu; mambo muhimu sana katika maisha ya binadamu awaye yote! Utu wa binadamu unafumbatwa katika maisha tangu pale mtu anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake na wala si upendeleo unaoweza kutolewa na serikali au Jumuiya ya Kimataifa kwani ni sehemu ya maisha yenyewe. Katika miaka ya hivi karibuni kumeibuka dhana mpya ya haki msingi za binadamu. Kumbe, dhana ya “haki msingi za binadamu” inapaswa kuchukuliwa na kuheshimiwa katika uzito wake, vinginevyo, dhana hii inaweza kupokwa na wajanja wachache kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao.

Askofu mkuu Benardito Auza anakaza kusema, utekelezaji wa haki msingi za binadamu ni changamoto inayopaswa kutekelezwa kwa uaminifu na uwajibikaji mpana zaidi. Utekelezaji huu unahusika na ujenzi wa mahusiano ya kiraia kati ya watu, sheria na masuala ya mahakama katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Miaka 70 ya Umoja wa Mataifa imesaidia kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu hususan miongoni mwa wanyonge.

Umoja wa Mataifa unapoadhimisha kumbu kumbu hizi zote, unapaswa kutambua kwamba, bado kuna mambo mengi yanayopaswa kutekelezwa kutokana na ukweli kwamba, haki msingi za binadamu zinaendelea kuvunjwa, sera na ubaguzi vinazidi kutawala na kushamiri katika akili na nyoyo za watu. Mambo yote haya yanapaswa kufanyiwa kazi na Umoja wa Mataifa ili kujenga na kudumisha utamaduni wa kuheshimu haki msingi za binadamu pamoja na kuunda mazingira ambayo yatasaidia kwa siku za usoni kukuza, kudumisha na kuendeleza mazingira ya kulinda haki msingi za binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.